ZILE kelele za mashabiki wa Yanga kwamba hawamuelewi kocha wa timu hiyo, Romain Folz huku wakisisitiza wanataka aondoke kwani timu imepoteza utambulisho wa soka la kuvutia, jambo limekuwa jambo na muda wowote inaweza kutolewa taarifa kwa umma.
Tangu kuanza kwa kelele hizo, kulikuwa na makundi mawili ya viongozi, wapo waliokuwa wakimkingia kifua, wengine wakisikiliza wanachosema mashabiki na kuunga mkono. Hapo akatokea mmoja wa vigogo wa juu wa Yanga akasisitiza kocha huyo hawezi kutemwa ghafla namna hiyo. Lakini sasa, upepo umebadilika na Mfaransa huyo lolote linaweza kumtokea.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 35 aliyetua Jangwani Julai 2025, amekuwa katika shinikizo la kutakiwa atimuliwe kutokana na kushindwa kuwafurahisha mashabiki kwa timu kucheza soka la kawaida, licha ya kwamba hajapoteza mechi yoyote kati ya 10 alizoiongoza Yanga.

Timu hiyo imecheza mechi 10 zikiwamo tano za mashindano na nyingine kama hizo za kirafiki na kushinda tisa, sare ikiwa ni moja, ikifunga mabao 21 na kuruhusu mawili, lakini hiyo haijawa nafuu kwa Folz kwani suluhu ya jijini Mbeya dhidi ya Mbeya City, Septemba 30, 2025 imeongeza shinikizo la kutakiwa aondolewe.
Hata hivyo, awali ilionekana kama angesalimika baada ya baadhi ya viongozi wa Yanga kumtetea, lakini kundi la mabosi wasiotaka kuona kocha Romain Folz anasalia klabuni hapo ni kama linaanza kukaribia kupata ushindi baada ya kuanza kwa mchakato wa siri kutafuta mrithi wake.
Taarifa kutoka ndani ya Yanga zinasema, kundi la mabosi wanaokubaliana na uamuzi wa kufanya mabadiliko kwa benchi la ufundi limezidi kupata wanaounga mkono huku presha ya msako mpya ukianza kimya kimya.

Kwa siri sana Yanga iko sokoni ikitafuta kocha mpya, atakayekuja kuchukua nafasi ya Mfaransa huyo mchakato ambao unafanyika kwa uficho mkubwa.
Bosi mmoja wa juu kutoka ndani ya Yanga ameliambia Mwanaspoti, presha kubwa inatokana na mashabiki wengi kutokukubaliana na mbinu za kocha huyo.
Hatua hiyo mabosi wanaona kama itaiathiri timu hiyo lakini pia itawaathiri wadhamini mbalimbali wa klabu hiyo ambao hatua ya mashabiki hao kukosa furaha itapunguza soko la biashara zao.
Tayari zimeshaanza kupigwa hesabu za namna ya kusitisha mkataba wa Folz kabla ya kocha huyo kuitwa mezani kisha kumalizana na uongozi wa klabu hiyo.

“Hali sio nzuri sana, ni kweli unaweza kusimama na matokeo, lakini huko nje wafuasi wetu wengi hawana raha, sasa hizo kelele sio za kuzifumbia macho zina maana yake.
“Kutafanyika mabadiliko, ambayo yanatokana na kutuliza hiyo hali lakini pia tusiathiri biashara ya wadhamini wetu, unajua watu wakiwa na furaha ndio wakati unaweza kufanya biashara. Mfano hivi juzi unaona kuna jezi mpya zimekuja, lakini zinaingia sokoni nyakati ambazo watu hawana furaha na timu sio rahisi watu kukimbilia kitu hicho hata kama wanakipenda.
“Tunatafuta kocha kwa akili lakini hatutamuacha kocha mpaka tupate mtu sahihi ambaye atakuja kuendelea hapa alipoishia Folz,” amesema bosi huyo.

Yanga inataka kocha huyo aje haraka kuanza kusuka kikosi hicho, kabla ya kuendelea na mechi za mashindano ambapo timu hiyo itarudi uwanjani Oktoba 18, 2025 ikiwa ugenini kuumana na Silver Strikers ya Malawi katika mechi ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika hatua nyingine, Folz anakuwa kocha wa pili ndani ya Yanga kwa miaka ya karibuni kudondosha pointi katika mechi mbili za mwanzo wa Ligi Kuu Bara baada ya Mkongomani, Mwinyi Zahera.
Kwenye Ligi Kuu, alianza kwa kuifunga Pamba Jiji mabao 3-0, kisha matokeo ya 0-0 dhidi ya Mbeya City.
Matokeo hayo yamemfanya kushindwa kufikia matawi ya watangulizi wake na badala yake kufuata rekodi ya Zahera ya kuangusha pointi mbili ndani ya mechi mbili za kwanza.
Katika mechi mbili za kwanza kwenye ligi, Yanga ilikuwa haijawahi kupoteza wala kutoka sare tangu msimu wa 2020/21, chini ya kocha Mwinyi Zahera, ambapo ilitoka na alama moja, baada ya kufungana mabao 3-3 dhidi ya Polisi Tanzania.
Tangu wakati huo Yanga imefundishwa na makocha wanne kabla ya Folz, huku wawili kati yao ambao ni Sead Ramovic na Miloud Hamdi wakianzia katikati ya msimu.

Makocha ambao wameanza na timu hiyo mwanzo wa msimu ni Nasreddine Nabi na Miguel Gamondi, ambao rekodi zao zinafanana kwani hawakuangusha pointi ndani ya mechi mbili za mwanzo.
MWINYI ZAHERA (2020-2021)
RuvuShooting 1-0 Yanga
Polisi TZ 3-3 Yanga
NASREDINNE NABI
2021-2022
Yanga 1-0 Mbeya City
Kagera 0-1 Yanga
2022-2023
Polisi TZ 0-1 Yanga
Coastal 0-1 Yanga
MIGUEL GAMONDI
2023-2024
KMC 0-5 Yanga
Yanga 0-5 Tabora United
2024-2025
Kagera 0-2 Yanga
KenGold 0-1 Yanga