Tanzania yaanza afya kidijitali kuharakisha afya kwa wote

Dar es Salaam. Tanzania imeanza kuongeza uwekezaji katika afya ya kidijitali na teknolojia zinazotumia takwimu ili kuharakisha safari ya kufikia Huduma ya Afya kwa Wote (UHC).

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Seif Shekalaghe  amesema Serikali ipo mbioni kukamilisha Mkakati wa Afya Kidijitali 2025–2030 utakaolenga kuunganisha intelijensia ya Akili Unde (AI), kuimarisha usalama wa taarifa na kupanua mafunzo ya uelewa wa kidijitali kwa watumishi wa afya.

Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa Mkutano wa 12 wa Afya Tanzania (THS) ulioanza Oktoba mosi, 2025, Shekalaghe amesema ubunifu wa kidijitali utaibadili sekta ya afya nchini na kusaidia kuokoa maisha.

“Kaulimbiu ya mwaka huu, Kuzitumia Takwimu na Teknolojia kuharakisha Huduma ya Afya kwa Wote, ni ya wakati muafaka na inalingana na dira yetu ya Taifa. Takwimu na teknolojia si tena anasa bali ni nyenzo muhimu katika huduma za afya za kisasa,” amesema.

Aidha, ametaja majaribio yanayoendelea ya ‘telemedicine’ yanayounganisha vituo vya vijijini na madaktari bingwa wa mijini kwa njia ya mawasiliano ya video, akisema yatasaidia kuziba pengo la upatikanaji wa huduma za kibingwa.

“Tunataka kuhakikisha kila mtu, kila mahali, anapata huduma za afya bora bila kuingia kwenye umasikini kwa sababu ya gharama za matibabu,” amesema.

NHIF na mageuzi ya kidijitali

Kwa mujibu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), uko tayari kushiriki katika usajili wa afya kwa wote baada ya kuanzisha majukwaa ya kidijitali yanayowawezesha watu binafsi na mashirika kujisajili na kusimamia bima zao mtandaoni.


“Hadi sasa, ni asilimia 15 pekee ya Watanzania wamenufaika na bima, huku asilimia 85 bado hawajafikiwa. Hili ni pengo kubwa linalohitaji kushughulikiwa kwa haraka, ubunifu wa kidijitali ndio suluhisho,” amesema Meneja wa NHIF Mkoa wa Arusha, Hipoliti Lello.

Amesema awali waombaji walihitajika kuwasilisha nakala halisi za nyaraka kama vyeti vya Kitambulisho cha Taifa(Nida) na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), ili kujisajili.

Sasa, kwa kupitia mfumo wa kidijitali, wateja hawatalazimika tena kutembelea ofisi za NHIF bali watajisajili mtandaoni, kuchagua vifurushi na kulipia michango yao moja kwa moja.

Aidha, amesema madaktari watalazimika kuhakikisha sifa zao kitaaluma kidijitali kabla ya kuwatibu wanachama wa NHIF, na malipo yatashughulikiwa kwa wale tu wenye leseni halali na zilizohuishwa.

NHIF pia ilibainisha kuwa, gharama ya kutengeneza kadi za bima imepungua kutoka takribani Dola 5 kwa kila kadi hadi sifuri, kwa kutumia e-cards, namba za Nida, namba za simu, alama za vidole na hata utambuzi wa sura kwa ajili ya utambulisho wa wagonjwa katika vituo vya afya.

“Hii itapunguza gharama, ucheleweshaji na kero kwa wanachama waliokuwa wakilalamikia ucheleweshaji wa kadi za uanachama,” amesema Hipoliti.

Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kutoka Ofisi wa Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Eric Kitali amesema teknolojia haiwezi kuepukika iwapo nchi inalenga kufanikisha afya kwa wote.

“AI haitachukua nafasi ya binadamu, bali binadamu akiwa na AI ni muhimu sana kuzikubali na kuziendea teknolojia mpya ili tuendelee mbele,” amesema.

Mchumi wa afya mwandamizi kutoka Benki ya Dunia, Dk Moustafa Abdalah amesema teknolojia na takwimu za afya ni muhimu katika nchi ili kuweza kufanya uamuzi wa uwekezaji wa fedha.

“Lazima tuhakikishe tupo vizuri katika uwekezaji fedha katika sekta ili kuweza kufikia lengo. Tunaona katika nchi zingine fedha lazima ziwekezwe kutokana na takwimu zilizopo,” amesema.

Hata hivyo, baadhi ya wadau wameshauri kuwa ili kufikia afya kwa wote ufadhili wa ndani unahitajika.

Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), Mark Schreiner, amehimiza Serikali kuongeza uwekezaji katika afya ya kidijitali hasa wakati huu ambao ufadhili unapungua.


“Serikali lazima ichukue hatua thabiti kuimarisha ufadhili wa afya wa ndani, ikiwa ni pamoja na mifumo bunifu kama bima ya afya na kodi za afya,” amesema huku akitoa mfano wa kodi ya Ukimwi na mgao wake katika Mfuko wa Ukimwi kuwa ni ishara ya kujitolea kwa Taifa.

Pia, amesisitiza umuhimu wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi ili kuongeza uwekezaji na ufanisi katika sekta ya afya.

Aidha, amehimiza matumizi ya takwimu zilizogawanyika kwa ajili ya kushughulikia usawa na kuongeza uwajibikaji.

“Mkutano huu uwe chachu ya hatua thabiti. Kwa uongozi wa Serikali, ubunifu wa sekta binafsi na mshikamano wa washirika wa maendeleo. Tanzania inaweza kujenga mfumo wa afya imara, unaoongozwa na takwimu na unaotoa huduma bora kwa jamii zote,” amesema.

Ubunifu wa kidijitali wa mfano

Miongoni mwa ubunifu uliotajwa ni mfumo wa m-mama wa usafiri wa dharura unaotumia namba ya simu isiyolipiwa na programu ya simu kuratibu usafiri kwa ajili ya wajawazito na watoto wachanga walioko kwenye hatari.

Mradi huo uliotekelezwa nchi nzima mwaka jana, unatarajiwa kuwafikia zaidi ya wanawake na watoto 50,000 kila mwaka. Katika mikoa iliyojaribiwa, ulipunguza vifo vya wajawazito kwa hadi asilimia 27.

Mafanikio mengine ni mpango wa afya ya jamii wa Zanzibar wa kidijitali wa kwanza duniani kuongozwa na Serikali kwa ngazi ya kitaifa.

Mpango huu unaunganisha kaya na wahudumu wa afya ya jamii waliowezeshwa kidijitali, hivyo kuhakikisha karibu wakazi wote milioni 1.9 wa Zanzibar wanapata huduma za afya moja kwa moja majumbani mwao.