Kibaha. Wakazi wa Mtaa wa Kitende Kwa Mfipa, Kibaha mkoani Pwani, wamegubikwa na simanzi baada ya watoto watatu kufariki dunia kufuatia moto ulioteketeza nyumba ya ghorofa moja.
Tukio hilo lilitokea Jana Jumatano Oktoba Mosi, 2025 Saa 10:00 alasiri, katika nyumba inayomilikiwa na Marey Balele.
Imeelezwa kuwa moto huo ulizuka ghafla ghorofa ya juu na kuharibu sehemu kubwa ya jengo hilo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase aliyoitoa kwa vyombo vya habari leo Alhamisi Oktoba 2, 2025, kabla ya moto kushika kasi ilisikika mlipuko na baadaye sauti za watoto wakilia wakimwita bibi yao aliyekuwa akiishi nao.
“Ilisikika sauti za watoto wakipiga kelele ndani, lakini ghafla moshi mkubwa ulianza kutoka dirishani kabla haijafahamika kilichokuwa kimetokea,” imesema taarifa hiyo.
Watoto waliofariki katika tukio hilo ni Adriela Siprian (4), Gracious Kadinas (3) na Gabriela Kadinas (1).
Kamanda Morcase amesema uchunguzi wa chanzo cha moto huo bado unaendelea, huku akitoa salamu za rambirambi kwa familia na watu wote walioguswa na msiba huo.
“Hili ni tukio la kusikitisha sana. Tunaendelea kufuatilia kwa kina ili kubaini chanzo cha moto huu,” amesema kamanda huyo.
Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani, Tumbi kwa ajili ya taratibu za kisheria na mazishi.