PALE Simba hivi sasa kuna ushindani mkubwa wa nafasi ya mshambuliaji wa kati inayowahusisha wachezaji watatu, Steven Mukwala, Jonathan Sowah na Selemani Mwalimu.
Mukwala ni mwenyeji kwa vile alikuwamo katika kikosi cha Simba msimu uliopita ambacho alikifungia mabao 12 katika Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini wenzake wawili, Mwalimu na Sowah ndio wanaitumikia Simba kwa mara ya kwanza baada ya kusajiliwa wakitokea katika klabu tofauti.
Jonathan Sowah amejiunga na Simba akitokea Singida Black Stars ambapo msimu uliopita licha ya kujiunga na timu hiyo katika dirisha dogo la usajili, alimaliza akiwa katika nafasi ya pili kwa kufumania nyavu kwa kupachika mabao 13.

Mwalimu ametokea Wydad Casablanca ya Morocco ambayo ilimsajili Januari mwaka huu akiwa tayari alishaifungia Fountain Gate mabao sita katika Ligi Kuu na kwa kiasi kikubwa kuondoka kwake kuliacha pengo ambalo liliipa kazi ngumu timu hiyo kuliziba.
Hapa kijiweni tunaamini Simba itanufaika sana na uwepo wa nyota hao watatu katika kikosi chao msimu huu kwa vile watakuwa na ushindani wa kila mmoja kutaka kufanya vizuri ili aweze kujihakikishia nafasi.
Na mara kwa mara Simba imekuwa ikipendelea kutumia mfumo ambao unailazimisha kuwa na mshambuliaji mmoja tu wa kati uwanjani hivyo kuna uwezekano mkubwa ambaye atachelewa kujipata anaweza asiwe anapata nafasi ya kutosha ya kucheza.
Kati ya hao watatu, mchezaji ambaye kijiwe kinamshauri akaze buti zaidi ni Steven Mukwala kwa vile hadi sasa bado hajaziona nyavu katika mechi za mashindano ambazo Simba imeshacheza kulinganisha na wenzake.

Fikiria tayari Jonathan Sowah ameshafumania nyavu katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Fountain Gate wakati huo Selemani Mwalimu akifanya hivyo katika mchezo dhidi ya Namungo FC.
Hii inaongeza presha zaidi kwa Mukwala, kwani kama asipofunga au hata kutoa asisti, atazidi kupoteza hali ya kujiamini na hivyo kujikuta anasotea benchi huku wenzake wakipewa kipaumbele.