Dar es Salaam. Ili kuendelea kuimarisha mwingiliano wa kibiashara kati ya Kenya na Tanzania, vikwazo vinne vya kibiashara visivyo vya kiushuru vimeondolewa.
Vikwazo hivyo ni kati ya vile 14 vilivyojadiliwa jana Oktoba mosi, 2025 katika mkutano wa tisa wa kamati ya pamoja ya biashara baina ya nchi hizo, huku vikwazo 10 vilivyobakia vikitarajiwa kutatuliwa ifikapo Machi 31, 2026.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk Hashil Abdallah wakati wa mkutano huo uliofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Nchi hizo zimeondoa kikwazo cha usafirishaji wa mbegu baada ya hati ya makubaliano kusainiwa, tozo za barabara kwa kutoza dola za Marekani 10 kwa kila Kilomita 100, kuondoa masuala ya bima ya Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (Comesa) kwa kuwa haihusiani na Tanzania.
Akizungumza baada ya kufikia muafaka huo, Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk Hashil Abdallah amesema watahakikisha biashara kati ya Tanzania na Kenya inafanyika kwa haki, kwa kuzingatia mikataba ya Afrika Mashariki.
Ili kufanikisha hilo, tayari imeundwa Kamati ya Ufundi ya Pamoja (JTC) itakayosimamia utekelezaji wa mabadiliko hayo.
“Lengo letu ni kuhakikisha hakuna mfanyabiashara anayekumbana na urasimu usio wa lazima. Tanzania ni lazima ionekane kuwa sehemu salama, yenye uhakika na rafiki kwa ufanyaji wa biashara. Tunataka Jumuiya nzima ya Afrika Mashariki ionekane kama ukanda salama wa kufanya biashara,” amesema.

Amesema kati ya vikwazo 14 vilivyotajwa kama kero kubwa, vinne tayari vimeondolewa na 10 vimesalia.
Amesema vikao vya mapitio vitafanyika mara kwa mara ili kuona kila sekta na wizara inatimiza wajibu wake ndani ya muda uliowekwa.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Carolyne Kalugha amesema hatua hiyo ni kubwa tayari imeweza kufanikisha suluhu kwa asilimia 78.
“Hii ni ishara ya dhamira thabiti za Serikali zote mbili,” amesema Kalugha.
Amesema mafanikio hayo yanatokana na makubaliano yaliyowekwa wakati wa ziara rasmi ya Rais wa Kenya, William Ruto, nchini Tanzania Oktoba 9–10, 2022.
“Leo hii tunaweza kujivunia kwamba tumeanza kufunga masuala yaliyodumu kwa muda mrefu na kutoa suluhu. Hii siyo kwa manufaa ya Tanzania na Kenya pekee, bali ni kwa ustawi wa Jumuiya nzima ya Afrika Mashariki,” amesema.
Katibu Mkuu wa Biashara katika Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda nchini Kenya, Regina Ambam amesema makubaliano hayo ni hatua muhimu katika mageuzi ya biashara ya kikanda.
“Biashara kati ya Kenya na Tanzania ni muhimu kwa ustawi wa wananchi wetu. Changamoto yoyote inayojitokeza katika moja ya nchi hizi huathiri Afrika ya Mashariki nzima. Kwa kuondoa vikwazo na kurahisisha mifumo, tunaunda mazingira bora kwa wafanyabiashara wetu na kwa ukanda mzima,” amesema.
Alitumia nafasi hiyo kuwasisitiza watu wa pande zote mbili juu ya umuhimu wa kujiandaa kwa biashara ya kidijitali na fursa mpya katika uchumi wa dunia.
“Makubaliano haya yanaonyesha dhamira yetu ya kuboresha biashara na kuiweka Afrika Mashariki katika nafasi ya ushindani duniani,” amesema.
Oktoba 10, 2025 Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Kenya, William Ruto walitoa maagizo kwa mawaziri wa uwekezaji kuhakikisha kuondoa vikwazo hivyo 14 vya biashara baina ya nchi hizo.