KHAMIS FAKI MGAU: Akishinda urais Zanzibar asiyeoa wake wawili jela

Wanaume kuoa kuanzia wake wawili hadi wanne, nani angewaza kuwaza inaweza kuwa agenda ya uchaguzi ya mgombea urais yeyote? Michuano ya kidemokrasia huchagiza mawazo anuwai. Khamis Faki Mgau, ameamua kutumia ndoa za mitala kama gia yake ya kuwashawishi Wazanzibari wamchague kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

“Vijana wakae tayari, mimi nikiwa Rais, ndani ya Zanzibar, kwanza ni marufuku kijana yeyote kumiliki mke mmoja. Tunaanza na wake wawili kwenda mbele. Na kijana ambaye hataoa wake wawili ni kifungo cha miaka sita jela,” anasema Mgau na kufafanua kuwa akiwa Rais wa Zanzibar, Mzanzibari mwenye umri wa miaka mitano na kuendelea, atalipwa mshahara, na kima cha chini ni Shilingi 900,000. 

Chama cha NRA (National Reconstruction Alliance), ndicho kimemsimamisha Mgau kuwa mgombea urais Zanzibar. Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), ikamteua na kumthibitisha kuwa mgombea urais. Sasa hivi, Mgau yupo kazini akisaka uungwaji mkono ili kutimiza malengo yake kushinda urais, ili aboreshe maisha ya Wazanzibari wenzake.

Jeuri ya Mgau ni kwamba Zanzibar chini ya uongozi wake, maisha yatakuwa mazuri, uchumi utakuwa mkubwa, watu watakuwa na fedha za kutosha, ndiyo maana haoni sababu ya kijana Mzanzibari kuendelea kumiliki mke mmoja, wakati atakuwa na uwezo wa kuhudumia hadi wake wanne. Kutaka Wazanzibari wathamini hali bora ambayo atawatengenezea akiwa madarakani, basi atawapeleka jela wote watakaong’ang’ana na mke mmoja.

Hii si mara ya kwanza Mgau kuwania urais wa Zanzibar. Uchaguzi Mkuu 2020, Mgau pia alikuwemo kwenye ushindani. Tena kwa tiketi ya chama chake hichohicho, NRA. Mwaka 2020, baada ya NRA kumthibitisha kuwa mgombea urais, ahadi ya kwanza ya Mgau ilikuwa kuweka kambi Pemba ili kumwonyesha aliyekuwa Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, marehemu Seif Sharif Hamad, kuwa kisiwa hicho hakikuwa mali yake.

Wakati huo, Mgau alisema: “Kwa miaka mingi sasa, yule bwana (Seif), anajiona ile Pemba ni yake. Sasa, mimi nimeamua, kwenye kampeni zangu za mwaka huu, nitaweka kambi Pemba ili niwakomboe Wapemba na siasa za Seif.”

Februari 17, 2021, Seif alipokea wito wa mauti na sasa hagombei. Mgau naye malengo yamebadilika, kwa sasa anajielekeza katika ndoa za mitala, Wazanzibari waone zaidi, wazaliane.

Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025, Mgau anasema kuwa ana uhakika atapata matokeo mazuri, kwani Wazanzibari wenzake wanamwelewa. Anaamini kuwa yeye ndiye mgombea ambaye anazungumza lugha inayotakiwa ndani ya visiwa hivyo. Anaomba uchaguzi uwe mzuri na wenye amani. Siku ya uchaguzi, wananchi wajitokeze kwa wingi kupiga kura, na baada ya kumaliza kuchagua viongozi wanaowataka, warudi nyumbani kwa usalama.

Kwa Mgau, kipimo cha maendeleo ya Zanzibar ni Dar es Salaam. Mgau anataka kuona Zanzibar inasheheni madaraja ya juu yenye kupitisha magari (flyovers), kama ilivyo Mfugale na Chang’ombe, Barabara ya Nyerere na Daraja la Kijazi, katika makutano ya Barabara za Morogoro na Mandela, Ubungo. Mgau anasema anataka kuifanyia Zanzibar mambo makubwa kuliko hayo.

Zanzibar ya sasa, chini Rais Hussein Ali Mwinyi, imepiga hatua kwa kujenga madaraja ya juu ya Mwanakwerekwe na Aman, kusaidia kuondoa foleni. Pamoja na hivyo, Mgau anasema Zanzibar kwa sasa imekuwa na magari mengi na mji ni mdogo, matokeo yake foleni zimekuwa kubwa.

Na kwa namna anavyoona, suluhu ni kuiwezesha kuwa na barabara za juu nyingi kadiri iwezekanavyo. Anaendelea kueleza kwamba kama kuna eneo atalifanyia vizuri yeye akishakuwa Rais wa Zanzibar, basi ni ujenzi wa miundombinu.

Mgau ni Makamu Mwenyekiti wa NRA Zanzibar. Asili yake ni Pemba, lakini kwa sasa anaishi Unguja kwa sababu za kikazi. Pamoja na ahadi ya kulipa mshahara kila mwezi kwa Mzanzibari yeyote kuanzia umri wa miaka mitano, vilevile anaahidi posho kwa kila mtoto, hata yule wa siku moja.

Juni 12, 1978 ndiyo tarehe aliyozaliwa Mgau. Mahali alipokulia ni Kangagani, Wilaya ya Wete, Pemba. Ni mtoto wa nne kati ya watoto tisa wa familia ya mzee Faki Mgau Haji na mama Kame Hamis Saleh. Wote ni wenye asili ya Pemba.

Mgau alianza darasa la kwanza mwaka 1989, Shule ya Msingi Kangagani, iliyopo Wete, Pemba. Alisoma hapo mpaka alipohitimu kidato cha nne mwaka 2000 katika shule hiyohiyo ya Kangagani. Baada ya kuhitimu kidato cha nne, hakuendelea na masomo, badala yake alianza kujishughulisha na siasa.

Maisha ya kisiasa na harakati zote, Mgau alianzia chama cha TLP (Tanzania Labour Party), alichojiunga nacho mwaka 2000 kwa kuvutiwa na siasa za aliyekuwa mwenyekiti wake, Augustino Lyatonga Mrema.

Kati ya mwaka 2000 na 2004, Mgau alikuwa mwanachama wa kawaida. Mwaka 2004, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa TLP wa Wilaya ya Wete.

Mwaka 2005 wakati wa Uchaguzi Mkuu, Mgau alikosa imani na TLP, kwa hiyo alikihama chama hicho na kujiunga na Chadema (Chama cha Demokrasia na Maendeleo). Sababu ya kuchukua kadi ya Chadema, ilikuwa imani kuwa chama hicho kingepata matokeo mazuri kwenye Uchaguzi Mkuu 2005.

Kile ambacho chama hicho kilivuna kwenye uchaguzi, kilimfanya Mgau atafakari na kupata jibu kwamba alitakiwa kutafuta chama kingine. Ni hapo alichagua NRA.

Mwaka 2006, Mgau aliwaaga Chadema baada ya kuwa nao kwa mwaka mmoja, kisha akatua NRA. Mwaka huohuo, Mgau alichaguliwa kuwa Katibu wa NRA, Mkoa wa Kaskazini, Pemba.

Kazi ambayo Mgau aliifanya Mkoa wa Kaskazini, iliwavutia wanachama wa chama hicho Pemba yote, hivyo kutamani kumpa majukumu makubwa zaidi.

Mwaka 2007, Mgau alichaguliwa kuwa Mratibu wa NRA Pemba nzima. Akiwa mratibu wa chama Pemba, si tu kwamba alifanikiwa kukijenga chama, bali pia alijitengeneza yeye binafsi. Ulipowadia Uchaguzi Mkuu 2010, wana-NRA wa Kojani, Wilaya ya Wete, Pemba, walimpitisha kwa kauli moja kuwa mgombea ubunge, Jimbo la Kojani.

Katika uchaguzi huo, Mgau alitoka wa tatu. Mshindi wa ubunge Kojani alikuwa mgombea wa CUF, wakati CCM walitoka wa pili. Hiyo ilikuwa alama kuwa Mgau, aliiwezesha NRA kuwa chama cha tatu jimbo la Kojani, baada ya CUF na CCM.

Baada ya Uchaguzi Mkuu 2010, Mgau aliendelea na nafasi yake ya uratibu wa NRA Pemba. Mwaka 2015, alirejea ulingoni, akagombea tena ubunge jimbo la Kojani. Na kama ilivyokuwa mwaka 2010, alitoka wa tatu, nyuma ya wagombea wa CUF na CCM.

Mwaka 2017, wakati wa Uchaguzi Mkuu wa NRA, Mgau aliona anatosha kuongoza nafasi kubwa zaidi, kwa hiyo akachukua fomu ya kugombea umakamu mwenyekiti Zanzibar. Ulipowadia mkutano mkuu, wajumbe walimchagua kwa kura za kishindo.

Mgau ni mume wa Hazala Hassan Khamis. Anasema kuwa mbali na kujenga barabara za juu Zanzibar, kubwa zaidi anakusudia kuiongoza nchi vizuri kuliko Rais yeyote aliyepata kuviongoza Visiwa vya Karafuu. Anachoomba ni Wazanzibari kumwanini na kumpa nafasi hiyo kubwa ili wafurahie uongozi wake bora.

Mgau anasema kuwa anazijua changamoto nyingi za Zanzibar, kwa hiyo endapo atashika madaraka ya urais wa Zanzibar na uenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, atahakikisha kila changamoto iliyopo inatatuliwa na Wazanzibari wanaishi kwenye ardhi yao kwa raha mustarehe.

Kingine ambacho Mgau anasema atakifanya ni kuboresha maisha ya wafanyakazi. Anasema kuwa atapandisha mishahara ya watumishi wa umma ili kuwawezesha kujenga maisha yao na familia zao.

Mkazo mwingine wa Mgau ni kwenye sekta ya usafiri wa anga. Anasema atahakikisha Zanzibar inakuwa na ndege kubwa zenye uwezo wa kubeba watu 250 na kuendelea ili kuichangamsha sekta ya utalii.

Mgau anasema kwa msisitizo kuwa atasimamia kwa amani akiwa Rais wa Zanzibar na wakati wote wa kampeni zake, pamoja na sera zake, lakini atatumia muda mrefu kuhubiri amani kwa sababu hilo ndilo la muhimu.