Dkt. Samia Amebarikiwa na Mungu, Atapata Miaka Mitano Tena – Global Publishers



Arusha, Oktoba 2, 2025 – Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Paul Makonda, amemwagia sifa Mgombea Urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisema hatakiwi kukatishwa tamaa kwa maneno ya wapinzani, kwani urais wake ni kwa mapenzi ya Mungu na atapewa ridhaa ya kuongoza tena kwa miaka mitano ijayo.

Akihutubia maelfu ya wananchi katika mkutano wa kampeni za CCM Jijini Arusha, Makonda alisema:

“Yapo maneno ya kukukatisha tamaa na kukuvunja moyo. Nakuhakikishia, umekaa kwenye kiti cha Urais kwa mapenzi ya Mungu, na Mungu atakupa tena miaka mitano ya kuendelea kuongoza Taifa letu la Tanzania.”

Makonda pia alimpongeza Dkt. Samia kwa kufanya kampeni zake binafsi bila kutegemea nguvu za mtu, akibainisha kuwa wapiga kura ndiyo “Godfather” wake halisi.

“Nimefurahi sana kukuona unazunguka mwenyewe na kutafuta kura zako. Huna Godfather, Godfather wako ni wapiga kura wa Tanzania ambao tayari wameonesha utayari wa kutiki jina lako,” alisema Makonda huku akishangiliwa na wananchi.

Kauli hiyo imeibua shangwe kubwa kwenye mkutano huo, ikiwa ni sehemu ya kuongeza hamasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.