Dk Mwinyi: Msidanganyike kujitokeza siku ya kura ya mapema

Unguja. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi amewasihi wananchi wasidanganyike kujitokeza siku ya kura ya mapema kwani walengwa wanafahamika.

Kadhalika, amewataka wanachama wa chama hicho, wasibweteke kujiaminisha kuwa tayari wameshashinda, badala yake wajitokeze Oktoba 29, 2025 kukipigia kura chama hicho ili washinde kwa kishindo.

Kura ya mapema Zanzibar itapigwa Oktoba 28, 2025 ambapo kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), wanaolengwa katika kura hiyo ni askari na watendaji wa Tume ambao watakuwa na kazi maalumu siku ya uchaguzi.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni viwanja vya Jimbo la Bumbwini Mkoa wa Kaskazini Unguja, Dk Mwinyi amesema kuna baadhi ya wanasiasa wameanza kuhamasisha wananchi kujitokeza siku ya kura ya mapema, jambo ambalo ni kosa kisheria na ni njia ya kutafuta uvunjifu wa amani.

“Nimeanza kusikia kuna watu wanataka kusindikiza wapigakura siku hiyo, ndugu zangu hiyo ni dalili ya kutaka kuvunja amani, mkisikia mtu anakwambieni kutoka majumbani mwenu siku hiyo, kama wao ni hodari waache watoke wenyewe,” amesema Dk Mwinyi ambaye pia ni Rais wa Zanzibar.

Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk Hussein Mwinyi akionesha kadi za wanachama wa ACT Wazalendo waliojiunga na chama hicho katika mkutano wa kampeni Jimbo la Bumbwini



Dk Mwinyi amesema kura ya mapema ipo kisheria ambayo imetungwa na Baraza la Wawakilishi na sio matakwa ya mtu wala chama.

Licha ya kutowataja waliotoa kauli hiyo, lakini imekuwa ikitolewa na mgombea wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman kwamba siku ya kura ya mapema, watatoka kuwasindikiza wanaokwenda kupiga kura siku hiyo.

Amewasihi wanachama wa chama hicho kuendelea kuhubiri amani kila wanapopanda kwenye majukwaa ya kisiasa na kampeni zao ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Amesema suala la amani, mshikamano na umoja, ndio linatakiwa kuwa ajenda ya kudumu wakati wote wa shughuli za kisiasa na baada.

“Sisi tuhakikishe tunaendelea kuhubiri amani, na hii ndio ajenda yetu ya kudumu, na hii ndio njia pekee ya kudumisha utulivu katika nchi yetu,” amesema.

Akizungumza kuhusu kubweteka, Dk Mwinyi amesema wasijidanganye kwamba tayari wameshashinda badala yake wajitokeze kwa wingi kupiga kura.

“Ndugu zangu tusibweteke kwamba tumeshashinda, tunatakiwa tujitokeze kupiga kura,” amesema.

Ametumia fursa hiyo kueleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha kwanza cha utawala wake akiomba ridhaa nyingine ili wafanye mambo makubwa zaidi ya hayo.

Amesema katika sekta ya elimu wamefanya makubwa kwa kujenga shule za kisasa, kuweka miundombinu mizuri na tayari tija imeanza kuonekana kwa ufaulu kuongezeka.

Kwa upande wa afya, amesema baada ya kujenga hospitali za wilaya 11, wakirejea madarakani watajenga hospitali za mikoa ambapo mkakati huo tayari umeanza.

“Kwa upande wa sekta ya maji, tumejenga matanki makubwa yanayozalisha lita za maji milioni moja, lakini tunataka tukirejea madarakani huduma hizi ziongezeke zaidi,” amesema Dk Mwinyi.

Akizungumza fidia ya wananchi waliopisha mradi wa Bandari jumuishi ya Mangapwani, Dk Mwinyi amesema tayari Serikali imetoa Sh11 bilioni na imejenga nyumba zaidi 300 ambazo iwapo kuna watu hawatataka kupewa fedha watawekwa kwenye nyumba hizo.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Mohamed Said Dimwa, amesema Dk Mwinyi amebadilisha nchi katika mambo makubwa kutokana na maono yake aliyonayo.

Mkazi wa Bumbwini Masoud Amour Masoud amesema katika kipindi cha miaka mitano wanajivunia mafanikio makubwa waliyoyapata ambavyo hayakuwahi kutokea akitaja katika sekta ya afya, miundombinu na elimu

“Bumbwini tuna mradi wa nyumba zaidi ya 300 zimejengwa hapa kwa ajili ya fidia, tuna bandari jumuishi Mangapwani, shule za ghorofa mbili na barabara sita za lami, haya hatukuwahi kuyashuhudia,” amesema