Morogoro. Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu ameahidi kupunguza kodi kwenye vifaa vya ujenzi endapo atachaguliwa kuwa rais katika uchaguzi ujao.
Amesema lengo ni kuwawezesha Watanzania kujenga nyumba za kisasa kwa gharama nafuu.
Akihutubia wakazi wa Kata ya Kimamba, wilayani Kilosa mkoani Morogoro leo Alhamisi, Oktoba 2, 2025 Mwalimu amesema Serikali yake haitavumilia kuona wananchi wanaishi katika makazi duni huku gharama za ujenzi zikiwa juu kutokana na mzigo wa kodi na tozo mbalimbali.
“Tutapunguza Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye vifaa vyote vya ujenzi kutoka asilimia 18 ya sasa hadi asilimia 9 ili kuchochea ukuaji wa sekta ya ujenzi na kupunguza gharama kwa wananchi,” amesema Mwalimu.
Katika maelezo yake, ameahidi kutoa motisha kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa vifaa vya ujenzi ili kuwekeza hadi maeneo ya vijijini, lengo likiwa ni kufanikisha upatikanaji wa vifaa hivyo kwa urahisi na gharama nafuu katika kila pembe ya nchi.
Katika hatua nyingine, mgombea huyo ameeleza kuwa serikali yake itaondoa tozo za maendeleo ya viwanda kwenye bidhaa za ujenzi kwa kipindi cha miaka 10, ili kuwezesha wananchi wengi zaidi kumudu ujenzi wa nyumba bora.
Kwa lengo la kuwawezesha wananchi wa kipato cha chini, Mwalimu amesema ataanzisha Benki au dirisha maalum la mikopo nafuu ya ujenzi kwa kila halmashauri nchini.
Mikopo hiyo itatolewa kwa dhamana ya nyumba inayojengwa, hivyo kuwawezesha wananchi wote kuwa na makazi bora bila masharti magumu.
Mbali na hayo, Mwalimu ameahidi kuweka mazingira rafiki kwa sekta binafsi kuwekeza katika ujenzi wa nyumba nafuu, wananchi watawezeshwa kulipia nyumba hizo kwa mfumo wa kidogo kidogo hadi kumaliza mkopo.
Akimulika hali ya sasa, Mwalimu amesema Serikali iliyopo madarakani imeshindwa kupunguza mzigo wa kodi, ushuru na tozo, hali inayowakwamisha wananchi, wafanyabiashara na wawekezaji.
Ameahidi kubadilisha hali hiyo kwa kuweka mfumo wa kodi rafiki na unaomjali mwananchi wa kawaida.
Mwalimu aliyetumia siku 32 kusaka kura za kuchaguliwa na wananchi kushika wadhifa huo, Oktoba 29 mwaka huu kabla ya kesho kuingia Dar es Salaam, amesema Watanzania wanakabiliwa na maisha magumu hivyo Serikali yake imejipanga kushughulikia changamoto za Watanzania.
Akiwa katika mkutano wa hadhara, Mwalimu ameeleza kuwa hofu na kukata tamaa kwa wananchi ndizo silaha zinazotumiwa na wale wanaojimilikisha ardhi na kuwanyima wananchi fursa ya kutumia rasilimali zao kujiletea maendeleo.
“Wanataka mkate tamaa ili waendelee kutawala kwa kujiamini. Wanachukua mashamba yenu bila huruma, wanawanyima haki zenu, lakini bado mnabaki kimya kwa hofu. Huu ni wakati wa kubadilika,” amesema.
Mgombea Ubunge wa Kilosa kupitia chama hicho, Devid Chiduo amezungumzia changamoto mbalimbali zinazowakabili wakazi wa Kilosa, akiahidi kuzisimamia na kuzitafutia suluhu endapo atachaguliwa kuwa mwakilishi wao bungeni.
Akitaja changamoto ya kwanza, Chiduo amesema wakulima katika maeneo ya jirani na Hifadhi ya Taifa ya Mikumi wanakabiliwa na uvamizi wa tembo wanaoharibu mashamba na kula mazao yao.
Hali hiyo imesababisha wananchi kufanya shughuli za kilimo kwa hofu, wakikosa amani ya kufanya kazi zao kwa uhuru.
“Shughuli yetu kubwa hapa Kilosa ni kilimo, lakini tukilima mazao yanatafunwa na tembo wanaotoka Hifadhi ya Mikumi, wanakula na kutuacha maskini,” amesema Chiduo.
Ametaja pia migogoro ya muda mrefu kati ya wakulima na wafugaji kama kikwazo kikubwa cha maendeleo katika jimbo hilo.
Ameahidi akipewa ridhaa atahakikisha migogoro hiyo inapatiwa ufumbuzi wa kudumu kwa kushirikiana na mamlaka husika.
“Tusikubali wanakilosa kutumika, tunazo shida nyingi zinazotuhitaji mtu anayezijua na kwenda kuzitatua. Tunahitaji mtu kama mimi, mwenye nia ya dhati ya kurudisha heshima ya Kilosa,” amesisitiza.