Ibenge kuongeza nguvu eneo la mbele Azam FC

KOCHA wa Azam FC, Florent Ibenge amesema moja ya kipaumbele chake katika kipindi cha mapumziko ya kalenda ya FIFA ni kuimarisha safu ya ushambuliaji na kurekebisha nidhamu ya timu hiyo katika kulinda mpira, baada ya kasoro hiyo kuwagharimu dhidi ya JKT Tanzania.

Katika mechi hiyo, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, iliisha kwa sare ya bao 1-1, matokeo yaliyomnyima Ibenge na kikosi  hicho nafasi ya kupanda juu katika msimamo wa ligi.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ibenge alisema: “Tulicheza vizuri dhidi ya JKT Tanzania, tulitengeneza nafasi, lakini tatizo lililotuangusha ni kushindwa kuuficha mpira. Tulipokuwa mbele tulipaswa kuwa na umakini zaidi, kuusambaza mpira kwa utulivu na kupunguza presha ya wapinzani. Lakini hatukufanya hivyo na tukalipa gharama kwa kuruhusu bao la kusawazisha.”


Kocha huyo raia wa DR Congo amesisitiza, anataka kuona Azam ikicheza soka la ubora unaoendana na matarajio ya klabu hiyo, akieleza mapumziko haya ya kimataifa ni nafasi bora ya kufanya marekebisho ya kiufundi.

“Tunapaswa kuwa bora zaidi kwenye safu ya ushambuliaji. Ni kweli tumefunga magoli katika mechi zetu, lakini nafasi nyingi zimepotea. Nimewaeleza washambuliaji wangu kuwa wanapaswa kuwa na ubora wa mwisho, kila nafasi ni lazima kuwa na maana,” alisema Ibenge.

Azam inakwenda mapumziko ikiwa na pointi nne, baada ya kushinda mechi moja dhidi ya Mbeya City kwa mabao 2-0 na kutoa sare dhidi ya JKT Tanzania. Matokeo hayo yanaifanya timu hiyo kushika nafasi ya tano katika msimamo wa ligi inayoongozwa kwa sasa na Simba yenye pointi sita kama ilizonazo Singida Black Stars zikitenganishwa na uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.


Baada ya kalenda ya FIFA, Azam itakuwa na mechi mbili ngumu za kuwania nafasi ya kutinga makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika Oktoba 18 na 25 kwa kucheza dhidi ya KMKM ya viswani Zanzibar.