Unguja. Wakati ikiadhimishwa siku ya wazee duniani, wazee kisiwani hapa wameiomba Serikali kuwaboreshea huduma za upatikanaji wa fedha za pensheni vijijini, kwani ufuatiliaji wake umekuwa na changamoto kwao.
Hayo yameelezwa leo Oktoba Mosi, 2025 katika maadhimisho ya wazee duniani yaliyofanyika Sebleni, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Jaku Jabu kutoka Matemwe, amesema pensheni ya wazee imekuwa na ugumu wa kuipata kwani wanatumia kilomita tano kufuatilia huduma za benki ili kupata fedha hizo.
Pia, amesema awali waliambiwa kuwa Sh50,000 inayotolewa na Serikali haitakuwa makato badala yake itatolewa yote kwao, ila kinachowashangaza ni kukatwa Sh3,000 kutoka katika fedha hizo hivyo wanahitaji kuelewa inakwenda wapi.
“Tunatumia masafa ya kilomita tano kufuata fedha ya pensheni Sh50,000 hii ni changamoto upande wetu, pia tunahitaji kueleweshwa kuhusu makato ya Sh3,000 yanakwenda wapi kwani awali tuliambiwa fedha hizo hazina makato,” amesema Jaku.
Mbali na hilo, Jaku ameiomba Serikali kuboresha miundombinu kwa sababu nyumba ambazo zinajengwa Mjini, kwa upande wa vijijini bado hawajafikiwa kwa maana hiyo wazee wa mjini ndio wanafaidika zaidi kuliko vijijini.
Naye, Fatma Hamza Amir amesema anapata faraja kuona kufikia umri huo akiwa mzima wa afya na viungo bado vikiwa vinafanya kazi vizuri na anafurahi Serikali kuwapa hadhi inayowafanya kutambulika kitaifa.
Fatma, ametoa wito kwa watoto ambao hawaoni thamani ya wazee waelewe kuwa ipo siku watafikia hatua hiyo, hivyo ikiwa hawahitaji kudharauliwa wasiwafanyie wazee mambo yasiyostahili.
Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Abeda Rashid Abdalla amesema bado wanahitaji kupaza sauti kwa ajili ya kutafuta haki zao na kutathmini maendeleo yao.
Amesema, maendeleo hayawezi kufikiwa bila ushirikishwaji wa wazee kwa sababu wana busara, hekima na maarifa hivyo wananchi waendelee kuwathamini wazazi wao.
Vilevile, amesema Serikali inaendelea kufanya juhudi mbalimbali za kuimarisha mazingira kwa wazee ikiwemo kuwapatia huduma za afya, usafiri na kuwajengea nyumba zenye hadhi.
Naye, Mwakilishi kutoka Shirika la Idadi ya Watu Duniani (UNFP), Dk Azzah Amin Nofli amesema siku hiyo sio ishara pekee ya heshima bali ni ya mwito wa kutafakari changamoto wanazokutana nazo.
Amesema, maadhimisho hayo yanatoa nafasi ya kutetea sera na programu zinazolenga mahitaji yao ikiwemo upatikanaji wa huduma bora za afya, ulinzi wa kijamii na namna ya kujitunza.
Ameeleza kuwa, maarifa yao ni hazina ya Taifa yanayoweza kuwaongoza vijana katika kuimarisha ushirikiano wa kwa jamii.