Dar es Salaam. Wafanyabiashara wawili Ibrahim Mohamed na Matei Joseph, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 57 yakiwemo ya kughushi wito wa Polisi wakionyesha umetolewa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi na kuongoza genge la uhalifu.
Mashtaka mengine ni kughushi cheti cha ndoa, cheti cha kifo, cheti cha kuzaliwa, hati za viwanja, mihuri kutoka Benki ya CRDB na DTB namba ya mlipakodi kutoka TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania), kughushi mhuri wa Mahakama ya Mkoa wa Vuga na muhuri wa Mkuu wa Kituo cha Polisi Madema kilichopo Mjini Unguja.
Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka yao, leo Oktoba 2, 2025 na Wakili wa Serikali, Roida Mwakamele mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini.
Kati ya mashtaka hayo 57, mashtaka 42 ni ya kughushi nyaraka mbalimbali, moja kuongoza genge la uhalifu na lingine ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, ambapo mashtaka 56 yanamkabili Ibrahimu peke yake.

Wakili Roida amedai washtakiwa hao wanadaiwa kati ya mwaka 2023 na Septemba 2025 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, waliongoza genge la uhalifu na kughushi.
Wakili huyo alidai, katika tarehe hizo, mshtakiwa Mohamed anadaiwa kughushi barua ya Septemba 4, 2024 ikionesha Bendi ya African Minofu ilialikwa kwenda Paris nchini Ufaransa, na Christine Mleary kushiriki tamasha la majadiliano ya muziki wa mama “Mama Music conversation Fastival”, wakati akijua kuwa ni uongo.
Ilidaiwa, mshtakiwa huyo pia anakabiliwa na mashtaka manne ya kughushi nyaraka mbalimbali ikiwemo hati ya dhamana, wito wa polisi, hati za malipo na cheti cha kuzaliwa.
Iliendelea kudaiwa, katika kipindi hicho mshtakiwa anadaiwa kujipatia Sh1.5 milioni kutoka kwa watu mbalimbali kutokana na mashtaka ya kumiliki mihuri.
Washtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yao, upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Hakimu Mhini alitoa masharti manne ya dhamana ambapo, mosi kila mshtakiwa anatakiwa awe na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh8 milioni kila mmoja.
Pia, wadhamini hao wawe wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na sio vinginevyo.
Vile vile , wadhamini hao wanatakiwa kuwa na barua za utambulisho kutoka serikali ya mtaa na pia wawe na kitambulisho cha Nida.
Washtakiwa walifanikiwa kutimiza masharti ya dhamana na kuachiwa kwa dhamana.
Hakimu Mhini aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 30, 2025 kwa ajili ya kutajwa.