Vijana wapatiwa mafunzo ya kilimo biashara kujikwamua kiuchumi

Dodoma. Vijana takribani 83,000 kutoka mikoa saba nchini wamepewa mafunzo ya kuendesha kilimo biashara ili kujikwamua kiuchumi, kujiajiri na kuajiri wengine kupitia mnyororo wa thamani wa sekta ya kilimo.

Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 asilimia 75 ya idadi ya watu nchini ni vijana wenye umri wa kuanzia mwaka 0 hadi 35 huku kati yao asilimia 44 wenye umri kuanzia miaka 0 hadi 15 ni tegemezi na asilimia 31 tu ndiyo wenye uwezo wa kuzalisha.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula Duniani (WFP) kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la Rikolto limetoa mafunzo kwa vijana 40,000 wanaoishi kwenye mikoa ya Dodoma na Singida ili kuwajengea uwezo kwenye mnyororo wa thamani kwenye kilimo cha mtama, alizeti, matunda na mbogamboga.

Ili kuwapata vijana hao Shirika la Rikolto liliendesha shindano la kupata mawazo bora ya kilimo biashara ambapo jumla ya vijana 100 wenye umri kati ya miaka 18 hadi 35 walijitokeza na mawazo ya biashara, yaliyochujwa hadi kupatikana biashara bora 27.

Akizungumza leo Alhamisi Oktoba 2, 2025 jijini Dodoma, kwenye kilele cha shindano hilo meneja miradi kutoka Shirika lisilo la kiserikali la Rokolto, Willifaston Ntoroma amesema lengo la kuanzisha shindano hilo ni kuwajengea uwezo vijana wanaotaka kujiajiri kupitia sekta ya kilimo.

Amesema vijana wengi walijitokeza kushiriki shindano hilo wenye mawazo mazuri ya kuendesha kilimo biashara hali iliyoonyesha kuwa wapo tayari kujiajiri kupitia sekta ya kilimo, isipokuwa hawana mitaji ya kuendeleza biashara hizo.

Meneja huyo amesema wengi wa vijana waliojitokeza ni wasomi wa vyuo vikuu ambao wametumia elimu waliyonayo kujiajiri kwenye sekta ya kilimo kuanzia kwenye uzalishaji, uchakataji na uuzwaji na uzalishaji wa pembejeo za kilimo.

“Lengo la mradi huu ni kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na usalama wa chakula kwa sababu tuna amani kwa sababu tuna uhakika wa chakula, hivyo ni lazima tuongeze kiwango za uzalishaji kupitia kundi la vijana ili waweze kujiajiri na kutoa ajira kwa wengine,” amesema Ntoroma.

Amesema pia vijana hao wamepewa elimu ya usalama wa chakula kutoka uzalishaji shambani hadi kinapomfikia mlaji, utunzaji wa mazingira, elimu ya fedha na jinsi ya kufanya biashara zao ziwe endelevu hata ufadhili utakapokwisha.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Mkurugenzi wa WFP nchini, Abiudi Gamba amesema mradi wa kilimo biashara umewafikia vijana 83,000 kutoka mikoa ya Shinyanga, Tabora, Simiyu, Singida, Dodoma, Arusha na Manyara ambapo wamepewa mafunzo kwa awamu tatu tofauti.

Amesema kwa mikoa ya Singida na Dodoma, takribani vijana 40,000 wamepewa mafunzo lakini walioingia kwenye shindano la kupata wazo bora la kilimo biashara watapewa zawadi ya fedha jumla ya Dola za Marekani 24,000 (sawa na Sh60 milioni), ambazo watagawana kwa watu 10 ambao mawazo yao yameshinda.

Naibu Katibu Mkuu wizara ya Kilimo, Dk Stephen Nindi



Amesema pamoja na kuendesha mradi wa kilimo biashara lakini kilimo nchini kimekuwa kikikabiliwa na changamoto kadhaa ambazo zinakatisha jitihada za vijana kujikwamua, ikiwemo mabadiliko ya tabianchi ambayo yamesababisha ukame na mavuno kidogo.

 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Dk Stephen Nindi amesema Serikali imetoa fursa nyingi za ajira kwa vijana kupitia sekta ya kilimo na ndiyo maana kuna programu nyingi zinatekelezwa ikiwemo ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT), ambapo kuna BBT kilimo, BBT uvuvi na BBT mifugo ambayo yote kwa pamoja inatekelezwa kwa asilimia 100 na vijana wa Kitanzania.

Amesema pia Serikali imeongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo kutoka Sh294 bilioni kwa mwaka wa fedha 2021/2022 hadi kufikia Sh1.243 trilioni kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

 Amesema ongezeko hilo linadhihirisha kuwa Serikali imeamua kuwekeza kwenye sekta ya kilimo ili kuinua kipato cha wakulima.

Dk Nindi amesema kwa kupitia sekta ya kilimo hivi sasa Tanzania ina usalama wa chakula kwa asilimia 100, na ziada ya chakula asilimia 28 ambayo inaweza kulisha Bara la Afrika kibiashara.

“Na ili kuwafikia wakulima wote nchini Serikali ina mpango wa kuanzisha wakala wa huduma za ugani ambayo itakuwa inajitegemea ili kuwahudumia wananchi popote walipo, kuanzia ngazi ya chini kabisa kwa sababu kuna maeneo ambayo maofisa ugani hawafiki kutokana na uchahe wao,” amesema Dk Nindi.