MGOMBEA UDIWANI KATA YA MJINI SONGEA, MATHEW NGALIMANAYO AOMBA RIDHAA YA AWAMU YA PILI

Songea_Ruvuma.

Mgombea Udiwani wa Kata ya Mjini, Manispaa ya Songea kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mathew Casian Ngalimanayo, ameomba tena ridhaa ya wananchi ili aweze kuendelea kulitumikia eneo hilo kwa kipindi cha pili, akiahidi kuendeleza jitihada za maendeleo hususan kwenye sekta ya elimu, miundombinu na mazingira rafiki kwa wafanyabiashara.

Akizungumza Oktoba 1, 2025 katika uzinduzi wa kampeni uliofanyika eneo la Mahenge C, Ngalimanayo alipokea Ilani ya CCM ya mwaka 2025-2030 kutoka kwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Songea Mjini, Mwinyi Msolomi, na kusema kuwa amekuwa mstari wa mbele kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi wa Kata ya Mjini, hasa katika elimu.

“Tumeweza kufanya maboresho makubwa katika shule zetu. Shule ya Msingi Mfaranyaki tumekarabati madarasa matano yaliyoharibiwa na upepo mwaka 2021, tukajenga vyoo tisa na kuboresha madarasa mengine matatu. Katika sekondari, tumejenga madarasa ya kisasa, matundu ya vyoo na mabweni. Haya yote yamechochea ongezeko la ufaulu,” alisema Ngalimanayo.

Diwani huyo wa zamani aliongeza kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wa karibu kati yake na Mbunge wa Jimbo hilo, Dkt. Damas Ndumbaro, ambaye pia amepewa ridhaa ya CCM kuwania tena ubunge Oktoba mwaka huu. “Tumekuwa tukishirikiana bega kwa bega na kwa umoja wetu, tumeweza kutekeleza miradi mingi kwa ufanisi,” alieleza.

Katika hatua nyingine, Ngalimanayo alisema uongozi wake umekuwa rafiki kwa wafanyabiashara wa Kata hiyo, bila kuwabughudhi, akiwataka wananchi kuwachagua tena wagombea wote wa CCM kuanzia ngazi ya udiwani hadi urais ili kuendelea kusukuma maendeleo kwa kasi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Songea Mjini, Mwinyi Msolomi, alisema CCM ndicho chama pekee kilichosimamisha wagombea nchi nzima na kinachoongoza serikali, hivyo wananchi waendelee kuwaamini wagombea wake. “Tumezingatia vigezo na uwezo wa viongozi wetu kabla ya kuwateua, hatufanyi makosa,” alisema.

Katibu wa CCM Wilaya, James Mgego, alisema mapokezi ya wananchi wa Kata ya Mjini yamekuwa makubwa na ni dalili kuwa chama hicho kinaungwa mkono kwa nguvu. Alisema chama kitaendelea kufanya ziara za kampeni katika kata nyingine kuomba kura.

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Kata ya Mjini alisisitiza kuwa maendeleo ya miundombinu ya barabara ni matokeo ya kazi kubwa ya Mbunge Dkt. Ndumbaro na Ilani mpya itaweka mkazo katika kumalizia vipande vilivyosalia ili kuunganisha kata hiyo kwa njia ya lami.

Kwa niaba ya wazee wa Kata hiyo, Mzee Gayo alisema: “Wananchi wa Mjini wanapaswa kuendelea kuiamini CCM ambayo imewaonyesha heshima kwa kuteua viongozi wenye ushawishi na uwezo kama Dkt. Nchimbi kuwa mgombea mwenza wa urais, Katibu Mkuu Dkt. Asha-Rose Migiro na Dkt. Ndumbaro kuwa Waziri wa Katiba na Sheria.”

Ngalimanayo, ambaye alihudumu katika awamu ya kwanza 2020-2025, amesema anatambua bado kuna kazi kubwa ya kufanya na anahitaji ridhaa ya wananchi ili kuikamilisha. “Nawaomba mniamini tena. Yale tuliyoyaanzisha kwa pamoja, kwa kushirikiana na viongozi wenzangu, tutaendelea kuyakamilisha,” alihitimisha.