Na Mwandishi Wetu,
Mageuzi ya mfumo mkuu wa kibenki wa Benki ya CRDB yameonekana kuwa na faida kubwa kwa sekta ya fedha, ikiwa ni pamoja na kuimarisha usalama wa miamala, kuongeza ubora wa huduma na kuwezesha upanuzi wa kimataifa wa huduma za kifedha.
Hatua hiyo imeongeza uwezo wa benki kuhudumia wateja wake katika matawi ya ndani na nchi jirani kama Burundi na DRC, huku ikiwa imejipanga kupenya kwenye masoko ya kimataifa, yakiwemo ya Mashariki ya Kati na Ulaya.
Kwa kutumia teknolojia mpya, CRDB imeweza pia kuongeza kasi ya utoaji huduma, kupunguza changamoto za kiufundi, na kuwezesha huduma bunifu kama vile matumizi ya akili mnemba (AI) katika kuhudumia wateja wa sekta zote.
Ubunifu huo umefungua milango ya ushirikiano wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na makubaliano na Huawei kwenye mabadiliko ya kidijitali, na Crop Trust kwa usalama wa chakula kupitia kilimo stahimilivu. Hii ni fursa ya kiuchumi kwa taifa na sekta binafsi.
Kutokana na mafanikio hayo, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Emmanuel Tutuba, ametoa pongezi kwa Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela, akisema mageuzi hayo ni ya kimkakati na yanaakisi ukomavu wa sekta ya fedha nchini.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Makao Makuu ya Benki jijini Dar es Salaam, leo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Bi. Tully Esther Mwambapa, alisema pongezi hizo zinadhihirisha imani endelevu ya wadau wa sekta ya fedha kwa Benki ya CRDB.
“Hakuna
safari ya mageuzi ambayo imewahi kuwa rahisi na hivyo ndivyo ilivyokua kwa
upande wetu pia. Katika kipindi cha mabadiliko, baadhi ya wateja walipata
changamoto za muda mfupi, jambo ambalo ni la kawaida katika mageuzi makubwa ya
mifumo.
Timu yetu ya wataalamu imekuwa ikifanya kazi usiku na mchana
kuhakikisha changamoto hizo zinashughulikiwa kwa haraka. Leo hii nafurahi
kuwajulisha kuwa huduma zetu zimerejea katika hali ya kawaida na mabadiliko
haya yaliyofanyika yamejenga msingi imara wa kutoa huduma hapa Tanzania,
Burundi, DRC, Dubai ambapo tunapanua wigo wetu na masoko mengine mapya
tunayoyaendea,” alisema Tully.
Pongezi hizo zilitolewa katika kikao maalum kilichowakutanisha BOT na uongozi wa juu wa CRDB, zikijikita zaidi katika uthubutu wa benki hiyo kusimamia mabadiliko makubwa bila kuathiri huduma kwa wateja.
Viongozi wengine serikalini na katika sekta binafsi nao wameunga mkono mageuzi hayo, wakisema yameongeza imani ya wawekezaji, yameonesha uongozi wa kijasiri, na kuweka Tanzania kwenye ramani ya kidijitali barani Afrika.
PICHA ZOTE NA JAMES SALVATORY