Huyu hapa kocha mpya Simba, mwenyewe atia neno

TAKRIBANI siku kumi za Simba kukaa bila ya kocha mkuu, zimeleta majibu ya kupatikana mrithi wa Fadlu Davids ambaye rasmi ataanza kazi Jumatatu kukinoa kikosi hicho.

Tangu Septemba 22, 2025 Fadlu alipoaga rasmi anaondoka Simba, klabu hiyo iliingia kwenye mchakato wa kumsaka mrithi wake ambaye tayari amepatikana na leo Oktoba 3, 2025, ameagwa huko alipokuwa akifundisha huku kesho Oktoba 4, 2025 akitarajiwa kutua Dar.

Kwa mujibu wa taarifa za uhakika ndani ya Simba, viongozi wa timu hiyo wamemalizana na aliyekuwa kocha wa Gaborone United raia wa Bulgaria, Dimitar Pantev mwenye Umri wa miaka 49.


Kocha huyo anatarajiwa kuingia nchini muda wote kuanzia sasa kujiunga na Simba na kuanza rasmi kazi ya kukinoa kikosi hicho siku ya Jumatatu ambapo wachezaji watakuwa wanarudi kambini kutoka mapumziko mafupi baada ya kucheza mechi ya ligi dhidi ya Namungo.

“Tumepata kocha kijana ambaye tunaamini ataendana na mipango ya klabu, tumekuwa na vikao naye kadhaa kwa njia ya mtandao na hata ana kwa ana, hivyo tumekubaliana mambo kadhaa ikiwemo kuhakikisha timu inafanya vizuri katika mashindano ya kimataifa pamoja na ndani,” kilibainisha chanzo chetu ndani ya Simba.

Mbali na kiongozi huyo ambaye hakutaka kuwekwa wazi jina lake, Mwenyeki wa Bodi ya Klabu ya Simba, Crescentius Magori, amenukuliwa na mmoja wa waandishi wa habari huko Nigeria akisema: “Yeye (Pantev) ni kocha mzuri na timu yake Gaborone United, licha ya kutolewa kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ilituonyesha mchezo mzuri sana. Ni kweli tupo kwenye mazungumzo naye, lakini si yeye peke yake. Bado kuna majina mengine mezani.”


Pantev ameaga huko Botswana na uongozi wa Gaborone United kupitia Mkurugenzi wa michezo, Nicholas Zakhem ameonyesha kusikitishwa na uamuzi wa kocha huyo ambaye walikuwa na malengo naye msimu huu.

“Imekuwa ghafla na tumekuwa na mipango naye tangu msimu uliopita na hatuwezi kuficha juu ya kazi nzuri na kubwa ambayo alifanya hadi kuchukua ubingwa wa ligi hatuna budi kukubaliana na kilichotokea ndio maisha ya mpira yalivyo,” amesema kiongozi huyo.

Alipotafutwa na Mwanaspoti, kocha huyo amethibitisha kumalizana kwa amani na Gaborone huku akimtaka mwandishi kusubiri hadi pale ambapo kila kitu kitakuwa sawa ili kuongea hilo kwa undani.

“Kwa kazi yetu ya ukocha ni kawaida leo unaweza kuwa hapa na kesho pale, Simba ni moja ya timu kubwa Afrika hilo lipo wazi kuhusu kufanya nao kazi kocha yoyote anaweza kuvutiwa nao,” amesema kocha huyo.


Kabla ya kwenda Botswana kwa mujibu wa taarifa inaelezwa kuwa kocha huyo alikuwa kuwa na mazungumzo na aliyekuwa kocha wa Yanga, Luc Eymael na kuhitaji kujua zaidi kuhusu soka la ukanda wa Afrika Mashariki, inaelezwa kuwa wawili hao wanafahamiana.

Kwa mujibu wa ratiba, kocha huyo anatarajiwa kutua Tanzania kesho Oktoba 4, 2025 kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kujiunga na Simba.