DK SAMIA AACHA KICHEKO KWA WAKAZI WA ARUSHA AKITOA TAARIFA UJENZI RELI YA SGR

*Azungumzia ujenzi VETA kuandaa vijana kuajiriwa,kujiajiri

*Aelezea maboresho yaliyofanyika katika sekta ya afya nchi kote

Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Arusha.

MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ameecha taarifa ya faraja kwa wakazi wa Mkoa wa Arusha baada ya kueleza serikali itajenga reli ya kisasa ya SGR kwa sababu ya kurahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa na watu.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara katika mkutano wa kuomba kura kuelekea uchaguzi Mkuu Oktoba 29,2025 amewaeleza wananchi kuwa kwasababu Arusha ni mji mkubwa lazima kutakuwa na kituo kikubwa cha reli. 

“Serikali inatarajia kujenga reli ya kisasa itakayoanzia Mkoa wa Tanga,Kilimankaro itapita hapa Arusha hadi Musoma mkoani Mara.Hapa Arusha Mjini kitajengwa kituo cha SGR hivyo kituo hicho kitaleta fursa za ajira kwa wafanyabiashara na vijana.

Kuhusu barabara ameeleza kuwa serikali itakamilisha miradi yote inayoendelea na ile mipya ambayo imeahidiwa katika ilani itakwenda kujengwa.

Ametaja miongoni mwa barabara hizo ni Malula – Ngarenanyuki ambayo imetengewa sh. bilioni 30 na barabara ya Tengeru – Mbuguni – Mererani yenye urefu wa kilometa 24 ambayo upembuzi yakinifu umekamilika hatua iliyobakia ni kutafuta mazabuni ili ujenzi uendelee.

Nyingine ni Mto wa mbu – Selela yenye urefu wa kilometa 23 ambapo mkataba unasubiri kusainiwa mkandarasi anze kazi, barabara nyingine ni Selela – Engaruka ambayo ina urefu wa kilometa 27 tayari upembuzi yakinifu umekamilika.

“Barabara ya Engaruka – Ngaresero kilometa 24 usanifu umekamilika kazi inayosubiriwa ni kutangaza zabuni apatikane mkandarasi aanze kujenga. Kwa upande wa Karatu kuna ujenzi wa lami kilometa 10 barabara ya Hotelii.

“Katika kuzidi kurahisisha biashara ya kikanda tutakiboresha kituo cha huduma kwa Pamoja mpakani eneo la Namanga kwa kuweka mashine za kisasa ili maroli ya bidhaa na watu wapiti kwa haraka na biashara zifanyike kwa haraka,” amesema.

Kuhusu sekta ya afya amesema hadhi za hospitali nchini zimeimarika zaidi kwani vimewekwa vifaa vya kisasa vikiwemo vipimo vyenye uwezo wa kupima saratani za matiti na anayebainika matibabu hatolazimika kwenda Ocean Road bali atatibiwa katika hospitali ya KCMC.

“Tumejenga bunker ya mionzi na inatibu kama wanavyotibiwa Ocean Road kwa hiyo wakazi wa Kanda ya Kaskazini hongereni sana.”

Kwa upande sekta ya elimu amesema Serikali imetumia Sh.bilioni 267 katika sekta ya elimu, lakini kimkoa imeendelea  kujenga VETA kila wilaya na wilaya ambayo haijapata VETA basi wakae mkao wa kupokea kwani lengo lao ni kujenga VETA kila wilaya na vyuo vya ufundi kila wilaya ili vijana waweze kupata ajira.

“Lengo la VETA hizi na vyuo vya ufundi ni kuwaandaa vijana waweze kujajiri na kuajirika kwani nimetaja miradi mikubwa inayopita huku.Kunq reli ya SGR inayokuja Arusha inataka mafundi waumeme, kuunganisha vyuma ili reli ikija ikute vijana wameshasomeshwa. 

“Tunakwenda na VETA na vyuo vya ufundi wilayani lakini kuna VETA ya mkoa kila mkoa tutajenga VETA kubwa.”

Aidha, amesema katika mradi wa elimu ya juu serikali iliamua kuanzisha matawi ya vyuo katika mikoa mbalimbali ili kurahisisha wanafunzi wanaofanya vizuri wapate elimu hiyo katika mikoa yao bila kulazimika kwenda vyuo vikuu maeneo yao.

Dk.Samia amesema pia Serikali itaendelea kujenga miundombinu ya elimu na kuhakikisha maslahi ya walimu, nyumba za walimu, vifaa vya kufundisha na kufundishia vinapatikana ili kukuza elimu nchini.

“Kama mnavyojua tumebadilisha mitaala ya elimu nasi tunajipanga kuendana na mabadiliko ya mitaala, vifaa vipatikane. Hata kwa wale wenye mahitaji maalum serikali imejipanga vizuri sana elimu yao sasa haina shida kuna mabweni kwa ajili yao vifaa vya kusomea tumejiandaa navyo. 

“Tanzania hatutaki kumuacha nyuma kwenye elimu, afya, upatikanaji maji safi, umeme kote hatutaki kumuacha mtu nyuma. Tumeyatekeleza malengo yale kwa kiasi kikubwa.”