EABC yaja na dawati la kidijitali kukuza biashara ya kuvuka mpakani

Arusha. Baraza la Biashara Afrika Mashariki (EABC) limezindua dawati la kidijitali la utoaji taarifa ili kusaidia wafanyabiashara wadogo wa mpakani kukabiliana na vikwazo visivyo vya kiforodha (NTBs).

Vikwazo hivyo ambayo vimetajwa kuwa changamoto kubwa za biashara za ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), vitaweza sasa kutatulika haraka baada ya utoaji wa Taarifa.

Uzinduzi huo, uliofanyika katika mpaka wa Taveta- Holili, uliambatana na mafunzo ya siku tatu yenye lengo la kujengea uwezo wafanyabiashara katika elimu ya fedha, usimamizi wa biashara na mbinu jumuishi za kijinsia katika biashara ya mpaka.

Akizungumza na waandishi wa habari, Afisa utafiti, sera na biashara ya bidhaa wa EABC, Gift Mbuya amesema mafunzo hayo yamewaleta pamoja zaidi ya wafanyabiashara 100 wa mazao ya nafaka, mbogamboga na matunda kutoka eneo hilo la mpaka.

Amesema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa “Kukuza Biashara ya kilimo-chakula ndani ya EAC kwa kukabiliana na vikwazo visivyo vya kiforodha.

“Mradi huu unalenga kuongeza ushiriki wa wanawake na vijana wafanyabiashara wa kilimo cha chakula na kuongeza wingi wa biashara ya mazao kama mahindi, mchele, maharage, soya na mazao ya bustani kupitia biashara za EAC”.

Mradi huu wa miaka mitatu (2025–2027), unaotekelezwa na EABC kwa ushirikiano na Shirika la Mapinduzi ya Kijani Afrika (AGRA), unalenga kuwawezesha takribani wafanyabiashara 2,440 wa mipaka yote ya EAC, hasa wanawake na vijana.

Aidha mradi unalenga kupunguza gharama na muda wa kufanya biashara kwa kuondoa NTBs, kuongeza uelewa wa matumizi ya vyombo vya urahisishaji biashara (STR), pamoja na kuanzisha madawati ya kidijitali ya taarifa za biashara mipakani.

Mradi huu umewezeshwa kwa ufadhili wa dola za Marekani 399,900 kutoka AGRA, ukiungwa mkono na Mastercard Foundation pamoja na Bill & Melinda Gates Foundation (BMGF).

Hapa nchini Utekelezaji wake unafanywa kwa kushirikiana na Chama cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) huku EABC ikiwa mratibu mkuu.

Naibu Mkurugenzi wa Uratibu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka Wizara ya Mambo ya EAC, Mary Maisory amesema licha ya kupunguzwa kwa ushuru wa forodha ndani ya jumuiya, bado vikwazo visivyo vya kiforodha ni vingi.

“Wafanyabiashara bado wanakabiliwa na ucheleweshaji wa mizigo, ukaguzi usio wa lazima, taratibu zisizoratibiwa na upungufu wa uelewa kuhusu nyaraka na viwango vya biashara,” amesema Maisory na kuongeza;

 “Kuwajengea wafanyabiashara uwezo na ujasiri kutawasaidia kuelewa Mpango Rahisi wa Biashara wa EAC (STR), taratibu za afya na usalama wa mimea na wanyama (SPS), viwango vya bidhaa na namna ya kuripoti na kutatua.”

Ameongeza kuwa kuondoa vikwazo visivyo vya kiforodha, kuimarisha miundombinu ya biashara mipakani, na kuhakikisha wanawake na vijana wananufaika ipasavyo na fursa za EAC ni msingi wa ukuaji wa uchumi wa jumuiya hiyo.

“Kuwawezesha wafanyabiashara wadogo wa mpakani si suala la kuongeza biashara pekee, ni suala la kubadili maisha, kuinua uchumi wa wananchi wetu na kuijenga Jumuiya ya Afrika Mashariki jumuishi na endelevu,”.

Maisory aliwahimiza washiriki kuyatumia mafunzo hayo kama nafasi ya kujifunza, kushirikiana na kuchukua hatua za dhati kwa maendeleo yao binafsi na ya nchi zao.

Mshiriki wa mafunzo hayo, Ester Mbaruku amesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu hasa kwa wafanyabiashara wadogo ambao wamekuwa wakipata vikwazo na kushindwa kusaidika haraka na mzigo kuharibika kutokana na kukosa pa kutoa taarifa.