TFF yabanwa kesi ya kumfungia maisha kocha Katabazi

MAHAKAMA Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, imetengua hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu iliyoifuta kesi ya Kocha Listoni Katabazi dhidi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kupitia Bodi yake ya Wadhamini.

Badala yake, mahakama hiyo imeirejesha kesi hiyo katika Mahakama ya Kisutu huku ikiiamuru mahakama hiyo ya chini iendelee kuisikiliza kesi hiyo katika ustahilifu wake, yaani kusikiliza hoja zake za msingi za kuishtaki TFF.

Uamuzi huo umetolewa na Jaji Butamo Phillip kufuatia rufaa aliyoikata Katabazi akipinga uamuzi huo wa Mahakama ya Kisutu kuifuta kesi yake; baada ya kukubaliana na hoja za Kocha Katabazi za rufaa hiyo.

“Hatimaye, rufaa hii imekubaliwa. Uamuzi uliokatiwa rufaa unaondolewa. Jalada la kesi litarejeshwa mara moja Mahakama ya Awali (Kisutu) ili iendelee kusikiliza shauri,” amesema Jaji Phillip.

Katabazi ambaye anajitambulisha kuwa ni mdau wa mchezo wa mpira wa miguu na kocha wa mchezo huo mwenye leseni ya daraja C, iliyotolewa na TFF, mwaka 2021, alifungiwa na TFF kujishughulisha na masuala ya mchezo huo ndani na nje ya nchi maisha yake yote.

Adhabu ya kufungiwa ilikuja baada ya kuliandikia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) barua Juni 15, 2021 akilishtaki TFF kuwa limeshindwa kusimamia mchezo huo kulingana na Sheria, Kanuni na miongozo yake.

Kufuatia barua hiyo, aliitwa katika Kamati ya Maadili, lakini hakuhudhuria badala yake alijibu kuwa yeye si mwanachama wa Chama cha Makocha Tanzania (Tafca) ambacho kiko chini ya usimamizi wa TFF, hivyo yeye si mwanachama wa TFF.

Juni 24, 2021 TFF lilichapisha katika tovuti yake uamuzi wa kumfungia Katabazi maisha kujishughulisha na masuala ya mpira wa miguu ndani na nje ya nchi.

Hivyo mwaka 2024 alifungua kesi Mahakama ya Kisutu dhidi ya TFF na wadhamini wake akipinga uamuzi huo wa kufungiwa.

Katika kesi hiyo ya madai namba 14708/2024, pamoja na mambo mengine alidai kuwa Kamati ya Maadili ya TFF haikuwa na mamlaka ya kutoa uamuzi huo dhidi yake kwa kuwa Kanuni za Maadili za TFF, Toleo la Mwaka 2021, zilizotumika kumfungia si halali.

Alidai kuwa kanuni hizo hazijasajiliwa na BMT kwa mujibu wa matakwa ya Sheria namba 12 ya mwaka 1967 na marekebisho yake, na hivyo kuzifanya kuwa batili kutumika dhidi ya wanachama wake na mtu mwingine yeyote.

Katabazi alidai kuwa amri hiyo iliingilia haki yake ya kufanya kazi katika nyanja ya soka na hivyo kumkosesha fursa ya kupata mshahara na kipato kwa ajili ya kuendeleza maisha yake ya kila siku na familia yake, na kumsababishia maumivu ya kisaikolojia.

Hivyo aliiomba mahakama iiamuru TFF imlipe Sh600 milioni kama fidia ya madhara ya jumla aliyoyapata kutokana na uamuzi huo wa kumfungia maisha uliotolewa kwa maksudi, kimakosa na kwa nia ovu.

Pia aliomba alipwe Sh100 milioni kama fidia ya adhabu kwa kitendo cha wadaiwa kutoa uamuzi huo wakijua kuwa hawana mamlaka ya kisheria kuchukua hatua hiyo dhidi yake, riba ya kiwango cha Mahakama kwa cha tuzo (fedha ambazo ingeamuriwa alipwe) na gharama za kesi.

Vilevile aliiomba mahakama itoe zuio la matumizi ya Sheria (Katiba) na Kanuni za Maadili za TFF, kwa madai kuwa si vyombo halali kwa kutokusajiliwa kwa utaratibu na unaofaa.

Miongoni mwa vielelezo alivyoviwasilisha mahakamani ni barua ya BMT ya Juni 13, 2022 iliyothibitisha kuwa yeye si mwanachama wa TFF.

Mahakama ya Kisutu iliifuta kesi hiyo, kufuatia pingamizi la awali lililoibuliwa na TFF.

Katika uamuzi wake uliotolewa na Hakimu Mfawidhi, Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswaga alisema kuwa hakuna ubishi kuwa Katabazi ni mwanachama wa TFF.

Alikubaliana na hoja za wakili wa TFF kuwa kwa mujibu wa Katiba ya TFF, mwanachama asiyeridhika na uamuzi wa Kamati ya Maadili anapaswa kukata rufaa katika Kamati ya Rufaa ya Maadili na asiporidhika anakata rufaa Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS).

Hivyo alisema kuwa mahakama hiyo haikuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo kwani mlalamikaji, Katabazi alipaswa kukata rufaa Kamati ya Rufaa ya Maadili na kama asingeridhika angekata rufaa CAS kama Katiba ya TFF inavyoelekeza.

Katabazi hakuridhika na uamuzi huo, hivyo alikata rufaa Mahakama Kuu pamoja na sababu nyingine, akidai kuwa Mahakama ya Kisutu ilikosea kisheria kushughulikia pingamizi la wajibu rufani ambalo halikuwa na msingi wa kisheria na kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa wakati wa usikilizwaji wa pingamizi.

Pia alidai kuwa Hakimu alikosea kisheria na kiukweli kwa kutegemea ushahidi wakati wa kusikiliza pingamizi la awali na pia kwa kufuta kesi baada ya kubaini kwamba hakuwa na mamlaka ya kuisikiliza, badala ya kuifuta bila kuathiri haki ya kufunguliwa upya (striking out).

Rufaa hiyo ilisikilizwa kwa njia ya maandishi, ambapo mrufani, Kocha Katabazi aliwakilishwa na wakili Peter Majanjara, huku warufaniwa (TFF na Bodi yake) wakiwakilishwa na wakili Rahim Shaban.

Jaji Phillip katika uamuzi huo alioutoa Septemba 26, 2025, amesema kuwa baada ya kupitia uamuzi uliokatiwa rufaa, alibaini kwamba uamuzi huo ulitegemea mambo mawili; Mosi, kama mrufani (Kocha Katabazi) ni mwanachama wa TFF, hivyo amefungwa na Katiba na Kanuni za TFF.

Jambo la pili amesema ni kama Mahakama ya Awali (Kisutu) haina mamlaka ya kusikiliza shauri kesi hiyo kwani Katiba ya TFF inatoa utaratibu wa kukata rufaa dhidi ya uamuzi ya Kamati ya Maadili, ambao Mrufani, Kocha Katabazi alipaswa kuufuata, badala ya kufungua kesi mahakamani.

Hata hivyo amesema kuwa amebaini kuwa Mahakama ya Awali ilijihusisha na kutafsiri masharti ya Katiba ya TFF na matumizi yake, ikaamua kwamba mrufani ni mwanachama wa TFF, ilhali yeye alikana kuwa si mwanachama wa TFF, hivyo hakufungwa na Kanuni zake.

Jaji Phillip amesema kuwa kwa kuangalia hati ya madai, haikuwa sahihi Mahakama hiyo kukubali pingamizi la awali la mamlaka ya mahakama lililowekwa na wajibu rufani, kwani baadhi ya hoja zilihitaji kuthibitishwa kwa ushahidi.

Amefafanua kuwa ilipaswa kuchambua nyaraka zilizoambatanishwa kwenye hati ya madai baada ya kupokelewa kama vielelezo, ili kubaini baadhi ya mambo muhimu kuhusiana na madai ya mrufani, kama vile uanachama wake katika TFF, ili kufanya uamuzi sahihi.