Iringa. Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Kanda ya Kati, imewataka wananchi na wawekezaji mkoani Iringa kuhakikisha wanapata vibali halali kabla ya kujenga vituo vya mafuta, wakionya kuwa ujenzi holela utaibua athari kwa usalama wa watu na mazingira.
Wito huo umetolewa leo Oktoba 3, 2025 na Mhandisi wa Petroli wa EWURA Kanda ya Kati, Rose Mndeme, wakati wa kikao cha wadau wa sekta hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa VETA, Manispaa ya Iringa.
Rose amesema baadhi ya watu wamekuwa wakijenga vituo vya mafuta kiholela bila kufuata sheria, jambo linalohatarisha usalama na maisha ya watumiaji wa huduma hizo.
Ameeleza kuwa ujenzi wa kituo cha mafuta mjini unahitaji kibali chenye thamani ya Sh500,000 wakati wa vijijini ni Sh50,000 pekee, hivyo hakuna sababu ya kukwepa taratibu.
Aidha, amewataka wamiliki kuhakikisha wanakuwa na leseni ya uendeshaji wa vituo ambayo hudumu kwa miaka mitano, pamoja na bima ya kituo kwa ajili ya kujihami dhidi ya majanga.
“Kituo cha mafuta kinapaswa kuwa na akiba ya mafuta ya angalau siku tatu na kiwe kinanunua mafuta kutoka kwa wauzaji waliosajiliwa na Ewura tu,” amesema Rose
Vilevile, alisisitiza umuhimu wa kuweka bango la bei elekezi katika maeneo ya wazi ili kulinda haki za watumiaji na kudhibiti udanganyifu wa bei.
Rose ameonya kuwa Ewura haitasita kuchukua hatua za kisheria kwa wamiliki wa vituo watakaokaidi sheria, kanuni na taratibu za mamlaka hiyo.
Kikao hicho pia kilihusisha wadau wa mafuta kutoka wilaya mbalimbali za mkoa wa Iringa wakiwemo watoa huduma na wafanyabiashara wa sekta ya nishati.
Wadau hao walipata fursa ya kutoa maoni tofauti tofauti.
Mmoja wa washiriki kutoka Kilolo alisema elimu hiyo imekuja wakati muafaka kwani baadhi yao hawakuwa na uelewa wa kutosha juu ya masharti ya uendeshaji.
“Nimejifunza kuwa si kila mtu anaweza kujenga kituo cha mafuta bila kufuata utaratibu. Sasa nitarekebisha mipango yangu,” amesema Emmanuel Ndazi mkazi wa halmashauri ya Kilolo.
Mwingine kutoka Isimani alitaka Ewura kuongeza ukaguzi wa mara kwa mara kwa vituo vya mafuta ili kudhibiti wale wanaokiuka taratibu.
Ofisa Huduma kwa Wateja kutoka Ewura mkoa wa Iringa, Brenda Magoma, amesema elimu waliyoitoa itasaidia sana watumiaji na watoa huduma kuelewa haki na wajibu wao.
Brenda alisema lengo la Ewura si kuadhibu bali kuhakikisha huduma za nishati zinatolewa kwa usalama, ufanisi na kwa kuzingatia maslahi ya umma.
Alisema mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya uwazi, ushirikishwaji na uwajibikaji wa taasisi za umma kwa wananchi.
Viongozi wa vyama vya wafanyabiashara walioshiriki kikao hicho waliipongeza Ewura kwa kuwapa elimu muhimu inayowasaidia kufanya biashara kwa uhalali.
Pia walipendekeza mafunzo hayo yafanyike mara kwa mara katika wilaya nyingine ili kuwafikia wadau wengi zaidi.
Ewura imeeleza kuwa itashirikiana na Halmashauri, Jeshi la Polisi na mamlaka zingine kuhakikisha hakuna kituo kinachoanzishwa au kuendeshwa kinyume na sheria.
Mkaguzi Msaidizi, Msaidizi wa Udhibiti wa majanga ya moto Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Robert Myinga amesema amewaomba wahandisi kuanisha jengo litakuwaje na vitu vinginevyo vya muhimu.
Myinga amesema ujenzi holela unazuia zoezi la uzimaji moto kwa haraka.