Nabi avunja ukimya, afafanua ishu ya kutua Simba

KUNA taarifa zimesambaa kwamba, Simba SC imemfuata Kocha Nasreddine Nabi kwa ajili ya kumrithi Fadlu Davids aliyetimkia Raja Casablanca ya Morocco huku uwepo wake jijini Dar es Salaam ukichochea taarifa hizo.

Nabi kwa sasa yupo Dar es Salaam baada ya kutokuwa na kikosi cha Kaizer Chief baada ya uongozi wa klabu hiyo kuwa kwenye mipango ya kuachana naye rasmi.

Kocha huyo raia wa Tunisia, amezungumzia ujio wake hapa nchini huku akiweka wazi suala la yeye kutakiwa na Simba.

Nabi amesema ujio wake hapa nchini ni safari binafsi wala haihusiani na masuala ya kazi yake ya ukocha.

Mtunisia huyo amesema hadi jana Oktoba Mosi, 2025 alikuwa hajapokea ofa yoyote kutoka Simba au Yanga na kusisitiza kuwa sio mara ya kwanza kwake kuja Tanzania kwa kuwa ni kama nyumbani.


Kocha huyo aliyewahi kuzifundisha Yanga na FAR Rabat ya Morocco, amesema tangu atue Tanzania hajaonana na kiongozi yeyote wa klabu hizo mbili kubwa nchini na anashangaa taarifa zilizoenea mtandaoni kuwa anajiandaa kutua katika timu za Kariakoo.

“Nimeona watu wanasema nimekuja hapa kwa ajili ya Simba, wengine wanasema Yanga, hapana! Nipo hapa kwa safari yangu binafsi, nadhani hii ni mara ya tatu nakuja hapa.

“Tanzania ni nyumbani ndio maana napenda sana kuja hapa, tangu nimefika sijakutana na kiongozi yeyote wa Simba wala Yanga, nikimaliza mambo yangu nitaondoka,” amesema Nabi.

Kocha huyo amesema amefurahishwa na namna mashabiki wanavyompenda akisema kila anapopita watu wote wanamkaribisha na kufurahi naye.

“Nawapenda Watanzania, unajua kila unapopita wanakwambia wewe ni kocha wetu, watu wa Yanga na hata Simba, hii ni nchi yenye watu waungwana sana,” amesema Nabi aliyeifikisha Yanga fainali za Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022-2023 na kupoteza mbele ya USM Alger ya Algeria.


Hata hivyo, wakati Nabi akifafanua hajapokea ofa yoyote kutoka Simba wala Yanga, taarifa kutoka kwa vyanzo vya ndani ya timu hizo zinafichua kuwa vigogo wa klabu hizo wameanza kumpigia hesabu kwa ajili ya kumpa majukumu ya kuongoza benchi la ufundi.

Yanga ambayo kocha wake Romain Folz amekuwa akikosolewa na mashabiki kwa staili yake ya timu inavyocheza na upangaji wa kikosi, inadaiwa imeanza maandalizi ya kuachana na Mfaransa huyo na inamtazama Nabi kama chaguo sahihi kwa vile anaifahamu vyema klabu hiyo na maisha ya Tanzania.

Kwa upande wa Simba, inaamini Nabi anaweza kuwa mrithi sahihi wa nafasi iliyoachwa na Fadlu ambaye hivi karibuni ametimkia Raja Casablanca.

“Nabi ni kocha mzoefu na anaijua vyema ligi yetu na ana rekodi nzuri katika mashindano ya kimataifa. Ni kocha mkubwa ambaye hata wachezaji wanaweza kumheshimu hivyo hata yeye inawezekana tukampa nafasi hiyo,” kimesema chanzo ndani ya Simba.


Mbali na Nabi, Simba imekuwa ikihusishwa pia na kocha Miguel Gamondi anayeinoa Singida Black Stars kwa sasa sambamba na aliyekuwa kocha wa Al Ahly, Jose Ribeiro, japo uongozi umekuwa ukisisitiza mchakato unafanyika na kila kitu kikikamilika itatolewa taarifa kwa umma.