Shirikisho la Soka nchini (TFF) limemchukulia hatua kali mchezaji wa Young Africans, Ibrahim Abdullah, baada ya kumpiga rafu mbaya mchezaji wa Mbeya City, Ibrahim Ame, kitendo kilichotajwa kuwa cha kuhatarisha usalama wa wachezaji.
Kwa mujibu wa Kanuni ya 41:21 ya Ligi Kuu, Abdullah amefungiwa mechi tano (5) mfululizo, adhabu ambayo ni pigo kwa Yanga inayopambana kutetea ubingwa wake.
Si hilo tu – mwamuzi wa kati, Omary Mdoe kutoka Tanga, ameondolewa kwenye orodha ya waamuzi kwa mizunguko mitano (5) kwa kushindwa kutafsiri na kusimamia sheria za mpira ipasavyo katika mchezo huo.
Tukio kubwa lililotajwa ni dakika ya 46 ambapo mchezaji wa Mbeya City, Matheo Anthony, alishika mpira ndani ya eneo la penati, lakini mwamuzi hakuona kosa. Aidha, hakuchukua hatua stahiki kwa rafu mbaya ya mapema dakika ya 3 iliyochezwa na Abdullah.
Hivyo, TFF imesisitiza kuwa hatua hizi ni sehemu ya kuhakikisha nidhamu, usawa na ulinzi wa wachezaji vinadumishwa katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Related