Miradi ya Sh4.15 trilioni inavyotimiza ndoto ya ‘kumtua ndoo kichwani’

Dar es Salaam. Ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan ya ‘kumtua mama ndoo kichwani’ imekuwa alama ya mwelekeo mpya wa sera ya maji nchini Tanzania. Ndoto hiyo sasa inatekelezwa kupitia zaidi ya miradi 100 ya maji nchini kote, ikiwemo miradi mikubwa 25 yenye thamani ya Sh4.15 trilioni.

Kuanzia Arusha hadi Mtwara, Tabora hadi Kigoma, Dodoma hadi Dar es Salaam, miradi hii ambayo kwa sasa iko hatua mbalimbali na mingine imekamilika, itapunguza mzigo wa kutafuta maji uliowakumba wanawake na watoto kwa vizazi.

Kwa mujibu wa takwimu mbalimbali za Wizara ya Maji, mradi wa maji Arusha wenye thamani ya Sh520 bilioni na wenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 200 kwa siku na kunufaisha wakazi 850,000 upo kwenye hatua za mwisho kwa sasa.

Kukamilika kwake kutaongeza upatikanaji wa maji mijini hadi asilimia 91.6 na vijijini hadi asilimia 83, huku lengo la taifa likiwa kufikia asilimia 95 mijini na 85 vijijini ifikapo 2030.


Kwa wakazi wa mikoa ya Kilimanjaro na Tanga, kwa sasa Serikali imekamilisha mradi wa maji Same–Mwanga–Korogwe wenye thamani ya Sh406 bilioni ambao, utahudumia wakazi 300,000 kwa kuzalisha lita milioni 51.65 kwa siku nao umekamilika na wananchi wameanza kusahau changamoto za uhaba wa maji.

Ujenzi wa bwawa la Kidunda mkoani Morogoro utaokaogharimu Sh335 bilioni huku uwezo wa kuhifadhi maji ukitarajiwa kufikia lita bilioni 190 na kuhudumia zaidi ya watu milioni 6.77.

Ujenzi wa mradi huo utakuwa chachu ya kudhibiti mtiririko wa maji kwenye Mto Ruvu ili kuimarisha upatikanaji wa maji kwa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Kwa mujibu wa taalamu, mradi huu ndio unatajwa kuwa mwarobaini wa kupunguza ama kumaliza kabisa kero ya uhaba wa maji kwa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.

Kwa sasa wakazi wa Dar es Salaam wamekuwa wakipata huduma ya majisafi na salama mara tatu hadi nne kwa wiki kulingana na muda wa kufunguliwa.

Mbali na mradi huo, mwingine ni mradi wa maji Tabora-Nzega-Igunga-Singida wenye thamani ya Sh602 bilioni ukiwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 54.1 kwa siku nao utakwenda kumaliza tatizo la uhaba wa maji kwa wakazi milioni 1.2.

Kwa upande wa mkoani Mara, Serikali ya Samia inatekelezaji mradi wa maji Mgango–Kiabakari–Butiama wenye thamani ya Sh70.9 bilioni ambao utahudumia vijiji 13 kwa kuzalisha lita milioni 2 kwa siku.

Miongoni mwa miradi mingine ni ule wa Same–Mwanga–Korogwe (Kilimanjaro na Tanga) uliogharimu Sh406 bilioni ambao unakwenda kuwahudumia wakazi zaidi ya 300,000 na utakuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 51.65 kwa siku.

Mradi wa Bwawa la Kidunda uliopo mkoani Morogoro wenye thamani ya Sh335 bilioni ambao utahudumia watu milioni 6.77. Pia una uwezo wa kuhifadhi lita bilioni 190 na kuimarisha mtiririko wa maji kwenda Mto Ruvu.

Mradi mwingine ambao umekuwa mkombozi kwa wananchi ni Tabora–Nzega–Igunga–Singida uliogharimu Sh602 bilioni ukiwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 54.1 kwa siku na kuhudumia zaidi ya wakazi milioni 1.2.

Mbali na mradi huo, mwingine ni ule unaotekelezwa wilayani Bunda, Mara wenye thamani ya Sh29.5 bilioni.

Mradi huu utakwenda kuwanufaisha wakazi zaidi ya 320,000 ukiwa na uwezo wa kuzalishaji lita milioni 15 kwa siku. Wananchi wa Singida hasa wale wa Manyoni, wameanza kunufaika na mradi wa maji wa Kintinku–Lusilile unaozalisha lita 6.5 milioni kwa siku ukiwa na uwezo wa kuhudumia wakazi 55,000 huku ukigharimu Sh13 bilioni.

Katika kuhakikisha rasilimali zinawanufaisha Watanzania wote, Serikali ya Rais Samia inatekeleza mradi wa maji kutoka Ziwa Viktoria hadi Singida kisha Dodoma kwa awamu ya kwanza. Mradi huu unagharimu Sh326 bilioni, wakazi milioni 1.5, lita milioni 200 kwa siku.

Mradi wa Chalinze Awamu ya Tatu (Sh bilioni 96, ufadhili kutoka India) umekamilika kwa asilimia 96, ukiongeza uzalishaji kutoka lita 500,000 hadi milioni 2 kwa siku, kwa zaidi ya wakazi 200,000 wa Chalinze, Handeni na Morogoro.


Kanda ya Kusini nayo inanufaika na miradi ya maji kama ilivyo kwa maeneo mengine, ambapo mkoani Mtwara kunatekelezwa mradi wenye thamani ya Sh87 bilioni utakaozalisha lita milioni 40 kwa siku na kuhudumia wakazi 600,000.

Mradi wa maji Ruangwa–Nachingwea mkoani Lindi unaogharimu Sh119 bilioni ukihudumia watu 200,000 kwa lita milioni 15 kwa siku, na hivyo kutatua changamoto ya chumvi kwenye maji.

Mahitaji ya mijini pia yanashughulikiwa kupitia miradi ya Kigamboni Awamu ya Pili wenye thamani ya Sh65 bilioni ambao utazalishaji lita milioni 20 kwa siku na kupunguza uhaba wa maji kwa wakazi 250,000.

Mradi huo unahusisha visima virefu saba, tanki la kuhifadhi lita milioni 15 na mtandao wa mabomba wa kilomita 20.

Mkoani Mwanza kuna mradi wa maji Butimba wenye thamani Sh71 bilioni ambao utazalisha lita milioni 48 kwa siku na kuhudumia wakazi 450,000 ifikapo 2025, kwa ufadhili wa AFD, EIB na EU-Africa Infrastructure Trust Fund.

Miradi mingine ya miji ni pamoja na Chamwino (Sh13.5 bilioni), Nanyumbu (Sh80 bilioni), Kigoma (Sh42 bilioni), Chato (Sh65 bilioni), Makambako (Sh42 bilioni) na Singida wenye thamani ya Sh45 bilioni ambao utazalisha kati ya lita milioni 3 hadi 15 kwa siku.

Mradi wa uhimilivu wa Simiyu wenye thamani ya Sh500 bilioni ambao utahudumia wakazi 495,000 na wategemezi wao milioni 2.5, kwa kuzalisha lita milioni 30 kwa siku.

Mradi huu utakuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi ambao, kwa sasa wamekuwa wakipata maji, lakini sio kwa kiwango ambacho Serikali ingetamani.

Kwa mujibu wa Wizara ya Maji, miradi mikubwa 25 itawanufaisha zaidi ya Watanzania milioni 20, kuboresha afya ya jamii na kupunguza kwa kiasi kikubwa muda wanaotumia wanawake kuchota maji.


“Kipaumbele cha serikali ni wingi na ubora, miradi hii ni endelevu, yenye ufanisi na inayoendana na changamoto za tabianchi,” imesema sehemu ya taarifa ya Wizara ya Maji na kuongeza: “Uwekezaji huu si tu kwamba unabadilisha maisha ya kila siku, bali pia unaweka msingi wa maendeleo ya taifa kupitia upatikanaji wa uhakika wa moja ya rasilimali muhimu zaidi ya maji.”