Dk Tulia aja na ahadi ya maboresho ya Tazara akitaja fursa muhimu kiuchumi

Mbeya. Mgombea ubunge wa Jimbo la Uyole kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Tulia Ackson amesema Serikali imeandaa mkakati maalum wa maboresho makubwa ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) kwa lengo la kuchochea fursa za kiuchumi kwa wananchi.

Dk Tulia ameyasema hayo leo Alhamisi, Oktoba Mosi, 2025, wakati wa mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya Makondeko, Kata ya Igawilo, aliko mnadi pia mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan.

“Ndugu zangu wa Igawilo, Serikali ya CCM ndiyo yenye dhamana ya kusimamia Ilani ya uchaguzi. Ninaposema Samia mitano tena namaanisha aendelee kutenga mabilioni ya fedha kwa ajili ya maendeleo, akishirikiana na mimi mbunge wenu niliyetulia,” amesema.

Ameeleza kuwa maboresho ya reli hiyo yataleta manufaa makubwa kwa wafanyabiashara wa Tanzania na Zambia, ikiwamo kurahisisha usafirishaji wa bidhaa kwenda mataifa mbalimbali.

“Ilani ya uchaguzi imeweka mwelekeo wa safari ya miaka mitano ijayo. Niwasihi mkaende kupiga kura Oktoba 29, kwa sababu hiyo ni haki yenu ya msingi na itawapa nafasi ya kufuatilia utekelezaji wa miradi hii,” amesisitiza.

Akizungumzia uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, Dk Tulia amesema mgombea urais wa CCM, Samia ameahidi ndani ya siku 100 baada ya uchaguzi, atatenga Sh200 bilioni kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali wadogo.

Amesema fedha hizo zitawanufaisha wauza vyakula, mboga mboga, madereva bajaji na bodaboda pamoja na makundi mengine ya vijana na wanawake.

“Lengo ni kuwasaidia kuwa na miradi endelevu ya kujikwamua kiuchumi, hususan kwenye sekta ya kilimo kwa kuweka mazingira wezeshi yenye masoko ya uhakika. Lakini yote haya yatafanikiwa iwapo mtapiga kura kwa CCM Oktoba 29, 2025,” amesema mgombea ubunge huyo.

Kwa upande wa huduma za afya, Dk Tulia amesema Serikali ina mpango wa kujenga vituo vipya vya afya katika Jimbo jipya la Uyole, hususan Kata ya Igawilo kama sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa miaka mitano ijayo.

Aidha, amesema sekta ya kilimo imepewa kipaumbele na Serikali imedhamiria kujenga miundombinu ya umwagiliaji ili kuongeza tija kwa wakulima, hasa wa mboga mboga katika Bonde la Uyole.
Amesema endapo atachaguliwa, atahakikisha viwanja vya Nanenane vinajengwa ghala kubwa la kuhifadhia mazao kabla ya kupelekwa sokoni, sambamba na kuhakikisha mbolea ya ruzuku na pembejeo zinapatikana kwa wakati.

Kwa upande wake, mkulima wa viazi mviringo kutoka Kata ya Simambwe, Sikujua Mwaikambo ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa mkakati wake wa kuinua sekta ya kilimo.
“Tumesikiliza sera za mgombea wetu wa Ubunge, Dk Tulia na tunaona wazi dhamira ya Serikali katika miaka mitano ijayo ni kusaidia Watanzania kuondokana na umaskini, jambo ambalo limekuwa matarajio yetu kwa muda mrefu,” amesema.