Watatu walioshtakiwa kumuua bodaboda wahukumiwa kifo

Arusha. Mahakama Kuu Masjala ndogo ya Geita, imewahukumu watu watatu adhabu ya kunyongwa hadi kufa baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la mauaji ya dereva bodaboda.

Waliohukumiwa adhabu hiyo ni Faraji Liyugana, Said Ponera na Rashid Fussi ambao walishtakiwa kwa mauaji ya Fanyeni Adam, kosa walilolitenda kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu.

Jaji James Karayemaha alitoa hukumu hiyo Septemba 29,2025 na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa mahakama.

Mauaji hayo yalitokea Januari 12, 2023, ambapo baada ya kumuua dereva huyo wa bodaboda waliutelekeza mwili wake porini karibu na eneo la Tanesco, Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma.

Baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili, Jaji Karayemaha alieleza kuwa Mahakama imewakuta washtakiwa wote watatu na hatia ya mauaji na kuwahukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.

Miongoni mwa ushahidi uliotumika kuwatia hatiani ni pamoja na maelezo ya onyo ya washtakiwa wa pili na wa tatu (Said na Rashid) ambao walikiri kuhusika na mauaji hayo kwa kushirikiana na mtuhumiwa mwenzao.

Ilielezwa mahakamani hapo kuwa marehemu alikuwa akiendesha pikipiki ambayo mmiliki wake ni Abbasy Gangisa, ambaye aliikabidhi kwa shahidi wa 12, Faraji Ngonyani, ili aitumie kupata fedha watakazogawana.

Shahidi wa 12 alisema kumkabidhi Fanyeni (marehemu kwa sasa) pikipiki hiyo ili aiendeshe kwa ajili ya biashara kwa malipo ya kila siku Sh10,000 waliyokubaliana.

Shahidi wa sita, alisema Januari 12, 2023 Fanyeni (marehemu) alienda nyumbani kwake akiwa na rafiki yake, Yasin Lika na walimjulisha kuwa walikuwa wakielekea shambani eneo la Tanesco kuchukua jembe, ila usiku huo hakurudi nyumbani.

Alisema siku iliyofuata walianza kumtafuta ambapo walimuulizia hadi kwa shahidi wa 12, lakini hakujulikana alipo hadi Januari 14, 2023 mwili wake ulipokutwa ukiwa porini na shahidi wa tisa, Mariju Mwenyeheri (mmiliki wa shamba lililokuwa karibu na eneo la Tanesco).

Tukio hilo liliripotiwa polisi ambao walifika eneo la tukio   na kuchukua mwili huo uliokutwa na jeraha ambapo pikipiki aliyokuwa akiitumia kwa ajili ya biashara hakukutwa nayo ila simu yake ilikutwa eneo hilo.

Shahidi wa pili, SP Cathbet Mnogi kwa kushirikiana na wapelelezi wengine na raia, walidokezwa washtakiwa waliomuua Fanyeni ambapo kwa mujibu wa maelezo ya mtoa taarifa alisema kuwa wauaji hao walikuwa marafiki wa Yasin na marehemu pia.

Ilielezwa mahakamani hapo kuwa kutokana na ushahidi uliokusanywa shahidi wa pili alikwenda nyumbani kwa mshtakiwa wa kwanza aliyekuwa akiishi na mchumba wake, Ziaba Saidi (shahidi wa tatu wa Jamhuri), baada ya kujulishwa pikipiki hiyo ilikuwa nyumbani kwao.

Akisaidiwa na shahidi wa saba, Sejasi Milinga, ambaye wakati huo alikuwa Mwenyekiti wa kitongoji cha Changarawe, msako ulifanyika na kufanikiwa kuipata pikipiki hiyo.

Akihojiwa na shahidi wa pili na saba, shahidi wa tatu alidai kuwa mshtakiwa wa kwanza alimweleza kuwa pikipiki hiyo ni mali ya rafiki yake ambaye anadaiwa Sh300,000.

Shahidi huyo alisema kuwa rafiki huyo ambaye jina lake halikutajwa alishindwa kumlipa hivyo pikipiki hiyo ilichukuliwa ili alazimishwe kulipa deni hilo.

Shahidi wa pili alisema kuwa wakati wa mahojiano mshtakiwa wa kwanza alikiri kuhusika na mauaji hayo na kuwataja washtakiwa wa pili na tatu kumsaidia katika tukio hilo na kuwa baada ya mauaji hayo walimkabidhi mshtakiwa wa kwanza pikipiki, ili akaiuze kisha fedha inayopatikana wagawane wote watatu.

Mshtakiwa wa kwanza alisema Januari 24, 2023 akiwa nyumbani kwake, rafiki yake (Yasin) alimwomba amuhifadhie pikipiki hiyo ila kwa bahati mbaya Yasin hakurudi hadi maofisa wa Polisi walipoenda kupekua nyumba yake na kuikuta kisha kuchukua pikipiki hiyo.

Alisema muda mfupi baadaye, alipelekwa Kituo cha Polisi Namtumbo akiwa na pikipiki hiyo, akidai hakuwahi kuwataja washtakiwa wenzake na hawakuwa marafiki zake.

Akihojiwa na upande wa mashtaka, alikiri kuwa shahidi wa tatu wa Jamhuri ni mchumba wake huku akikana kuipeleka pikipiki hiyo nyumbani kwao.

Mshtakiwa wa pili alijitetea kuwa alikamatwa Januari 15, 2023 usiku na kupelekwa Kituo cha Polisi Nambumbo na kujulishwa anakabiliwa na kesi ya mauaji, huku akikana kuandika maelezo ya onyo mbele ya shahidi wa nane na kukana kuwafahamu washtakiwa wenzake.

Mshtakiwa wa tatu alidai kukamatwa Januari 15, 2023 akiwa nyumbani kwake na kupelekwa kituo cha polisi alikoambiwa anakabiliwa na kesi ya mauaji, na kuwa ilikuwa mara yake ya kwanza siku hiyo kukutana na washtakiwa wenzake huku akikana kuandika maelezo ya onyo kwa shahidi wa 10.

Jaji Kayaremaha, alisema baada ya kuzingatia ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo na pande zote mbili, masuala mawili yanayohitaji uamuzi ni ikiwa kifo hicho hakikuwa cha asili, na iwapo watuhumiwa ndiyo walifanya mauaji hayo kwa nia mbaya.

Alisema kwa ushahidi uliopo ni wazi kuwa kifo hicho hakikuwa cha asili, ushahidi ambao ulithibitishwa na daktari aliyeufanyia mwili huo  uchunguzi ambaye alieleza ulikutwa ukiwa na jeraha kubwa karibu na fuvu la kichwa.

Jaji alisema suala linalofuata ni kuhusu nani alimuua Fanyeni ambapo kutokana na ushahidi wa mashtaka uliotolewa mahakamani hapo hakuna shahidi aliyeshuhudia kwamba aliwaona washtakiwa wakimuua mtu.

Alisema katika kesi hiyo mazingira ambayo yanawahusisha washtakiwa ni kuanzia mshtakiwa wa kwanza alipokamatwa akiwa na kielelezo (pikipiki), ambayo ilikuwa ikitumiwa na marehemu katika biashara zake.

Alieleza  kuwa baada ya kifo cha Fanyeni mshtakiwa wa kwanza  kukutwa na mali za marehemu ni kielelezo kuwa aliuawa kwanza na kisha kuibiwa pikipiki.

Alisema na  baada ya kupitia kwa kina ushahidi wa shahidi wa pili, wa tano,  wa nane, wa tisa, 10 na 12 unaonyesha baada ya Fanyeni kushambuliwa aliuawa.

Jaji aliongeza kuwa katika utetezi wake, Faraji hakukana kuwa alikutwa na pikipiki tajwa na kwamba si yake.

Jaji alinukuu maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa pili (Said) ambaye alikiri Januari 10,2023 marafiki zake ambao ni Yasin, Faraji (mshtakiwa wa kwanza), na Rashidi aliwaeleza anahitaji pikipiki, hivyo wamteke mtu na kunyang’anya pikipiki kisha atawapatia Sh1 milioni.

Alinukuliwa akieleza kuwa walipanga kumlaghai dereva bodaboda na kumpeleka maeneo ya Tanesco, ambapo walimnyang’anya, na kabla ya tukio hilo Yasin alienda nyumbani kwake kuazima panga lake jipya alilonunua.

Kupitia maelezo hayo mshtakiwa huyo alieleza mchakato mzima wa namna walivyopanga kumnyang’anya dereva huyo pikipiki yake  ambayo Yasin alibeba panga hilo alilomkabidhi Faraji ambaye alimkata marehemu kichwani, wao wakampiga  na kumkata kwa panga hadi alipofariki dunia, ila Yasin hakufanya lolote alisimama kuwaangalia tu.

Jaji alinukuu maelezo ya mshtakiwa wa tatu ambaye pia alitoa maelezo yanayofanana na ya mshtakiwa wa pili na kueleza kuwa yeye alipewa jukumu la kusimama njiani kusubiri pikipiki ifike ili wamvamie na kuipora ambapo alichukua kipande cha mti na kujificha.

Mshtakiwa huyo alinukuliwa akieleza kuwa Yasin aliyekuwa amepakiwa kama abiria, alishuka kwenye pikipiki hiyo na Faraji aliyekuwa ameshika panga alikimbilia kumkata kichwani na dereva alipotaka kukimbia alimpiga kichwani.

Jaji alisema ni wazi kuwa katika maelezo ya onyo ya washtakiwa wa pili na tatu, walitajana na kumtaja zaidi mshtakiwa wa kwanza na kuwa maelezo hayo waliyatoa kwa hiari, hivyo ni sehemu ya ushahidi uliotumika kuwatia hatiani washtakiwa hao.

Baada ya kuchambua ushahidi wa pande zote Mahakama hiyo iliwatia hatiani washtakiwa wote watatu kwa kosa la mauaji na kuwahukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.