Chaumma yaahidi kuboresha usafiri, huduma za kijamii Dar

Dar es Salaam. Kutokana na nafasi kubwa ya kiuchumi ya Jiji la Dar es Salaam, wingi wa watu na uwepo wa vitega uchumi vikubwa kama bandari, Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kimeahidi kuja na suluhisho la changamoto ya usafiri jijini humo.

Chama hicho kimesema kikipewa ridhaa Jumatano Oktoba 29, 2025 kwenye uchaguzi mkuu ya kuongoza nchi, kitajenga barabara za juu za kutosha ili kupunguza msongamano wa magari unaokwamisha shughuli za kiuchumi. Aidha, mabasi yaendayo haraka maarufu mwendokasi yatatoa huduma kwa saa 24 kupitia mpango wa ubinafsishaji utakaosimamiwa na chama hicho.

Ahadi hizo zimetolewa leo Alhamisi, Oktoba 2, 2025 na mgombea mwenza wa urais wa Chaumma, Devota Minja, wakati akihutubia mkutano wa kampeni katika Kata ya Msongola, Jimbo la Kivule, mkoani Dar es Salaam.

“Chaumma tuna mkakati wa kujenga barabara za juu kama ilivyo Nairobi. Kuhusu mwendokasi, tutayabinafsisha sambamba na kuruhusu daladala binafsi kuendelea na ruti zake za mjini,” amesema Devota.

Amesema ongezeko la idadi ya watu Dar es Salaam linahitaji mipango madhubuti ya muda mrefu, akisema miaka ijayo idadi hiyo itakuwa kubwa zaidi.

Akiwa Kivule, Devota amesema amejionea changamoto za miundombinu hususan barabara zisizopitika kirahisi hasa nyakati za mvua.

“Jimbo la Kivule linakabiliwa na changamoto ya barabara zenye mashimo. Mvua zinaponyesha hali inakuwa mbaya zaidi,” amesema.

Hivyo, mgombea mwenza huyo amesisitiza kuwa yote hayo yanawezekana iwapo Watanzania wataamua kuiondoa CCM madarakani kupitia kura za Oktoba 29, 2025.

Kwa upande mwingine, Minja amewaomba wakazi wa Kivule kumpigia kura mgombea ubunge wa Chaumma, Benson Kigaila, akisema ana uwezo wa kurudisha heshima ya jimbo hilo na kuhakikisha barabara za lami zinapatikana ndani ya muda mfupi.

Akizungumzia changamoto ya ajira, Minja amebainisha kuwa ukosefu wake umewasukuma vijana wengi kuzurura mitaani na kujihusisha na michezo ya kubahatisha.

“Serikali ikiajiri vijana, itapata kodi halali kupitia mishahara yao ya kila mwezi. Katika siku 100 za kwanza, tutaanza kufufua ajira kupitia viwanda vya nguo, viatu na vinginevyo ili vijana wetu wapate kazi,” amesema.

Pia ameahidi kuwa Chaumma itawekeza katika kilimo ili kuhakikisha Watanzania wanapata chakula cha kutosha.

“Tutapunguza kodi kwenye mafuta, viatilifu, pembejeo na dawa ili watu walime. Tutaanzisha maghala ya wilaya kwa ajili ya kuhifadhi chakula ili kuwe na uhakika wa upatikanaji,” amesema.

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Kivule kupitia Chaumma, Kigaila amesema changamoto kubwa zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo ni pamoja na barabara mbovu, ukosefu wa maji safi, elimu duni na usimamizi hafifu wa taka.

“Wakati mvua zinanyesha, wananchi wanalazimika kuvua viatu na kutembea peku kutokana na ubovu wa barabara. Pia kuna migogoro ya ardhi, hasa hapa Msongola, pamoja na changamoto ya usalama kutokana na kukosekana kwa ulinzi shirikishi,” amesema.

Kigaila ameahidi kuwa endapo atachaguliwa kuwa mbunge, atahakikisha anashughulikia changamoto hizo ili wakazi wa Kivule waishi kwa amani na ustawi.