Arusha. Maboresho ya mfumo wa utoaji na usimamizi wa leseni za madini, yanatajwa kupunguza vitendo vya urasimu kwa wawekezaji na wachimbaji hapa nchini.
Hayo yamebainishwa leo Alhamisi Oktoba 2, 2025 jijini Arusha na Mkurugenzi wa Huduma za Sheria kutoka Tume ya Madini, Francis Kayichile wakati akizungumza katika mafunzo maalumu ya mfumo wa utoaji na usimamizi wa leseni za madini kwa maofisa leseni kutoka mikoa ya kimadini nchini.
Amesema mfumo wa sasa ulioboreshwa utapunguza mianya ya watu wengine kutumia vibaya nafasi zao na kuchelewesha waombaji kupata leseni kwa wakati.
“Kwa sasa waombaji wakiomba leseni wanaweza kuipata ndani ya siku tatu wakitimiza vigezo, tofauti na ilivyokuwa awali ambapo walikuwa wakitumia kati ya siku saba hadi 14 kupata leseni hizo. Tunataka kufikia malengo ya kuona mchakato huu wa utoaji leseni kusiwepo na mianya ya watu wengine kutumia vibaya nafasi walizonazo.
“Tumeona tukae pamoja maofisa leseni kutoka mikoa isiyopungua 30 ya kimadini ili tupeane mafunzo ya namna ambavyo hizi taratibu zinafanyika kupitia maboresho yaliyofanmyika katika mfumo wa utoaji na usimamizi wa leseni, ili tumrahisishie Mtanzania au mwekezaji anayekuja kuomba leseni asione urasimu,” amesema.
Amesema kupitia mafunzo hayo washiriki hao watapata fursa ya kujifunza na kujadili masuala yanayohusiana na maboresho, sambamba na utaratibu mzima wa namna ya kuchakata maombi ya leseni za madini.
“Nitumie nafasi hii kuwakumbusha kutumia muda huu wa mafunzo kujadili na kuweka mikakati ya kusafisha taarifa za leseni katika mfumo wa utoaji wa usimamizi wa leseni (data cleaning), ili kuwa na taarifa sahihi,” ameongeza.
Amesema ukusanyaji wa maduhuli hauwezi kufanikiwa endapo shughuli za utoaji wa leseni za madini hautafanyika kikamilifu na kwa ufanisi.
“Ni wazi kuwa hakuna mradi wa madini utaendeshwa pasipo kuwa na leseni za madini. Hata hivyo utoaji wa leseni za madini usiozingatia utaratibu unaweza kuwa chanzo cha migogoro ambayo inaweza kuzorotesha shughuli,” amesema.
Awali, Mkurugenzi wa leseni kutoka Tume hiyo, Mhandisi Aziza Swedi amesema wameona umuhimu wa kukutana na maofisa hao wanaoshughulikia uchakataji na utoaji wa leseni kwa lengo la kujadili kwa pamoja changamoto wanazopitia wakati wa uchakataji na utoaji wa leseni.
“Kama tunavyoelewa kitu kinachofanyiwa maboresho lazima kuna changamoto katika utekelezaji wa majukumu yake, tuliona ni muhimu kukutana pamoja na kuzitatua ili tuboreshe utendaji kazi na ufanisi katika utoaji wa leseni ili wawekezaji wapate huduma bora,” amesema.
Amesema utoaji wa leseni na mifumo iliyoboreshwa imesababisha Wizara ya Madini kwa kipindi cha mwaka 2024/25 ilipangiwa kukusanya Sh999 bilioni ila walivuka lengo na kukusanya zaidi ya Sh1.07 trilioni.
Mjiolojia kutoka Mkoa wa Songwe, Gworge Mchiwa amesema maboresho ya mfumo huo yamewawezesha kufanya kazi bila changamoto, na kuwa mfumo waliokuwa wakitumia awali ulikuwa na changamoto katika baadhi ya vipengele.
“Mafunzo haya yatasaidia kuboresha utendaji kazi na tunakumbushana wajibu wetu bila kukiuka taratibu na sheria na kwa sasa maboresho ya mfumo yanasaidia waombaji kupata leseni zao kwa wakati,” amesema.
“Na tutaenda kutoa mafunzo kwa wachimbaji ili watimize takwa la kisheria na kuongezea Serikali pato na ni muhimu wachimbaji kutochimba kiholela,” amesema.