Mtoto wa aliyewahi kuwa Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, amefikishwa katika mahakama ya Harare nchini humo akikabiliwa na shtaka la kupatikana na dawa za kulevya aina ya bangi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mahakama, Robert Mugabe Jr (33) alikamatwa Jumatano asubuhi alipokuwa akiendesha gari kwenye njia isiyo sahihi na muda mfupi baadaye polisi waligundua kuwapo misokoto miwili ya bangi na kufanya upekuzi katika mabegi yaliokuwa ndani ya gari hilo.
“Katika upekuzi huo kwenye gari watu watano walikamatwa waliokuwamo kwenye gari la mtoto wa kiongozi wa zamani,” imeelezwa.
Hata hivyo, wakili anayemsimamia Mugabe Jr, Ashiel Mugiya amesema wanatarajia kukata rufaa ya kupinga shitaka hilo ambalo amedai kuwa siyo la kweli kwani amedai lina msukumo wa kisiasa ndani yake.
Kutokana na uadui uliowahi utokea siku za nyuma baina baba wa mtoto huyo na rais wa sasa wa Taifa hilo, Emerson Mnangagwa licha ya kwamba wa sasa Mugabe Jr kuwa na ukaribu na kiongozi huyo wa sasa baada ya kifo cha Baba yake kilichotokea 2019.
Mugiya pia amedai kuwa awali polisi walidai kuwa wamepata gramu 0.02 ya bangi wakati karatasi ya mashtaka ya polisi inasema polisi walipata gramu 2.
Mbali na Mugabe Jr Polisi pia waliwakamata watuhumiwa wengine watano ambao walinaswa muda mfupi baada ya uchunguzi uliofanywa na Polisi ulioibua uwepo wa mtandao uliokuwa ukihusiana na tukio hilo.
Imeelezwa kuwa watuhumiwa hao kwa sasa wapo rumande wakingoja uchunguzi ukamilike ili wapandishwe kizimbani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Tukio hili ni mwendelezo wa kukamatwa kwa watoto wa kiongozi huyo wa zamani, kwani 2023, mtoto wa pili wa rais huyo alikamatwa kwa madai ya kuharibu mali na kumtemea mate afisa wa polisi katika tafrija huko Harare.
Imeandikwa na Elidaima Mangela kwa msaada wa Mashirika