Dar es Salaam. Kampeni za uchaguzi wa mwaka huu zimekuwa na sura tofauti na ilivyozoeleka katika historia ya siasa za Tanzania.
Tofauti na chaguzi zilizopita, mikutano ya hadhara ya juu ya majukwaa, ilikuwa kipimo cha nguvu za wagombea na ilikuwa ikifanyika kwenye viwanja, lakini safari hii hali ni tofauti.
Wagombea wameonekana kushuka mitaani, masokoni, nyumba kwa nyumba na hata kwenye vijiwe vya kahawa, kama mbinu ya kusaka kura, huku shamrashamra za kawaida zikikosekana. Hata katika miji mikubwa ikiwamo Dar es Salaam, hali imesalia tulivu, badala ya mikutano mikubwa, wagombea sasa wanabeba hoja na ahadi zao mtaa kwa mtaa, nyumba kwa nyumba, wakijumuika na wananchi kwenye shughuli zao za kila siku.
Mtindo huu mpya umeibua taswira ya kampeni zinazotazamwa kuwa za karibu zaidi na wananchi.
Wapo wanaosema uchaguzi wa mwaka huu umepoa kwa kukosekana mikiki mikiki ya majukwaani, lakini kwa wanaofikiwa moja kwa moja, mvutano wa hoja unaendelea kwa kasi ileile.
Mwananchi imezungumza na wagombea sambamba na wananchi kuhusiana na hali hii.
Mgombea Udiwani wa Kata ya Mbagala kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Hadija Mwago amesema hali ya kisiasa imeathiriwa na changamoto za maisha ya kila siku.
“Wananchi wengi wako bize kutafuta kipato, hivyo hawana muda wa kuhudhuria mikutano mikubwa ya hadhara. Hamasa ya mikutano imepungua sana, kwa hiyo tunalazimika kushuka chini na kuwafuata majumbani na kwenye shughuli zao za kila siku,” amesema.
Amesema mikutano ya hadhara haijapoteza maana kabisa, lakini imepoteza mvuto wa kuvutia umati mkubwa.
Kauli hiyo inaungwa mkono na mgombea wa Chaumma Jimbo la Kawe, Dorcas Francis anayesema kampeni za mwaka huu haziwezi kutegemea mbwembwe za kujaza viwanja.
“Leo hii watu wanataka nauli na posho ili waje mikutanoni, maana wengi wapo bize na kazi. Sioni maana ya kusomba watu kwenye magari ili kuonesha mkutano umejaa. Mimi naona bora nitembee nyumba kwa nyumba. Huko nakutana na wapigakura halisi, wanauliza maswali na mimi najibu moja kwa moja,” amesema.
Dorcas amesema mbinu hiyo imemsaidia kuelewa changamoto halisi za wananchi wa jimbo lake, kuanzia huduma za kijamii, biashara ndogondogo hadi mitazamo ya kisiasa kitaifa.
Kwa upande wake, mwanasiasa mkongwe na mgombea anayetetea Jimbo la Ubungo kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Profesa Kitila Mkumbo amesema mikutano ya hadhara haiwezi kupewa uzito mkubwa.
“Utaalamu unaonesha mikutano ya hadhara inaweza kukuletea kati ya asilimia tatu hadi kumi pekee ya kura. Lakini kuwatembelea watu moja kwa moja ndiko kunakoongeza nafasi ya kupata kura,” amesema Profesa huyo.
Wachambuzi wa siasa waliozungumza na Mwananchi akiwamo Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Dk Paul Loisulie amesema hali hii ni kielelezo cha mabadiliko ya mienendo ya kisiasa nchini.
Dk Loisulie amesema kwa muda mrefu, kujaza viwanja na barabara kulichukuliwa kuwa kipimo cha uwezo na umaarufu wa mgombea, lakini sasa wagombea wameanza kuelewa kuwa umati wa watu si kigezo cha kupigiwa kura.
“Hali ya uchumi na mabadiliko ya kijamii yamechangia wananchi kutilia shaka thamani ya kuhudhuria mikutano isiyo na manufaa ya moja kwa moja kwao. Wengi wanataka mgombea awafuate, asikilize shida zao na atoe majibu badala ya maneno ya jumla jukwaani,” amesema mchambuzi huyo.
Amesema kukosekana pia kwa ushindani mkubwa wa kisiasa nchini, ndiko kumeondoa hamasa iliyokuwapo.
“Kukosekana kwa vyama na wagombea wenye ushawishi mkubwa ndicho kimesababisha kupoa kwa kampeni. Ushindani huleta amsha amsha, na pale ambako hakuna, hali hubaki tulivu,” amesema Dk Loisulie.
Mchambuzi mwingine, Dk Benson Bana amesema muundo wa kampeni unategemea mazingira na hakuna fomula moja.
Amebainisha kuwa,mwaka huu kampeni zimepoa kutokana na ukosefu wa chama kikuu cha upinzani, (Chadema), ambacho kimekuwa kikionekana kuleta changamoto kubwa kwa chama tawala.
“Ni tofauti na Zanzibar, ambako vyama viwili vya CCM na ACT – Wazalendo vinasimama vizuri. Bara, chama kimoja pekee ndicho chenye nguvu, hivyo hakuna mvuto mkubwa wa kisiasa,” amesema Dk Bana.
Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha Bodaboda eneo la Bunju jijini Dar es Salaam, John Maganga amesema: “Watu wamechoka kushangilia majukwaani bila kuona mabadiliko kwenye maisha yao. Ndiyo maana mbinu hii mpya ya kampeni inapata nafasi kubwa.”
Amesema wananchi pia wameanza kuona faida ya kampeni za ana kwa ana. “Mtu anapokuja moja kwa moja nyumbani kwako, unajua huyu anakuhitaji kweli. Unaweza kumuuliza maswali magumu na unamsikia akijibu kwa sauti yake mwenyewe. Hii ni tofauti na mikutano yenye kelele na nyimbo.”
Hata hivyo, wachambuzi wamesema mikutano ya hadhara haiwezi kuondoka kabisa kwenye siasa za Tanzania.
Bado inabaki na nafasi yake ya kuonesha mshikamano wa vyama na kusambaza ujumbe wa kisiasa kwa hadhara. Lakini mbinu ya ana kwa ana inatarajiwa kuendelea kushika kasi hasa mijini, ambako watu wana shughuli nyingi na muda mdogo.
Baadhi ya wagombea mkoani Mbeya wamesema kutokana na ukata wameamua kutumia mbinu na njia mbalimbali kufanya kampeni kuomba kura kwa wananchi.
Mgombea ubunge wa Uyole kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Ipyana Njiku amesema baada ya mkutano wake uliojumuisha mgombea urais wa chama hicho, Salum Mwalimu, ameanza kupita nyumba kwa nyumba na kugawa vipeperushi.
Amesema pamoja na changamoto za kuwafikia wananchi mmoja mmoja, anaamini kupitia njia hizo anaweza kufikisha sera na ujumbe wa chama, kuomba kura akieleza matarajio yake ni kushinda Oktoba 29.
“Nimefanya mkutano mmoja Jumamosi iliyopita, nilikuwa na mgombea urais, Mwalimu, kwa sasa natumia vipeperushi na kutembea nyumba kwa nyumba kuomba kura, kunadi sera na kukitangaza chama, naamini wananchi wananielewa,” amesema Njiku.
Mgombea ubunge wa Mbeya Mjini kupitia Tanzania Labour Party (TLP), Shila Madoki amesema kutokana na hali ngumu ya uchumi kuanzia kwenye chama hadi yeye binafsi, ameamua kutumia pikipiki na baiskeli kutembelea makundi kuomba kura na kutangaza chama.
Amesema changamoto kubwa anayokutana nayo ni wananchi wengi kudhani TLP imepotea, hivyo anajikuta anafanya kazi mbili kwa wakati mmoja akijipa matumaini ya kufanya vizuri.
Mmoja wa wananchi, Salum Ally mkazi wa Sokoine jijini Mbeya, amesema uchaguzi wa mwaka huu umekuwa wa upande mmoja ikilinganishwa na chaguzi za nyuma.
“Mwaka huu akiwapo mgombea urais hakuna mgombea ubunge anaruhusiwa kufanya kampeni, lakini nguvu kubwa zaidi inaonekana kwa chama kimoja.
“Zamani tuliona vyama vingi vya upinzani lakini kwa mwaka huu hawa waliopo nguvu yao siyo kubwa, sasa wanaona wasitumie nguvu kubwa kupambana na wasiowaweza, ingekuwapo Chadema tungeona uhalisia wa kampeni,” amesema Ally.
Naye Lilian Temu ambaye ni mamalishe amesema kampeni za mwaka huu hazijachangamka akidai vyama vya upinzani vinavyoshiriki havina nguvu.
Nako wilayani Tarime mkoani Mara, baadhi ya wagombea hao wa ubunge na udiwani hawafanyi kampeni za majukwaani badala yake, wanazisaka kura mitaani na kwenye maeneo ya biashara na yale yenye mikusanyiko ya watu.
Mwananchi imewashudia wagombe ubunge Mgore Miraji (CCM), Angela Lima (Chaumma), Christina Ndengo (Sau), Omari Mohamed (CUF) na Hassan Ogola (Makini), wakipita mtaa kwa mtaa wakifanya kampeni zao za kuomba kura.