Serikali yajibu mapigo ripoti ya HRW haki za binadamu

Moshi/Dar. Serikali ya Tanzania imeijibu ripoti ya Shirika la Kimataifa la Uangalizi wa Haki za Binadamu (HRW) juu ya ukiukwaji wa haki za kiraia kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025, ikisema ni ya upotoshaji na uongo.

Wakati Serikali ikijua juu ripoti hiyo, wanazuoni waliozungumza na Mwananchi wametofautiana kimtazamo, baadhi wakisema yaliyosemwa na HRW si mageni yamekuwepo nchini, huku wengine wakisema ripoti hiyo imeandikwa na wanaharakati wenye agenda zao.

Mchambuzi wa siasa kutoka Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (Suza), Profesa Mohammed Makame amesema ripoti hiyo inatofautiana na nyingine zinazoeleza kuwa Tanzania imepiga hatua katika masuala ya utawala bora na haki za binadamu.

Ripoti ya HRW imeibua madai kadhaa dhidi ya Serikali ya Tanzania, ikidai imezidisha ukandamizaji wa kisiasa na hivyo kuibua wasiwasi mkubwa kwamba Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 29, 2025 utakuwa huru na wa haki.

HRW imedai ina matukio 10 ya mamlaka za Tanzania kuwanyanyasa, kuwateka kuwashambulia au kuwatesa wanaharakati wa haki za binadamu, wanachama wa vyama vya upinzani, mawakili na viongozi wa kidini tangu katikati ya 2024.

Hata hivyo, Serikali imesisitiza dhamira yake thabiti ya kulinda na kuendeleza haki za binadamu nchini, kama inavyothibitishwa na Katiba ya Tanzania na mikataba ya kimataifa na kikanda ya haki za binadamu, ambayo Tanzania imeridhia.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema katika taarifa yake, kuwa madai ya wasiwasi wa kupungua kwa haki za kiraia na vikwazo kwa vyama vya siasa kujihusisha na mchakato wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu, hayana msingi na ni potofu.

“Matukio ya utekaji nyara nchini yanachukuliwa kwa uzito mkubwa. Ifahamike kuwa haki ya kuishi, uhuru na usalama imehakikishwa na Katiba ya nchi,”amesema Msigwa katika taarifa yake ya Septemba 29, 2025 akijibu ripoti ya HRW.

“Serikali imejitolea kudumisha haki za binadamu kabla ya uchaguzi mkuu na kuendelea kama inavyofanya siku zote. Serikali pia imedhamiria kusimamia misingi ya utawala bora na utawala wa sheria katika chaguzi zijazo kama utaratibu wake.

“Serikali ya Tanzania inapenda kusisitiza kuwa iko wazi na tayari wakati wote kushirikiana na taasisi zinazotafuta taarifa sahihi, kuhusu haki za binadamu na maendeleo hapa nchini,” imesisitiza taarifa hiyo ya Msigwa.

“Tunatoa wito kwa mashirika na wadau wote kuwasiliana na mamlaka husika kabla ya kutoa ripoti ili kuepusha taarifa potofu zinazoweza kuchafua sifa ya nchi kimataifa,” imesema na kusisitiza kuwa taarifa ya HWR ililenga kuchafua taswira nchi.

Msigwa ambaye pia ni Katibu mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, amesema madai kuwa mamlaka mbalimbali za Tanzania zilipewa fursa kujibu tuhuma hizo, hazina msingi kwa kuwa hakuna mawasiliano ya aina hiyo yaliyofanywa.

Katika ripoti hiyo ya Septemba 29, 2025 HRW inadai Serikali ya Tanzania imezidisha ukandamizaji wa kisiasa, na hivyo kuibua wasiwasi mkubwa kwamba uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 29, 2025, kama utakuwa huru na wa haki.

“Mamlaka imekandamiza upinzani wa kisiasa na wakosoaji wa chama tawala, kukandamiza vyombo vya habari, na kushindwa kuhakikisha uhuru wa Tume ya Uchaguzi,” imedai taarifa hiyo iliyowekwa katika tovuti ya HRW.

“Mamlaka za Tanzania zinapaswa kuchukua hatua za haraka kulinda uadilifu wa uchaguzi wa Oktoba, ambao kwa sasa uko katika hatari kubwa,” anadai Nomathamsanqa Masiko-Mpaka, mtafiti wa Afrika katika shirika hilo.

“Mamlaka zinapaswa kuacha kukandamiza wakosoaji (wa Serikali) na vyombo vya habari, na badala yake zishiriki katika mageuzi ya maana ili kuhakikisha uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika,” anasisitiza mtafiti huyo wa HRW akitolea mfano kukamatwa na kushtakiwa kwa Tundu Lissu na kuenguliwa kwa Luhaga Mpina kwenye mchakato wa uchaguzi.

Kuanzia Julai hadi Septemba 2025, Shirika hilo linadai liliwahoji kwa mbali au ana kwa ana wanaharakati 24 wa mashirika ya kiraia, wanasheria, viongozi wa kidini, wasomi, waandishi wa habari, na wanachama wa vyama vya upinzani.

Miongoni mwa waliohojiwa ni waathirika wanane wa dhuluma, kutoka Tanzania Bara na Zanzibar na kwamba Septemba 19 HRW liliandikia Jeshi la Polisi Tanzania, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano na Wizara ya Mambo ya Nje kuwasilisha utafiti huo na kuomba taarifa kuhusu tuhuma hizo, lakini haijapata majibu yoyote wakati wa kuichapishwa.

“Haki ya kuishi ya watu ambao wana maoni tofauti na Serikali iko hatarini,” alinukuliwa kiongozi wa kidini ambaye alishambuliwa kwa uharakati wake.

“Watu wanapaswa kuwa na uwezo wa kuikosoa Serikali. Haipaswi kuhatarisha maisha yao. Utekaji nyara, kupotea, na baadhi ya mauaji ambayo hayawezi kuelezeka na huwezi kupata maelezo kutoka kwa Serikali,” anaeleza mtafiti huyo.

HRW limeorodhesha matukio 10 linayodai mamlaka ziliwanyanyasa, kuwashambulia, kuwateka nyara au kuwatesa wanaharakati wa haki za binadamu, wanachama wa vyama vya upinzani, mawakili na viongozi wa kidini.

Baadhi ya matukio hayo ni pamoja na tukio la usiku wa kuamkia Mei 2, 2025 ambapo watu wasiojulikana walimpiga na kumteka nyara mwanaharakati maarufu wa chama cha upinzani, Mpaluka Nyagali, anayejulikana kwa jina la Mdude.

Watu hao walimchukua Mdude kutoka nyumbani kwake Mbeya na hadi sasa hajulikani aliko na Polisi walikana kuhusika katika utekaji nyara wake.

Wametolea mfano wa tukio la Juni 16, 2025 jijini Dar es Salaam, ambapo watu wasiojulikana walimpiga kwa chuma Japhet Matarra, mkosoaji wa mara kwa mara wa Serikali kwenye mtandao wa X (zamani kama Twitter), hadi akapoteza fahamu.

Chanzo cha kuaminika kinadaiwa kuieleza HRW kwamba alipokuwa akisubiri kufanyiwa upasuaji hospitalini, watu waliokuwa wamevalia kama madaktari waliingia chumbani mwake na kumshambulia kisha kutokomea kusikojulikana.

Linadai kuwa Juni 23, 2024, jijini Dar es Salaam, polisi walimkamata kiholela mwanaharakati Edgar Mwakabela, anayejulikana mtandaoni kwa jina la Sativa ambaye alikosoa juu ya kupungua kwa nafasi ya kiraia na kisiasa nchini. Polisi walikana kuhusika na tukio hilo.

Kufuatia ripoti hiyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie amesema kilichoandikwa na HRW si kigeni kwani waathirika wa matukio hayo walishalalamika na Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) kilitoa orodha ya waliopotea.

“Hiyo ripoti ya Human Rights Watch imekuja tu kurasimisha, kuifanya iwe rejea rasmi, lakini hayo malalamiko yamekuwepo kwa muda sasa toka awamu ya tano, hayo malalamiko ya utekaji, uminyaji wa demokrasia na mengine mengi, kwa hiyo si kitu kigeni,” amesema.

Kuhusu Serikali kulalamika kutoshirikishwa, Dk Loisulie amesema inawezekana wametafutwa hawajapatikana au ni kweli hawajashirikishwa.

Hata hivyo, amesema bado hawajachelewa, bado wana uwezo wa kutoa taarifa sahihi ili kuondoa upotoshaji wanaodai.

“Ni kweli kwa uchaguzi huu, mwenye macho anaona na anapima, uchaguzi wetu wa mwaka huu uko tofauti na nyingine zilizopita kwa sababu hakuna ushindani kwa sababu washindani wenye nguvu hawapo kwenye kinyang’anyiro,” amesema.

“Chadema pamoja na ACT Wazalendo kwa upande wa Bara hawapo. Hiyo ni moja wapo inayoonyesha kwamba bado kuna kitu hakiko sawa, hata kama tutaficha, lakini kuna kitu hakiko sawa,” amefafanua mwanazuoni huyo.

Akiwa na mtazamo tofauti, mchambuzi wa siasa kutoka Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (Suza), Profesa Mohammed Makame amesema ripoti ya HRW inatofautiana na ripoti nyingine za kimataifa ambazo zinaeleza Tanzania imepiga hatua katika masuala ya utawala bora na haki za binadamu.

“Moja ya maeneo ambayo yametajwa Tanzania kupiga hatua yako katika utawala, usimamizi na haki za binadamu. Pia, wanaangalia jinsi gani Serikali imeweka mipango mizuri katika kuhakikisha hali ya nchi na maendeleo yake yanafikiwa kwa kiasi kikubwa,” amesema.

Ameonya kwamba taarifa zinazoandikwa na vyombo kama HRW, zinaandikwa na wanaharakati ambao wanaangalia zaidi mambo wanayoyaona yanafaa kwa upande wao na mara zote huwa ni ukosoaji.

“Kwa mwanaharakati, issue (suala) moja kwenye 100, yeye ndiyo inakuwa ya kuangalia, yaani ukitokea ufanisi wa asilimia 99, halafu asilimia moja tu ikawa ndiyo haijatimia, basi mwanaharakati ataangalia hiyo asilimia moja na kusema kuna kiwango hiki hakijakaa sawa,” amesema.