Na Janeth Mesomapya
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetoa rai kwa wafanyabiashara wanaokusudia kuanzisha vituo vya mafuta kuhakikisha wanapata kibali cha ujenzi kutoka EWURA kabla ya kuanza ujenzi.
Rai hiyo imetolewa leo tarehe 3 Oktoba 2025, mkoani Iringa na Meneja wa Kanda ya Kati wa EWURA, Bi. Hawa Lweno, wakati wa mkutano na wadau wa sekta ndogo za mafuta, umeme na maji.
Bi. Lweno alisema kumekuwa na mwitikio mkubwa wa wafanyabiashara kufungua vituo vya mafuta hasa maeneo ya vijijini, lakini changamoto imeibuka pale ambapo baadhi yao huanza ujenzi bila kuwa na kibali cha EWURA.
“Natoa wito kwa yeyote mwenye nia ya kuanzisha kituo cha mafuta kuhakikisha kwanza anapata kibali kutoka EWURA kabla ya kuanza ujenzi. Kukiuka sharti hili la kisheria kutasababisha mfanyabiashara husika kutozwa faini ya shilingi milioni 20,” alisema.
Kibali hicho ni muhimu kwa kuwa kinatoa nafasi kwa wataalamu wa EWURA kuhakiki na kujiridhisha kwamba ujenzi wa kituo husika unazingatia viwango na masharti ya kiafya, kiusalama na kimazingira yaliyowekwa.
Kwa upande wake, mmoja wa washiriki wa mkutano huo, Bw. David Mlyapatali, alisema kikao hicho kimekuwa na manufaa makubwa kwani kimewapa uelewa zaidi kuhusu taratibu na wajibu wao katika kuendesha biashara hizo.