Vyuo vikuu vitano vyaungana kukabiliana na mabadiliko tabianchi

Morogoro. Watafiti na wahadhiri kutoka vyuo vikuu vitano wamekutana mjini Morogoro kwa ajili ya kutafuta suluhisho kwa changamoto zinazochochewa na mabadiliko ya tabianchi hususani katika sekta za kilimo, afya na upatikanaji wa maji.

Katika mkutano huo unaohusisha vyuo vikuu vinne vya Tanzania na kimoja cha Canada, wanasayansi wamepanga kuja na majawabu jumuishi yatakayogusa maisha ya wananchi wa vijijini na mijini moja kwa moja yanayohusu sekta hizo muhimu.

Ushirikiano huo unajumuisha  Chuo Kikuu cha Aga Khan, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Chuo Kikuu cha Nelson Mandela cha Sayansi na Teknolojia (Arusha), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), na Chuo Kikuu cha Simon Fraser cha Canada.

Akizungumza katika mkutano huo wa pili wa kisayansi wa ushirikiano kati ya vyuo hivyo, leo Oktoba 2, 2025, Makamu Mkuu wa SUA, Profesa Raphael Chibunda amesema lengo si kufanya tafiti zinazobaki kwenye makabrasha, bali kutafuta suluhu za changamoto zinazogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.

“Kaulimbiu yetu mwaka huu ni ‘Zaidi ya kuishi: Kujenga jamii jumuishi na imara dhidi ya mabadiliko ya tabianchi”.

“Tunataka jamii zetu ziwe tayari kukabiliana na changamoto za kidunia zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi,” amesema Profesa Chibunda.

Ameeleza kuwa SUA imeendelea kuongoza katika tafiti za uhifadhi wa misitu, mazingira na wanyamapori ikiwemo utafiti wa nishati mbadala ili kupunguza matumizi ya mkaa na kuni, pamoja na mbinu za kilimo endelevu zisizo na madhara kwa ardhi na misitu.

Ameongeza kuwa chuo hicho kinashirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (Tafori) kutafuta miti inayokua haraka kwa ajili ya matumizi ya nishati bila kuharibu mazingira.

Akifungua mkutano huo wa pili, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa vyuo vikuu katika kutafuta majibu ya changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

“Tumeshaona matokeo ya moja kwa moja ya tafiti, mfano hapa Morogoro ambapo wakulima wameanza kubadilisha mbinu za kilimo kutokana na elimu na utafiti wa Sua, huu ni uthibitisho kuwa tafiti za vyuo vikuu zinaweza kuokoa maisha na kubadilisha jamii,” amesema Profesa Nombo.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Nelson Mandela, Profesa Maulilo Kipangula amesema ushirikiano huo utazaa ubunifu mpya wa kiteknolojia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Tayari tumepata nafasi ya kutuma wanafunzi wawili kwa ufadhili katika Chuo Kikuu cha Simon Fraser nchini Canada na tunatarajia kuanzisha maabara maalumu za utafiti wa mabadiliko ya tabianchi hapa nchini,” amesema Profesa Kipangula.