Dar City bingwa wa BDL ikiichapa JKT

DAR City imetawazwa kuwa mfalme wa Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), baada ya jioni ya Oktoba 2, 2025 kuivua ubingwa huo JKT.

Wafalme wapya wa BDL, Dar City wameivua ubingwa JKT kufuatia kuifunga mechi ya tatu mfululizo katika fainali za michuano ya msimu huu.

Ushindi wa pointi 76-62 umeirahisishia Dar City kubeba ubingwa huo kwani ni kipigo cha tatu mfululuizo kwa maafande wa JKT baada ya awali kupasuka katika fainali mbili zilizopita.

Awali Dar City iliitambia JKT kwa pointi 68-44 kisha zilipokutana mara ya pili ikaibutua tena kwa pointi 71-64 kabla ya jana Oktoba 2, 2025 kumaliza na ushindi huo ulioifanya fainali kumaliza bila kufikisha mechi tano kama kanuni zilivyo baada ya maafande wa JKT kushindwa kujitutumua, kwani kama ingepanda ushindi mechi hii ya tatu, ingeenda ya nne au hadi ya tano kuamua mbabe.

DA 01


Katika mechi hiyo, washindi hao walimaliza robo ya kwanza kwa ushindi wa 23-20, kisha ile ya pili ilitamba kwa 36-35 na robo ya tatu ikaendeleza ubabe kwa pointi 56-51 kabla ya kufunga hesabu na kubeba taji lililokuwa linashikiliwa na JKT iliyotwaa msimu uliopita kwa kuifunga UDSM Outsiders.

Kwa upande wa Wanawake, DB Lioness ilitetea ubingwa kwa mara ya pili mfululizo baada ya kuitambia JKT Stars katika mechi ya tatu mfululizo wa fainali ikiibuka kidedea kwa pointi 70-49.

DB Lioness ilianza na ushindi wa mechi ya kwanza ikivuna pointi 61-17 kabla ya kushinda tena mechi ya pili kwa pointi 68-48 na ndipo jana ikatamba tena na kutetea taji hilo inalolishikilia tangu msimu uliopita.

DA 02


Kwa ushindi huo, wanadada hao wamevuna Sh10 milioni mbali na kombe na medali, huku washindi wa pili wakipata Sh6 milioni, sawa na kiasi ilichopewa bingwa wa upande wa wanaume Dar City.

Katika fainali hizo wachezaji Ally Abdallah wa Dar City na Michele Sokoudjou wa DFB Lioness walicaguliwa Wachezaji Bora (MVP wa mechi hizo na kupewa zawadi na wadhamini wa ligi hiyo inayosimamiwa na Chama cha Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (DB).