BOT, Wadau Kimataifa waipongeza Benki ya CRDB Mageuzi ya Mfumo Mkuu

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Emmanuel Tutuba (kushoto) akimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Mussa Nsekela (kulia) wakati wa mkutano wa kujadili utekelezaji wa mageuzi ya mfumo mkuu wa benki hiyo, hatua ya kimkakati inayolenga kuboresha huduma, kuimarisha usalama wa miamala na kukuza uchumi. Mkutano huo ulihudhuriwa na Manaibu Gavana wa BOT, pamoja na viongozi wengine waandamizi wa BOT na Benki ya CRDB.

====   =======   ========

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Emmanuel Tutuba ametoa pongezi kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Mussa Nsekela, akieleza kwamba mageuzi ya mfumo wake mkuu wa kibenki (core banking system) ni hatua ya kimkakati na yenye kuonyesha ukomavu wa sekta ya benki nchini. Pongezi hizo zimetolewa wakati wa mkutano maalum kati ya menejimenti ya Benki ya CRDB na BOT ambao pia ulihudhuriwa na Manaibu Gavana, na Wakurugenzi wa Benki Kuu.

Pongezi za BOT zinakuja siku chache baada ya jumuiya ya kimataifa kutoa pongezi kwa Benki ya CRDB kufuatia mageuzi ya kihistoria ya mfumo wake, mageuzi ya kimkakati yaliyolenga kuongeza ubora wa huduma, kuimarisha usalama wa miamala, na kupanua wigo wa huduma bunifu kwa wateja wake.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Makao Makuu ya Benki jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Bi. Tully Esther Mwambapa, alisema pongezi hizo zinadhihirisha imani endelevu ya wadau wa sekta ya fedha kwa Benki ya CRDB. Vile vile pongezi hizo zinadhihirisha nafasi ya Benki ya CRDB kama benki kiongozi barani Afrika katika ubunifu wa kidijitali na uthubutu wa kimaamuzi.

“Hakuna safari ya mageuzi ambayo imewahi kuwa rahisi na hivyo ndivyo ilivyokua kwa upande wetu pia. Katika kipindi cha mabadiliko, baadhi ya wateja walipata changamoto za muda mfupi, jambo ambalo ni la kawaida katika mageuzi makubwa ya mifumo. Timu yetu ya wataalamu imekuwa ikifanya kazi usiku na mchana kuhakikisha changamoto hizo zinashughulikiwa kwa haraka. Leo hii nafurahi kuwajulisha kuwa huduma zetu zimerejea katika hali ya kawaida na mabadiliko haya yaliyofanyika yamejenga msingi imara wa kutoa huduma hapa Tanzania, Burundi, DRC, Dubai ambapo tunapanua wigo wetu na masoko mengine mapya tunayoyaendea,” alisema Tully.

Tully alifafanua kuwa mageuzi hayo ya mfumo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Muda wa Kati wa Benki ya CRDB (2023–2027), ambao unaweka ubunifu wa kiteknolojia kama msingi wa ukuaji wa benki na uchumi. Mageuzi haya pia yanaonesha ustahimilivu wa benki kwa kusimamia mabadiliko makubwa katika nchi tatu (Tanzania, Burundi na DRC) huku huduma zikiendelea bila kukatika, jambo lililopongezwa na wadau wa ndani na nje ya nchi.

Hivi karibuni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, alialikwa kushiriki katika Kongamano la Biashara kati ya Marekani na Afrika (US–Africa Business Forum) lililofanyika pembezoni mwa Mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) jijini New York. Katika kongamano hilo lililohudhuriwa na viongozi wa juu wan chi wakiongozwa na Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, mageuzi ya mfumo mkuu wa kibenki yaliyofanywa na Benki ya CRDB yalitambuliwa kama mfano wa kuigwa barani Afrika na duniani. Wawekezaji walipongeza kuona Benki kutoka Afrika ya Mashariki ikipaga hatua hiyo kubwa.

Aidha, vyombo vikubwa vya habari vya kimataifa ikiwemo Bloomberg vilimualika Nsekela kuelezea mageuzi hayo, ambapo mahojiano hayo yalitoa fursa ya kuonesha namna Benki ya CRDB inavyotumia teknolojia kuboresha huduma, kuongeza usalama wa kifedha na kuwezesha maendeleo ya sekta mbalimbali za kiuchumi barani Afrika. Hii imeifanya Benki ya CRDB kuwa miongoni mwa benki chache barani Afrika zinazotajwa kwa uwekezaji madhubuti wa teknolojia katika majukwaa makubwa ya kiuchumi duniani.

Mageuzi hayo pia yamepongezwa na wadau mbalimbali. Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Elijah Mwandumbya, alisema mageuzi hayo yametoa mfano wa uongozi wa kijasiri na yameongeza kujiamini kwa sekta ya fedha nchini. Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA (ICTC), Dkt. Nkundwe Mwasaga, aliyatambua mageuzi hayo kama mabadiliko ya kimkakati yanayodhihirisha uwezo wa Tanzania kuendesha mageuzi makubwa ya kidijitali kwa ufanisi mkubwa na salama. Wataalamu wa ndani wa TEHAMA, akiwemo Nguvu Kamando wa Vodacom, waliongeza kuwa mageuzi haya yanaweka Tanzania kwenye ramani ya kimataifa kama kiongozi wa ubunifu wa kifedha.

Tully alifafanua zaidi kuwa mageuzi hayo yamefungua milango ya ushirikiano wa kimataifa, ikiwemo makubaliano yaliyosainiwa hivi kando ya mkutano wa UNGA na Shirika la Crop Trust kwa ajili ya kuimarisha usalama wa chakula kupitia kilimo stahimilivu, na makubaliano na shirika la fedha la DIFC kwa ajili ya uwezeshaji wa wajasiriamali wadogo na wakati. Aidha, Benki hiyo imesaini makubaliano ya ushirikiano wa kiteknolojia na kampuni ya kimataifa ya teknolojia Huawei kwa ajili ya kuimarisha mabadiliko ya kidijitali, usalama wa mifumo na matumizi ya akili mnemba (Artificial Intelligence).

“Ushirikiano huu ni wa kimkakati na utafungua fursa kubwa kwa wakulima wadogo kupitia teknolojia za kilimo stahimilivu, kwa wafanyabiashara kupitia huduma za kifedha zilizo salama zaidi, na kwa sekta za maendeleo kupitia ubunifu wa kidijitali na akili mnemba. Ni hatua inayoongeza ushindani wa uchumi wetu kikanda na kimataifa,” alisema Tully.

Vilevile, alisema mfumo huo mpya umeongeza uwezo wa benki hiyo kutoa huduma kwa viwango vya kimataifa kwa wateja binafsi, wafanyabiashara na makampuni, ndani ya Tanzania, Burundi na DRC, huku ukiweka mazingira thabiti ya upanuzi katika masoko mapya duniani.

“Kama mnavyotambua hivi karibuni tumepata kibali cha kufungua ofisi yetu huko Dubai, hatua ambayo inathibitisha nafasi ya Benki ya CRDB kama daraja kati ya Afrika na masoko ya kimataifa. Hii ni hatua ya kimkakati ya kuwaunganisha wateja wetu na mitaji, teknolojia na fursa mpya zinazopatikana katika masoko ya kimataifa,” aliongeza Mwambapa.

Akihitimisha mkutano huo na waandishi wa habari, Tully alisema pamoja na pongezi hizo za kimataifa, Benki ya CRDB inatambua wajibu wake wa kuendelea kuboresha huduma, kuwekeza katika ubunifu na kuhakikisha kila hatua inayopiga inaleta mageuzi chanya katika maisha ya wateja wake na kuchochea ukuaji wa uchumi. Alisema mageuzi ya mfumo si tu yanadhihirisha uthubutu wa benki, bali pia ni ishara ya uimara na uthabiti wake katika kuhimili changamoto na kuendelea kusonga mbele kwa kujiamini.