WAKATI Tanzania ikibaki na wawakilishi watano katika michuano ya kimataifa ngazi ya klabu msimu huu 2025-2026, wadau mbalimbali wa soka hapa nchini, wamezipa nafasi kubwa timu nne za Tanzania Bara kucheza hatua ya makundi.
Katika timu zilizobaki, kuna KMKM ya Zanzibar inayoshiriki Kombe la Shirikisho baada ya Mlandege kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa. Kwa upande wa Tanzania Bara, Yanga na Simba zinashiriki Ligi ya Mabingwa, wakati Singida Black Stars na Azam zipo Kombe la Shirikisho.
Wadau hao walitoa maoni yao kupitia mjadala wa Mwanaspoti Space ulioandaliwa na Mwananchi Communications Limited (MCL) uliofanyika leo Alhamisi, Oktoba 2, 2025, katika mada isemayo ‘Umeonaje viwango vya timu za Tanzania katika mashindano ya CAF na zifanye nini zitoboe makundi?’
Sio wote waliozipa nafasi timu hizo kufuzu makundi, wapo ambao wamekuwa na wasiwasi juu ya viwango walivyoonesha kwa baadhi ya timu, lakini pia kuna ushauri wameutoa.
KINACHOZIBEBA SIMBA, YANGA
Kocha wa zamani wa timu ya vijana ya Azam FC, Mohamed Badru, amesema Yanga na Simba zinaweza kufika mbali, kutokana na kubebwa zaidi na ubora wa wachezaji hususani wa kigeni.

“Hatuko vibaya kwa sababu ukiangalia timu zote zina wachezaji wanaoweza kutufikisha mbali zaidi, ukiangalia tulipotoka na sasa kuna mabadiliko makubwa na hii inatokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika ambao tunaona faida zake,” amesema.
“Sina mashaka na hizo timu kutokana na mabenchi bora ya ufundi waliyonayo kwa sababu wameshakutana na changamoto kubwa katika michuano hiyo, kwa KMKM inastahili hapa ilipofika ingawa huwezi kulinganisha na klabu za Bara kwa uwekezaji.”
Badru aliyewahi kuzifundisha pia timu za Mtibwa Sugar na Gwambina, amesema kukutana kwa KMKM na Azam anaamini itakuwa ni mechi ngumu, kutokana na rekodi na historia ya miaka ya hivi karibuni wakati zinapokutana katika michuano mbalimbali.
Aidha Badru, amesema kwa upande wa KMKM kutoka Zanzibar, imeonyesha matumaini makubwa kutokana na kiwango ilichokionyesha hadi sasa, ingawa jitihada kubwa zinahitajika kwa sababu timu nyingi za visiwani humo hazina udhamini wa kutosha.
“Changamoto kwa timu za Zanzibar ni suala zima la uwekezaji kwa maana ya wadhamini wengi na maandalizi ya kutosha, japo kwa hapo tulipofikia tunaona kabisa kuna mwanga unaonekana na kwa miaka ijayo zitaleta ushindani zaidi,” amesema Badru.
Kocha wa zamani wa maafande wa Tanzania Prisons, Amani Josiah amesema hadi sasa timu za Tanzania zilipiga hesabu nzuri katika hatua ya awali ya mchujo ya kufuzu michuano ya CAF, hususani baada ya kuanza kucheza mechi za ugenini na kila mmoja kufanya vizuri.
“Hesabu za timu za Tanzania zilienda vizuri kwa raundi iliyopita kwa sababu ya kushinda ugenini, jambo ambalo kwa mitazamo ya mwanzo ilikuwa ni tofauti hasa kwa mechi za CAF.
“Kwa hatua ijayo ambapo timu tatu zitaanzia ugenini, lengo la kwanza ni kupata sare, naziona zote zikienda hatua ya makundi,” amesema.
Katika hatua nyingine, Josiah aliyewahi kuifundisha Geita Gold, amesema huu ni muda kwa timu shiriki kuboresha viwango vyao, ingawa kadri michuano inavyozidi kusonga mbele ndivyo wachezaji wanavyozidi kuelewana na kutengeneza balansi ya kiuchezaji.
“Sina shaka na timu za Tanzania kufuzu hatua ya makundi, japo kwa Simba kama inahitaji benchi jipya la ufundi inaweza kutumia kipindi hiki cha mapumziko kufanya hivyo, kwa lengo la kocha mpya kupata muda na wachezaji,” amesema Josiah.
Aidha, Josiah amesema licha ya Simba kuwa katika mchakato wa kutafuta kocha mpya, kuna uwezekano usiathiri moja kwa moja viwango vya wachezaji, tofauti na benchi jipya la ufundi linapokuta nyota wapya zaidi ya 10, walioingia kikosini.

EYMAEL ATEMBEA NA AZAM, SINGIDA BS
Kwa upande wa Kocha wa FC Lupopo ya DR Congo, Luc Eymael amesema ameridhishwa na kiwango kilichoonyeshwa na klabu za Singida Black Stars na Azam kwenye mechi za awali, huku akipata wasiwasi na Simba na Yanga.
Eymael ambaye ni kocha wa zamani wa Yanga, amesema Singida BS ambayo ina mchezaji wake wa zamani Horso Mwaku, pamoja na Azam zimenufaika na kuunda mabenchi imara ya ufundi.
Katika mechi za hatua ya awali, Yanga, Azam na Singida Black Stars zimeshinda ugenini na nyumbani bila ya kuruhusu bao, huku Simba ikishinda ugenini na kuambulia sare ya bao 1-1 nyumbani, lakini zote zimevuka.
“Nimefurahishwa na timu za Tanzania hususan Azam FC ambayo inafundishwa na kocha mzoefu Florent Ibenge wakati Singida ambayo ina mchezaji wangu wa zamani alikuwa mfungaji bora nayo imekuwa na mwanzo mzuri,” amesema Eymael.
“Ukiangalia hizi timu zimekuwa na makocha wenye uezofu, hili limewasaidia sana, Singida ina kocha Gamondi, ninamjua ni kocha mzuri, amefanikiwa kuibadilisha timu yake.”
Aidha Eymael raia wa Ubelgiji ameonyesha wasiwasi na klabu kongwe za Simba na Yanga akizitaka kuwa imara kwenye mabenchi yao ya ufundi huku akipongeza hatua ya kukua kwa soka la Tanzania.

“Kama sijakosea Simba hawana kocha na walikuwa wanasimamiwa na kocha waliyemuazima timu ya taifa lakini Yanga nako kunaonyesha benchi lao halijatulia nadhani wanatakiwa kujipanga.
“Naipongeza Tanzania naona kuna hatua kubwa zinaendelea kupigwa, ukiangalia tangu nimeondoka Tanzania kuna hatua kubwa zimepigwa, hili ni zuri kwa soka la hapo.”
Wasiwasi alionao Eymael juu ya kiwango cha Simba na Yanga ni sawa na Mwandishi wa Mwananchi, Devotha Kihwelo ambaye hata hivyo naye ameridhishwa na Azam.
Devota amesema anaridhishwa na kiwango cha klabu ya Azam kwani imeonyesha imejipanga kwenye mashindano ya Afrika huku akizitaka klabu kongwe za Simba na Yanga kujipanga.
Amesema Azam imeanza vizuri ikionyesha umakini kwenye mechi mbili za hatua ya awali ilizocheza ambapo anaamini ikiendelea hivyo itafikia malengo kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.
“Nimevutiwa na namna Azam ilivyocheza hizi mechi imeonyesha ina nguvu kubwa kwenye hizi mechi mbili ilizocheza,” amesema Devotha
Aidha, Devotha amezitaka Simba na Yanga kubadilika kwani hazikucheza vizuri kwenye mechi za kwanza huku mashabiki wake wakikosa kuridhishwa na viwango vya timu zao.
“Ukiangalia Simba haikucheza vizuri mashabiki wake wamekuwa wanalalamika, hivyo hivyo kwa Yanga, mashabiki wake nao wanalia, nadhani nini kifanyike zinatakiwa kuendelea kujipanga.”

Nyota wa zamani wa Simba na Taifa Stars ambaye sasa ni Kocha wa Soka la Ufukweni, Boniface Pawasa, amesema bado timu wawakilishi wa Tanzania kwenye mashindano ya Afrika hazijacheza vizuri, huku akibainisha kwamba ni mapema kuanza kuona ubora wa timu hizo kwa kuwa zimeingia mapema kwenye mashindano.
“Mimi ukiuliza naona hizi timu zimecheza kwa asilimia 50 tu, timu zote zinazotuwakilisha bado hazijaweza kucheza kwa ubora mkubwa kwa kuwa wachezaji wanapitia kipindi cha kujua falsafa za makocha wao,” amesema Pawasa.
“Timu zimetoka kwenye maandalizi ambayo unahitaji muda kabla ya kuanza kuona kile ambacho kinatarajiwa, tunaweza kuja kuona kitu kikubwa lakini tunatakiwa kusubiri.”
Aidha, Pawasa ameongeza amefurahishwa na namna wachezaji wazawa wanavyojituma na kuwapa changamoto wageni kwa kuanza kwenye timu zao huku wageni wakisubiri.
“Sijui niuitaje maana unakuta wachezaji wa kigeni wanapewa sifa kubwa sana kuliko ubora wao, kitu kilichonifurahisha ni wazawa kutokukubali unyonge wameshindana vizuri, ufike wakati tuthamini wachezaji wetu ili kuwapa nafasi makocha wa timu kupata wachezaji bora.”
Kocha wa zamani wa Azam FC, Idd Cheche amesema jambo la msingi timu zinazoshiriki michuano ya CAF zijitambue, ziweke malengo na kujituma kuhakikisha zinafika mbali.
“Mpira ni mchezo unaotengenezwa katika saikolojia, wachezaji wakijengwa naamini hata timu mbili zinaweza zikafika fainali za michuano hiyo.
“Kadri mechi zinavyochezwa ndivyo ugumu unaongezeka, kwa sasa mpira wa Afrika umeanza kufanana, hivyo timu ziangalie baadhi ya makosa yaliyofanywa katika mechi za mwanzo na ziboreshe.
“Timu ziwe tayari kukosolewa na kila mmoja asimame katika jukumu lake, mashabiki wawape nguvu wachezaji na wachezaji wapambane uwanjani na makocha mbinu zao ziwe imara.
“Mechi za nyumbani ziwe silaha yao kuhakikisha zinashinda ili za ugenini hata zikipata sare zinawaweka katika hali salama, kitu kingine cha msingi timu ziungane zinapochezwa nyumbani ziwe kitu kimoja na siyo kuunga mkono wageni,” amesema Cheche.
Ofisa Habari wa Azam FC, Thabit Zakaria amesema iko haja ya kama taifa kufanya jambo ili kuliinua soka la Zanzibar, ikiwamo kuwa na ligi moja.
Zaka amesema: “Kati ya Azam na KMKM kwa sababu ndio zitakutana katika hatua ya pili ya mchujo wa Kombe la Shirikisho Afrika, hii inamaanisha tayari tumejihakikishia timu moja katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho. Na timu zetu nyingine zikifuzu tukawa na timu nne, itatupa nafasi zaidi ya kufanya vizuri kuliko ikipita timu moja.
“Jambo zuri ni timu tatu kati ya tano zilizopo katika hatua hii zitaanzia ugenini. Hii ni faida kwa timu zetu. Tujitahidi mechi hizi tukazimalizie ugenini. Au zisipate madhara makubwa ugenini. Kama ni kufungwa basi isiwe kwa tofauti ya mabao mengi, ili zikirudi nyumbani zije kumaliza kazi hapa. Lakini ni vizuri ikiwezekana mechi hizi zikamalizikie ugenini.
“Kama taifa, tuweke kando upinzani wa klabu (hasa Simba na Yanga) linapokuja jambo la kitaifa. Muda wa kugombana upo tu. Tuwe kitu kimoja kitaifa, halafu tukimaliza tunaweza kurudi kugombana, lakini katika mechi hizi za kitaifa tuwe kitu kimoja.
“Tatizo la soka la Zanzibar, ni moja tu ligi haijulikani. Wachezaji hawasajiliwi katika Transfer Matching System (TMS) kwa sababu FIFA haiijui Zanzibar kama ina ligi inachezwa. Hii inaifanya ligi kukosa udhamini. Ligi haijulikani. Lakini kama taifa tunaweza kufanya jambo kwa ajili ya kuiinua ligi ya Zanzibar. Tuziunganishe tuwe na ligi moja ili tule pamoja keki ya taifa.”

Mwandishi wa Mwanaspoti, Mustapha Mtupa amesema baada ya KMKM kuvuka hatua ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika ni kitu kinachostahili kupongezwa huku akizitaka Simba na Yanga kubadilika.
Mtupa amesema KMKM inastahili pongezi kutokana na uwekezaji wao mdogo kulinganisha na klabu nyingine za Simba na Yanga.
“Nawapongeza sana KMKM. Zamani ilikuwa ni rahisi kuona hazina mechi nzuri, zilikuwa zinatoka mapema sana, huwezi kuzilinganisha timu kama KMKM na uwekezaji kama ambao umefanywa na Azam. Hili ililofanya ni jambo kubwa na hatuwadai,” amesema Mtupa.
Aidha, Mtupa amesema licha ya kutocheza vizuri kwenye mechi za awali kwa klabu za Simba na Yanga, bado ana imani nazo lakini amezitaka kujipanga zaidi ili kufuzu hatua ya makundi.
“Sio kitu kigeni kwa Simba na Yanga kufika makundi, lakini wengi wameona wasiwasi baada ya timu husika kuanza kwa kutocheza vizuri, lakini nina imani kubwa kwamba zitabadilika huko mbele.”
Kwa upande wa Mwandishi Mwandamizi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited inayochapisha Gazeti la Mwanaspoti, Khatimu Naheka amesema hana hofu na timu za Tanzania Bara na visiwani katika mchakato wa kufuzu hatua ya makundi ya michuano ya CAF.
“Timu zote za Bara zimekuwa na ushiriki bora kwa maana ya Yanga, Simba, Azam, Singida na hii imechagizwa na uwekezaji mkubwa sana uliofanyika ambao unaakisi hatua inayokwenda nayo kwa maana ya kile tunachokiona sasa,” amesema Naheka.
Pia, Naheka amesema kitu kingine kinachosababisha timu hizo kufanya vizuri ni kutokana na hamasa ya Serikali kutoka kwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Hussein Ali Mwinyi, ambao wamekuwa wakiitoa kwa washiriki.
Wakati huohuo, Naheka amesema hatashangaa kama timu zote za Tanzania zitafuzu hatua ya makundi ya CAF msimu huu baada ya kushinda hatua ya awali ya mchujo.
“Sitashangaa nikiona timu zetu zote zinafuzu hatua ya makundi,” amesema Naheka.
“Haya ni matunda ya uwekezaji ambao unafanywa. Kwa timu za Tanzania Bara ukiiangalia Simba unamwona Mohammed Dewji, ukiiangalia Yanga unaona Ghalib Said Mohammed ‘GSM’, Ukiiangalia Azam FC unaiona familia ya Bakhressa, iko hivyo hivyo kwa kabla kama Singida unawaona wadau wakubwa wakiwamo viongozi kama Mwigulu Nchemba na wadau wengine.
“Hii hamasa ya uwekezaji inachochea mabadiliko ya uwekezaji visiwani Zanzibar ambako unaona timu kama KMKM zimeanza kusajili wachezaji wa kigeni. Sitashangaa nikiona timu zetu zote zikifuzu.”
“Kwa mashabiki, usiende kwa nia kuicheka timu au kuzizomea, nenda kaisapoti. Haina maana kuiombea timu moja ishindwe.”
Mechi za hatua ya pili katika michuano hiyo zinatarajiwa kuchezwa kati ya Oktoba 17 na 19, 2025, kisha marudiano ni kati ya Oktoba 24 na 26, 2025 ambapo washindi wa jumla wanafuzu makundi.
Simba itacheza dhidi ya Nsingizini Hotspur ya Eswatini, wakati Yanga ikikabiliana na Silver Strikers kutoka Malawi. Singida Black Stars itacheza dhidi ya Flambeau du Centre ya Burundi, wakati Azam ni dhidi ya KMKM. Timu zote za Tanzania Bara zitaanzia ugenini, kisha kumalizia nyumbani.