Dar es Salaam. Ukosefu wa elimu ya masuala ya kisheria umetajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia baadhi ya watu kuchelewa au kushindwa kupata haki zao.
Kauli hiyo imetolewa jana Oktoba 2, 2025, jijini Dar es Salaam na wadau mbalimbali walioshiriki katika hafla ya uzinduzi wa kliniki ya msaada wa kisheria iliyozinduliwa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Akizungumza katika hafla hiyo, Dk Veronica Buchumi, Mratibu wa kliniki hiyo, amesema kuwa wananchi wengi hukosa uelewa wa taratibu za kisheria, jambo linalowafanya washindwe kuchukua hatua stahiki wanapokumbana na changamoto zinazohitaji msaada wa kisheria.
“Tupo katika jamii ambayo baadhi yao wanapopata changamoto hukimbilia kwa viongozi wa kisiasa sawa wanaweza kukusaidia, lakini wao pia watafuata utaratibu wa kisheria uliowekwa,” amesema.
Hivyo, ametoa wito kwa wadau wa sekta ya sheria kushirikiana kwa pamoja katika kutoa elimu kwa wananchi juu ya taratibu sahihi wanazopaswa kufuata, ili kupata msaada wa kisheria kulingana na changamoto wanazokumbana nazo.
“Kwa kufanya hivyo tutawasaidia wananchi kupata msaada kwa haraka hivyo kusaidia upatikanaji wa haki kwa haraka,” amesema.
Amesema uwepo wa kliniki za utoaji msaada wa kisheria ni muhimu kwani zinawasaidia wenye changamoto mbalimbali za kisheria kuweza kupata huduma hizo bila malipo.
“Hivyo inawasaidia hata wale wasioweza kumudu gharama za kulipa mawakili kusaidiwa kupata msaada wa kisheria na hivyo kustawisha upatikanaji wa haki kwa jamii,” amesema.
Vilevile kutoa elimu kwa jamii juu ya haki zao, jinsi ya kuzitambua na njia za kuzilinda.
“Watu wanaweza kushindwa kutafuta msaada kwa sababu hawajui haki zao au hawafahamu kwamba msaada upo. Kliniki zinasaidia kwa kutoa elimu na kuongeza uelewa,” amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa utoaji huduma kwa umma UDSM, Profesa Neema Mori amegusia umuhimu wa vyuo vikuu vinavyofundisha fani ya sheria kuanzisha kliniki za utoaji msaada wa kisheria.
Amesema pamoja na kusaidia kusogeza huduma hiyo kwa jamii pia zinasaidia wanafunzi kujifunza kwa vitendo na kuona uhalisia wa changamoto za kisheria zinazoikabili jamii.
“Kila mwanafunzi wa sheria anayeshiriki kwenye kliniki hupata uzoefu na uhalisia katika utendaji kwenye fani ya sheria kwa kusikiliza changamoto za watu, kushauriana juu ya kesi na kutoa huduma nyingine za kisheria inasaidia kufanya kwa vitendo kile alichojifunza,” amesema.
Wakili Mwandamizi wa Serikali, Edith Shekidole akiwakilisha Wizara ya Katiba na Sheria, amesema uwepo wa kliniki za msaada wa kisheria zinapanua wigo wa upatikanaji wa haki.
“Hivyo Wizara itaendelea kushirikiana na watendaji wa kliniki hizo kuhakikisha wananchi wenye mahitaji wanapata msaada wa kisheria bila malipo,” amesema.