Fufuni yakata unyonge Ligi Kuu Zanzibar

TIMU ya Fufuni kutoka Pemba, imekataa unyonge baada ya kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Kipanga katika Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), mechi ikichezwa Oktoba 2, 2025 kwenye Uwanja wa Mao A kisiwani Unguja.

Ushindi huo wa Fufuni unaifanya kuwa timu pekee kati ya nne zilizopanda daraja kucheza Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) msimu huu 2025-2026, kuanza na ushindi baada ya nyingine tatu kupoteza mechi zao za kwanza.

Timu hizo nne zilizopanda daraja ni Polisi na New King za Unguja, wakati Fufuni na New Stone Town zikitokea Pemba.

Polisi ilianza kupokea kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Uhamiaji katika mechi ya kwanza ya ufunguzi wa ligi iliyochezwa Septemba 25, 2025 kwenye Uwanja wa Mao A, Mjini Unguja.

New King ilikaribishwa kwenye ligi na Mwembe Makumbi kwa kichapo cha mabao 3-1, mechi iliyochezwa Septemba 29, 2025 kwenye Uwanja wa Mao A, huku Mafunzo ikiisulubu New Stone kwa kuifunga mabao 4-0. Hii imeweka rekodi ya kufungwa mabao mengi tangu kuanza kwa msimu huu.

Kocha Mkuu wa Fufuni, Suleiman Mohammed, amesema siri ya kutoboa ni timu hiyo kufanya mashambulizi ya haraka kwa wapinzani na kulinda kuhakikisha hawatoi mwanya wa kuingia eneo lao.

Amesema msimu huu wa kwanza lengo ni kuhakikisha timu haishuki daraja na ushindi huo unaleta taaswira njema kwao.

Naye Kocha Msaidizi wa Kipanga, Adam Ali Simai, amesema alitambua tangu awali kuwa mechi hiyo itakuwa ngumu kwa sababu ya ari ya timu pinzani kucheza baada ya kupanda daraja ili kuonesha walichonacho.

Pia, amesema mabao waliyoruhusu ni uzembe wa mchezaji mmoja lakini imeigharimu timu kwa kupoteza pointi tatu za raundi ya kwanza.

“Wapinzani walitumia udhaifu wa kupeleka mashambulizi kwa kutumia mipira ya chini baada ya kutuona hatuko vizuri katika eneo hilo na wachezaji kupoteza umakini,” amesema. 

Mchezo huo ulivutia mashabiki kwa mbwembwe za Kocha wa Fufuni na mchezaji Zubeir Yahya mwenye uwezo wa kukimbia akiwa na mpira, kutoa pasi zenye muelekeo mzuri kwa wenzake na kumfika mpinzani haraka pindi anapopoteza mpira.

Zubeir anaonekana kuitumia falsafa ya ‘keep the ball down’ kwa sababu ya kuwa na uwezo wa kumiliki mpira, kuutembeza kwa muda mrefu na  kufanya uamuzi sahihi ambapo sio wachezaji wengi wanaweza kuitumia falsafa hiyo lakini kwake imeonekana.