NIKAFIKIRIA kwamba ni vyema kama ningepata historia zaidi ya Christopher, ambaye ni baba yake Thomas tunayemtuhumu kwa mauaji.
Nikaona hakukuwa na mtu mwingine yeyote ambaye angeitambua historia ya Christopher isipokuwa yule mzee wa Makorora. Nikakusudia kwamba siku itakayofuata nimfuate na kumhoji zaidi.
Sikuona taabu kwenda kumhoji tena kwa sababu nilishamwambia kwamba endapo ningekuwa na la zaidi ningerudi tena kwake, na yeye akanikubalia.
Saa moja kamili usiku nikalisimamisha gari mbele ya nyumba ya Hamisa. Nilishuka kwenye gari nikaenda kwenye mlango. Nilibisha mlango kisha nikasubiri. Baada ya sekunde kadhaa mlango ukafunguliwa na binti mzuri aliyekuwa ameremba uso wake na kung’arika.
“Karibu,” akaniambia huku akiondoka mlangoni na kurudi ndani.
Niliingia ndani nikafunga mlango kisha nikamfuata sebuleni.
“Ndiyo umenifuata?” akaniuliza.
“Ndiyo. Ni saa moja sasa.”
“Subiri nivae tutoke. Nilikuwa nikijiandaa.”
Nikakaa kwenye kochi. Hamisa akaingia chumbani kwake.
Alichelewa sana humo chumbani mpaka nikainuka na kumfuata. Nikamkuta bado akijitazama kwenye kioo.
“Twenzetu, umeshapendeza,” nikamwambia.
Alikuwa amevaa suruali ya jeans, t-shirt na viatu vya mchuchumio.
“Nimependeza?” akaniuliza huku akitabasamu.
“Umependeza sana, mchumba wangu.”
Nikaielekeza midomo yangu kwake ili nimbusu. Akanisogezea uso wake na tukabusiana, kitendo ambacho kilinipa faraja ya ajabu.
Nikamshika mkono na kutoka naye.
Tukiwa kwenye gari Hamisa aliniambia:
“Si unajua kesho nakwenda kazini, nisingependelea tuchelewe sana.”
“Hapana, hatutachelewa. Tunakwenda kula tu. Baada ya hapo nakurudisha nyumbani.”
“Sawa.”
Tulikwenda Nyumbani Hotel. Tulikula, tulikunywa na kuzungumza hadi saa tatu tulipoondoka. Nilimrudisha Hamisa nyumbani kwake. Mimi sikushuka kwenye gari. Hamisa alipofungua mlango wake ndipo nilipoondoka.
Nikarudi nyumbani kwangu kulala.
Nilipoondoka nyumbani asubuhi nilikwenda ofisini kwangu kisha nikatoka kwenda Makorora kwa mzee Mustafa Abuu.
Kama kawaida nilipobisha hodi nyumbani kwake niliitikiwa na yule mwanamke aliyenikaribisha jana yake.
Baada ya kusalimiana naye aliniuliza:
“Umemfuata mzee Mustafa?”
“Ndiyo. Nimemfuata mzee Mustafa.”
“Karibu ndani,” akaniambia.
Nikaingia ndani. Mwanamke huyo alinipeleka katika chumba cha mzee huyo.
Nilimkuta amekaa kitandani. Kile kiti nilichokalia jana yake kilikuwa kipo pale pale.
Nikamwamkia mzee huyo kisha nikaketi.
“Natumaini umenikumbuka?” nikamuuliza.
“Nimekukumbuka. Wewe si yule kijana uliyekuja jana kumuulizia Thoms Christopher?”
“Naam. Ndiye mimi.”
“Karibu sana.”
“Asante. Kilichonirudisha tena kwako hii leo ni kuhusu marehemu Christopher ambaye uliniambia jana kwamba unamfahamu.”
“Ndiyo, ninamfahamu lakini kumfahamu kwangu kulianzia nilipoajiriwa na Unyeke. Wakati ule Christopher alikuwa mgonjwa.”
“Kutokana na kumfahamu kwako unaweza kuniambia huyu mtu alikuwa mtu wa wapi?”
“Alivyonieleza Unyeke ni kwamba huyu mtu ni Mnyasa aliyetokea Songea.”
“Alipokuja hapa hakuwa na mtoto?”
“Alikuja akiwa kijana sana. Alikuwa hajaoa bado. Mtoto alimpata baadaye baada ya kuanza kazi ya madini ambayo ilimtajirisha. Alioa mwanamke wa Kipare ambaye alimzaa Thomas.”
“Jana uliniambia kwamba Christopher alimuachia mali zake Unyeke, kwani hakuwa na ndugu?”
“Kwa hapa Tanga hakuwa na ndugu, sijui huko kwao Unyasa. Lakini hata kama alikuwa nao ndugu, aliondoka kwao miaka mingi akalowea huku. Ni wazi kwamba hawakuwa na mawasiliano.”
“Kwa kadiri unavyofahamu wewe, hakuwahi kurudi kwao?”
“Hakuwahi kurudi, hata kuzikwa alizikwa na Unyeke hapa hapa.”
Mzee aliwaza kidogo kisha akaniambia:
“Umeniuliza kuhusu Christopher kuwa na ndugu. Kuna tukio nimelikumbuka. Siku chache baada ya Christopher kufa alikuja mwanamke mmoja pamoja na mwanawe wa umri kati ya miaka ishirini na minane hadi thelathini. Yule mwanamke alidai kuwa Christopher ni ndugu yake ambaye aliasiana naye tangu walipokuwa wadogo.”
“Huyo mwanamke na huyo mwanawe walikuja kutoka wapi?”
“Walikuja kutoka Songea lakini walipokuja Unyeke alikuwa ameshakufa na Thomas naye ameshauawa. Alikaa Chuda kwa karibu wiki moja. Kwa vile hakukuwa na yeyote aliyemtambua ilibidi waondoke warudi walikotoka. Baadhi ya watu walishuku kwamba walikuwa matapeli waliokuwa wanataka mali ya marehemu.”
“Huyo mwanamke alidai kwamba alikuwa ndugu yake Christopher?”
“Ndiyo, alidai hivyo. Tulimuuliza, ‘Siku zote hizo ulikuwa wapi? Umengoja hadi hawa watu wote wamekufa ndio unakuja kujitambulisha?’ Lakini hakuwa na jibu.”
“Baada ya huyo mwanamke kurudi kwao aliwahi kuja tena?”
“Sijui. Na hata kama alikuja angempata nani wa kumuuliza wakati mali za Christopher zimechukuliwa na serikali.”
“Hapo mara ya kwanza alipokuja ulizungumza naye?”
“Ndiyo, nilizungumza naye na pia alinipa namba yake ya simu. Alinihakikishia kwamba Christopher alikuwa ndugu yake tumbo moja, walizaliwa wao wawili tu.”
“Hiyo namba ya simu aliyokupa bado unayo?”
“Nafikiri ninayo. Mimi huwa sifuti namba ovyo ovyo.”
Mzee alitia mkono kwenye mfuko wa shati alilokuwa amevaa, akachomoa miwani yake na kuivaa kisha akachukua simu yake iliyokuwa chini ya mto akaanza kuitafuta namba hiyo.
Baada ya sekunde chache alinambia:
“Hii hapa.”
“Nitajie namba zenyewe.”
Mzee huyo akanitajia namba hizo. Niliziandika kwenye simu yangu.
“Alikwambia anaitwa nani?”
“Jina lake nimeliandika hapa… anaitwa Margaret.”
Niliandika jina hilo na kulihifadhi kwenye simu yangu.
“Hebu jaribu kuipiga kwa maana sijaipiga hata siku moja.”
Nikaipiga ile namba.
Namba hiyo haikupatikana.
“Haipatikani.”
“Ni muda mrefu, sijui kama bado anaitumia au ameiacha lakini namba yake ni hiyo.”
“Nitaijaribu tena baadaye.”
“Sawa.”
“Ni hilo tu mzee wangu lililonileta kwako kwa leo.”
“Nakushukuru pia kwa kuja kunitembelea.”
“Asante sana,” nikamwambia kisha nikampa mkono kabla ya kunyanyuka kwenye kiti.
“Ninakwenda lakini naamini tutaonana tena.”
“Asante na karibu sana.”
Nikatoka na kujipakia kwenye gari. Nilirudi kituoni nikaingia ofisini kwangu. Wakati nakaa kwenye kiti simu yangu ikaita.
Nikaitoa kwenye mfuko wa koti langu na kutazama namba iliyokuwa inapiga. Ilikuwa namba ngeni kwangu. Nikaipokea.
“Hello…!”
“Natumaini nazungumza na Inspekta Fadhil?” Sauti ya kiume ikasikika kwenye simu.
“Ndiyo. Nani mwenzangu?”
“Ni mtu muhimu sana kwako. Ninahitaji kuonana na wewe.”
“Unadhani ninakufahamu?”
“Unanifahamu bila kuniona lakini nataka unione.”
“Ninakufahamu vipi?”
“Wewe si unachunguza kuhusu watu wanne walionyongwa hivi karibuni?”
“Ndiyo.”
“Mimi ninazo habari kuhusu watu hao.”
“Basi nakuomba ufike ofisini kwangu tuonane.”
“Bila kuniomba nitafika, najua kwamba unahitaji kuniona.”
“Utafika saa ngapi?”
“Sasa hivi ninakuja, nisubiri.”
“Sawa. Nakusubiri.”
Simu ya upande wa pili ikakatwa.
Nikawa najiuliza, mtu huyo alikuwa nani? Kwanini aseme kuwa alikuwa mtu muhimu kwangu? Ameniambia ana habari kuhusu watu wanne waliokuwa wamenyongwa, je yeye ni nani?
Maswali yaliyokosa majibu yakapita katika akili yangu.
Niseme ukweli mtu huyo alinitia shauku kubwa ya kumuona. Nikakaa mkao wa kumsubiri kwa hamu.
Hazikupita hata dakika thelathini polisi mmoja aliingia ofisini kwangu na kuniambia kwamba kulikuwa na raia aliyekuwa akiniuliza.
“Mwambie apite ndani.”
Polisi huyo alitoka. Baada ya dakika chache akaingia kijana mmoja aliyekuwa amevaa vizuri. Wakati anaingia ofisini kwangu nilimtazama kuanzia kichwani hadi miguuni nikimlinganisha na mtu aliyenipigia simu.
“Habari ya kazi?” akanisalimia.
“Nzuri. Karibu ukae,” nikamwambia huku nikiendelea kumtazama.
Kijana huyo akakaa.
“Natumaini wewe ndiye Inspekta Fadhil?” akaniuliza.
“Ndiye mimi.”
“Tuliongea kwenye simu dakika chache zilizopita.”
“Kama ni wewe, nilikuwa nakusubiri.”
“Kuna mkasa nataka kukusimulia.”
“Nisimulie.”
“Zamani watoto wawili wa mzee mmoja aliyekuwa akitambulika kwa jina la Gabriel, mmoja akiwa mwanaume na mwingine mwanamke, waliondoka bara na kutawanyika. Yule mtoto wa kike alikwenda kusini na yule wa kiume alikuja hapa Tanga.
“Wakati wanaondoka, hao watoto tayari walikuwa ni wakubwa na walichangukana baada ya wazazi wao kufariki dunia na kuona walikuwa wanapata mateso kutoka kwa ndugu. Yule wa kike alikuja kupata ujauzito huko alikokwenda akazaa mtoto mmoja wa kiume.
“Yule wa kiume naye alioa akapata mtoto mmoja. Lakini ndugu hawa waliotoka huko bara hawakukutana tena na kila mmoja alikuwa hajui mwenzake yuko wapi. Kila mmoja akaendelea na maisha yake bila kumjua mwenzake.
Bado Watatu – 47 | Mwanaspoti
