Buhigwe. Wananchi wa Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma wamesema kufunguliwa rasmi kwa ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wilayani humo kutasaidia kuwepo kwa usiri na usalama wao wa utoaji taarifa kuhusu vitendo vya rushwa ukilinganisha na hapo awali.
Wakizungumza leo, Alhamisi Oktoba 2, 2025 wakati wa uzinduzi wa jengo la ofisi ya Takukuru Wilaya ya Buhigwe, wananchi hao wamesema taasisi hiyo ilipanga ndani ya makazi ya wananchi, hivyo wananchi hao kuwa na hofu na usalama wao wakati wa utoaji taarifa zao.
Mkazi wa Buhigwe, Lukas Kabiga amesema kuwepo kwa ofisi hiyo itawarahisishia utoaji wa taarifa za viashiria vya vitendo vya rushwa na kuwa na uhakika wa usalama na taarifa zao kwani iko mbali na makazi ya watu na hakuna mtu atakayeona wakati akienda kutoa taarifa zao.

Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Chalamila (katikati aliyevaa stafu shingoni?akifungua jengo jipya la ofisi za Taasisi hiyo wilayani Buhigwe, leo Alhamisi Oktoba 2, 2025
“Awali, ofisi za Takukuru zilikuwa kijijini kabisa ukiingia na kutoka wananchi wanakuona hiyo ilikuwa inatupa hofu kama wananchi wa taarifa zetu tunazoenda kutoa na pia tulikuwa tunahofia usalama, lakini hapa ilipojengwa, kwanza ni karibu na ofisi ya Mkuu wa Wilaya na ukienda kutoa taarifa hakuna mtu anayekuona,” amesema Kabiga.
Naye Jumanne Kwiha, amesema kuna matukio mengi ya viashiria vya vitendo vya rushwa katika eneo lao na kwa kipindi hichi cha kampeni kuelekea uchaguzi, hivyo wako tayari kutoa ushirikiano kwa Takukuru kutoa taarifa wakiwa na uhakika wa usalama wao baada ya kufunguliwa kwa ofisi hiyo rasmi eneo ambalo sio kwenye makazi ya watu tofauti na awali ilipokuwepo.
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Crispin Chalamila amesema taasisi hiyo imejiwekea mkakati wa kudumu na endelevu wa kutenga bajeti ya kujenga ofisi zake kila mwaka, kwa kuzingatia kuwa taasisi hiyo ina ofisi 145 katika mikoa ya kiTakukuru 28, wilaya 111 pamoja na vituo maalumu sita.
Chalamila amesema kwa ujumla wake kati ya ofisi hizo 145, majengo ya mikoa yanayomilikiwa na Takukuru ni 70 na kwamba katika mwaka wa fedha 2025/26 majengo yatakayojengwa ni 11, huku ofisi ambazo bado hazijajengwa 64.
Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Kanali Michael Ngayalina amesema uwekezaji huo uliofanywa na serikali wanataka wauone kwenye utekelezaji wa majukumu yao, waone thamani ya fedha katika majengo, vitendea kazi na katika kazi wanazozifanya moja kwa moja kwa manufaa ya wananchi.
“Tunataka tuone mnazuia na kudhibiti udanganyifu, kuzuia na kudhibiti ubathilifu wa mali ya umma, kudhibiti na kufatilia utekelezaji wa miradi yote ya umma, kuendelea kutoa elimu na uelewa dhidi ya mapambano ya rushwa kupitia majukwaa mbalimbali na klabu zilizopo mashuleni,” amesema Ngayalina.
Akizungumzia ujenzi wa ofisi hiyo, Mkurugenzi wa Miliki Takukuru, Emmanuel Kiyabo amesema ujenzi ulianza Novemba Mosi, 2024 kwa kipindi cha miezi sita ambayo ulikamilika Juni Mosi, 2025 huku gharama za mradi zilikuwa zaidi ya Sh382 bilioni.