KATIKA kipindi hiki ambacho ndani ya Yanga kuna presha kubwa inapelekwa na mashabiki wa timu hiyo wanaodai hawamuelewi Kocha Mkuu, Romain Folz, taarifa mpya ni kwamba upande wa viongozi nao wameanza kuvutana.
Ukiangalia kwa nje, sakata la hatma ya Folz bado linakosa picha yenye utulivu baada ya kuibuka mijadala tofauti juu ya mustakabali wa kocha huyo.
Folz hajapoteza mechi yoyote ya mashindano na sio hicho tu, pia timu hiyo haijaruhusu nyavu zake kutikiswa, lakini ikatoa sare isiyo na bao katika mechi ya mwisho ya Ligi Kuu Bara kucheza ugenini dhidi ya Mbeya City.
Sare hiyo ndio ikatibua zaidi, kwani mashabiki waliokuwa karibu na jukwaa kuu pale Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya wakaanza kupeleka presha kwa mabosi wao wakitaka wafanye maamuzi ya kumuondoa Mfaransa huyo.
Presha hiyo ya mashabiki, ni kama imeanza kuwaingia baadhi ya mabosi wa klabu hiyo ambao wamegawanyika baadhi wakiona kama wanatakiwa kufanya mabadiliko ya kuishia njiani na kocha huyo raia wa Ufaransa.
Hata hivyo, kundi hilo bado linashindwa kwenda mbali likikutana na wengine wakiona ni kama mapema kufanyika kwa maamuzi hayo kutokana na sare ambayo imewavunja nguvu wengi ilichangiwa na uwanja mbovu.
Kundi ambalo linataka Folz ang’olewe linadai ni vyema uamuzi huo ukachukuliwa haraka, ili kikosi hicho kipate muda wa kukaa na kocha mpya wakati huu ambao Ligi Kuu Bara imesimama.
“Huyu kocha anatupa mashaka ni vile hatuna maamuzi ya mwisho, timu yetu haichezi kama zamani na hatuoni mwanga kwamba hayo yatabadilika, ndio maana tunashauru ni bora wakati huu ligi inasimama tumlete kocha mwingine akae na timu atengeneze timu ityakayocheza kwa kuturidhisha,” amesema bosi huyo ambaye ni mjumbe wa kamati ya utendaji.
Mwanaspoti imeingia ndani ya Yanga na kumpata bosi mmoja wa juu kati ya watatu wanaofanya maamuzi makubwa akisema bado akili yao kwa sasa ipo na Folz.
Bosi huyo ambaye akaenda mbali zaidi, akisema Yanga ni klabu inayoweza kuwasikiliza mashabiki na hata ushauri wa wadau wengine, lakini hatma ya kocha huyo haitafanyika kwa haraka kwa presha ambayo inaendelea sasa.
“Hii klabu ina uongozi makini sana kaka, tunakubaliana kuna hiyo presha, lakini ukiwa kiongozi unaongoza klabu yenye watu wengi kama hawa basi lazima maamuzi yako yawe yenye kuzingatia mambo mengi na sio tu kwasababu watu baadhi wanaona kocha hafai,” amesema bosi huyo.
“Ukiniuliza mimi naona hatuna sababu kubwa sana ya kufanya hayo maamuzi, hebu nikuulize hivi Yanga imewahi kuwa na mechi rahisi dhidi ya Mbeya City? Utaweza kufanya kitu sawasawa kwenye uwanja kama ule? ukipata majibu utaona unahitajika kutulia kuona sababu sahihi itakayokupeleka kukubaliana na mtazamo wa watu.
“Kila mmoja anatamani timu ishinde, hata huyo kocha na sisi viongozi, tunawasikia mashabiki, hatuwapuuzi, tunasikiliza pia ushauri wa watu wengine na baada ya hapo tunachuja yote na kupata msimamo mmoja , ninachokwambia kocha bado yupo muacheni aendelee na kazi yake.”
Akizungumzia kiwango cha timu hiyo, Folz amesema hana presha yoyote kwani bado timu ipo imara na kwamba muda si mrefu utafika kikosi chake kitacheza kwenye kiwango cha juu.
Folz amesema suluhu waliyoipata dhidi ya Mbeya City ilitokana na ubovu wa uwanja ambao anaamini hata zingetoka timu Ulaya zisingeweza kupata pointi ambayo wameipata.
“Ni matokeo ya soka ambayo tumeyapata, sina shida na wachezaji wangu walijituma sana kuitetea timu lakini wakati tunaishambulia Mbeya, uwanja nao ukawa unasaidia kutukaba, sisi (Yanga) tumepata pointi mnoja lakini naamini kwa hali ya uwanja ule hata ingetoka klabu kubwa Ulaya isingeweza kupata ambacho tulipata,” amesema Folz.
“Ligi bado ndio kwanza tumecheza mechi ya pili msimu huu, nani anajua kipi kitatokea huko mbele, inawezekana mwingine asione faida ya timu kucheza kwenye uwanja mzuri lakini mimi kama kocha na wachezaji tunajua faida ya kucheza kwenye uwanja mzuri, ile ilikuwa sehemu ya kupata historia mpya kwenye maisha yangu kwa uwanja ule, tutarekebisha.
“Kitu muhimu nataka kusema ni kwamba, utafika wakati Yanga itacheza kwenye kiwango bora ambacho tunataka, tutafika hapo sio muda mrefu tunafanya kazi kwa nguvu ili tufikie hapo.”
Tangu Folz atue Yanga akimpokea Miloud Hamdi, ameiongoza timu hiyo katika mechi 10 zikiwamo tano za kirafiki ambapo imeshinda tisa na kutoka sare moja, ikifunga mabao 21 na kuruhusu mawili pekee tena mechi za kirafiki.