Hitilafu ya umeme chanzo moto ulioteketeza Soko la Kawe

Dar es Salaam. Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limetaja chanzo cha moto ulioteketeza Soko la Kawe na hitilafu ya kifaa cha umeme.

Moto huo ulizuka usiku wa kuamkia Septemba 15, 2025.

Akizungumza na Mwananchi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Dar es Salaam, Peter Mabusi, amesema matukio ya moto yanayojirudia mara kwa mara jijini humo kwa kiasi kikubwa yanasababishwa na uzembe wa watumiaji, pamoja na matumizi yasiyo sahihi ya vifaa vya umeme.

Amefafanua uchunguzi kuhusu moto huo ulibaini kuchomekwa kifaa cha umeme kwenye swichi na kuachwa bila kuzimwa na kusababisha shoti ilipelekea kuzuka kwa moto huo.


 “Hivi karibuni Kawe kulitokea moto kwa sababu mtu aliacha ‘extension’ imeunganishwa kwenye soketi bila kuizima. Ikaendelea kupata joto na kusababisha moto. Huu ni uzembe mdogo, lakini madhara yake ni makubwa,” amesema Mabusi.

Jeshi la Zimamoto limeendelea kusisitiza kuwa uchunguzi kama huu ni muhimu ili kutoa elimu kwa wananchi kuhusu tahadhari za umeme na kuzuia majanga yanayoweza kusababisha vifo au hasara kubwa. Mabusi ameonya kuwa hata vifaa vidogo vya nyumbani vinaweza kusababisha moto mkubwa ikiwa havitatunzwa vizuri.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam , Albert Chalamila baada ya tukio hilo Septemba 15,2025 alitoa agizo la kutolewa kwa Sh100 milioni kwa wafanyabiashara waliokuwepo katika soko hilo ambao walitajwa idadi yao kuwa ni 1,000.

Mbali na hilo, alisema wafanyabiashara hao wahamishiwe katika uwanja wa Tanganyika Packers wakati soko hilo likiwa linajengwa upya na kuwa soko la kisasa lenye mpangilio.

Wafanyabiashara walitaka kuanza ujenzi wa vibanda vyao katika eneo hilo jipya, lakini Chalamila aliwataka kusubiri ili kujengwa kwa soko zuri na lenye mpangilio tofauti na lililoungua.

Akizungumza na Mwananchi leo Oktoba 2, 2025 Katibu wa soko hilo, Silvester Chedego amesema pesa hizo zitatolewa kwa wafanyabiashara hao baada ya kuhamia kwenye soko jipya.

“Kuhusu Sh100 milioni watu watakapohamia katika soko jipya ndiyo watafanya mchakato wa kuwakabidhi na idadi kamili ya wafanyabiashara itatolewa baada ya baadhi ya vitu kukamilika,” amesema.

Pia, amesema ujenzi wa soko la Tanganyika Packers walielezwa utakamilika ndani ya wiki nne tangu kutangazwa kuhamia hapo Septemba 15, hivyo matarajio yao hadi kufikia Oktoba 16 mwaka huu litakuwa limekamili.


Kwa upande wake, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya soko la Kawe lililoungua, Ibrahimu Waziri amesema wafanyabiashara wanaofanya shughuli za utengenezaji tayari wameanza kufanya kazi zao pembeni ya soko jipya, linalojengwa katika viwanja vya Tanganyika Packers.

“Wale wa kutengeneza, mfano mafundi, wao wameomba nafasi pembeni ya soko jipya kutokana na shughuli zao kuhitaji nafasi kubwa tofauti na wengine, na tayari wameanza shughuli zao huko,” amesema Waziri.

Amesema kwa upande wa wafanyabiashara wa bidhaa za kawaida, wameendelea na biashara zao pembezoni mwa barabara zinazozunguka soko lililoungua wakati ujenzi ukiendelea.

“Wafanyabiashara wengine wadogowadogo wapo pembezoni mwa barabara karibu na soko lililoungua, wanaendelea na shughuli zao kama kawaida,” amesema.


Waziri amesema wafanyabiashara wote waliopoteza biashara zao kutokana na janga hilo wameshajiandikisha kwenye orodha rasmi.

“Wote wameshajiandikisha ili kuhakikisha kila mmoja anahesabiwa na kushirikishwa kwenye mipango ya soko jipya,” amesema.