Ishu ya kocha mpya Simba, uongozi wafunguka

Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amewataka mashabiki wa timu hiyo kuwa na subira juu ya hatima ya benchi lao la ufundi baada ya kuondokewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids.

Ally amesema kuwa mchakato wa kumsaka Kocha Mkuu mpya unaendelea hivyo mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo hawapaswi kuwa na presha.

Amesema kuwa wakati wakiwa wanasaka kocha mpya, timu inaendelea na program zake kama kawaida na kuhusu Kocha Mkuu mpya, wakae mkao wa kula.

SIMB 01


“Kwa sasa tupo kwenye mapumziko kupisha Kalenda ya FIFA, Lakini vijana wetu watarejea mazoezini hivi punde kuanza maandalizi ya mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Swali kuu ni Kocha Mkuu!! Niwaombe Wana Simba tuwape nafasi viongozi wetu wakamilishe mchakato huo kwani mambo mazuri hayataki haraka.

“Tuutimie Wakati huu wa mapumziko, kuendelea kununua Jezi Original za timu yetu,” amesema Ahmed Ally.

SIMB 02


Fadlu Davids aliachana na Simba baada ya mchezo wa ugenini wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United ambayo Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0.

Kuondoka kwa Fadlu kulifungua mlango kwa Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’ kuinoa kwa muda katika mechi ya marudiano iliyochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ambayo ilimalizika kwa sare ya bao 1-1.

SIMB 03


Hata hivyo katika Ligi Kuu, Simbe imekuwa ikisimamiwa na Selemani Matola ambaye amekuwa akihudumu kama Kocha Msaidizi wa timu hiyo.

Kwa mujibu wa tetesi, Kocha anayewepewa nafasi kubwa ya kurithi mikoba ya Fadlu Davids ni Dimitar Pantev ambaye anainoa Gaborone United.