Dkt. Samia Aahidi Kuimarisha Utalii na Michezo Arusha – Global Publishers

Arusha, Oktoba 2, 2025 – Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewaambia maelfu ya wananchi wa Arusha Mjini kuwa endapo atapewa ridhaa ya kuongoza kwa miaka mitano ijayo, serikali yake itaendelea kuwekeza zaidi katika sekta ya utalii na michezo ili kukuza uchumi na fursa za ajira.

Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Dkt. Samia alisema tayari serikali imeshapanua na kuboresha Kiwanja cha Ndege cha Arusha ambacho kuanzia Januari 2026 kitaanza kufanya kazi saa 24, hatua itakayoongeza watalii, kurahisisha usafiri na kuchochea biashara.

Shamra shamra za wananchi wa Arusha waliohudhuria mkutano wa hadhara wa Kampeni za Uchaguzi kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha tarehe 02 Oktoba, 2025.

Katika ahadi zake, alisema serikali yake itaunda Ukumbi mpya wa Kimataifa wa Mikutano wenye uwezo wa kukaa watu 6,000 kwa wakati mmoja, pamoja na hoteli na huduma za kisasa. Pia, alitangaza ujenzi wa Kituo cha Urithi wa Kijiolojia Ngorongoro-Lengai, kitakachovutia wanasayansi na watalii kutoka duniani kote.

Kuhusu michezo, Dkt. Samia aliahidi kukamilisha ujenzi wa Uwanja wa AFCON Arusha ifikapo Julai 2026, mradi ambao kwa sasa umefikia asilimia 63 ya utekelezaji. Uwanja huo utahusishwa na maendeleo ya Mji wa AFCON katika eneo la Bondeni City, utakaokuwa kivutio kipya cha michezo na utalii.

“Arusha ni kitovu cha utalii na michezo nchini. Serikali yangu itaendelea kuwekeza ili kuongeza thamani ya vivutio vyetu, kukuza fursa za biashara na kuboresha maisha ya wananchi,” alisema Dkt. Samia.

Mkutano huo ni muendelezo wa kampeni za CCM ndani ya mkoa wa Arusha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.