Jamii iwekeze kuutua mzigo wa magonjwa yasiyoambukiza

Dar es Salaam. Magonjwa yasiyoambukiza kama vile kisukari, shinikizo la damu, magonjwa ya moyo, saratani na matatizo ya kupumua, yamekuwa tishio kubwa kwa afya ya jamii ya kisasa.

Tofauti na magonjwa ya kuambukiza, haya hayapitishwi kutoka mtu mmoja hadi mwingine, bali mara nyingi husababishwa na mtindo wa maisha, lishe duni, ukosefu wa mazoezi na matumizi ya tumbaku au pombe.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza kuwa magonjwa haya husababisha vifo vya watu milioni 41 kila mwaka duniani kote, sawa na asilimia 74 ya vifo vyote.

Kwa Afrika, mzigo huu unazidi kuongezeka kwa kasi. Ripoti ya WHO mwaka 2022 ilibaini kuwa ifikapo mwaka 2030, magonjwa yasiyoambukiza yatakuwa yanasababisha vifo vingi zaidi barani humo kuliko magonjwa ya kuambukiza. Hii ni hali inayotoa taswira ya hatari kubwa iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa.

Kwa hiyo, jamii sasa haina budi kuutua mzigo huu kupitia elimu ya umma, kampeni shuleni na katika nyumba za ibada na maeneo mengine kadri inavyowezekana.

Magonjwa yasiyoambukiza hayana tiba rahisi, na mara nyingi huhitaji matibabu ya kudumu. Mfano, mtu mwenye kisukari atahitaji kudhibiti sukari yake kila siku kwa maisha yake yote. Gharama za dawa, vipimo na matibabu huchosha familia na mifumo ya afya.

Kwa mujibu wa taarifa za Benki ya Dunia za mwaka 2021, gharama za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja za  magonjwa haya,  zinakadiriwa kufikia zaidi ya Dola za Marekani trilioni mbili kwa mwaka duniani.

Hali hii inasababisha umasikini zaidi kwa familia maskini, kwani sehemu kubwa ya kipato huishia kwenye matibabu.

Jamii ikijitokeza pamoja katika kuzuia na kupunguza hatari ya magonjwa haya, itapunguza gharama kubwa za kiafya na kuimarisha ustawi wa kijamii na kiuchumi.

Elimu sahihi ni ngao ya kwanza ya kupunguza magonjwa haya. Uelewa mdogo kuhusu hatari za ulaji wa vyakula vya mafuta na sukari nyingi, madhara ya uvutaji sigara au kutofanya mazoezi, huchangia ongezeko la wagonjwa.

Jamii inapaswa kuwekeza katika vipindi vya redio na televisheni vinavyofundisha lishe bora na umuhimu wa mazoezi. Uwepo wa mabango na vipeperushi kwenye vituo vya afya vinavyofafanua madhara ya shinikizo la damu au kisukari.

Mitandao ya kijamii itumike kusambaza ujumbe wa kinga kwa vijana, ambao wako kwenye hatari ya kuiga mitindo mibaya ya maisha.

Mfano wa mafanikio ni kampeni ya afya nchini Rwanda, ambapo  jamii  zilielimishwa kuhusu ulaji wa mboga na matunda  na hivyo kuongeza matumizi yake kwa asilimia 20 katika miji mikuu kati ya mwaka 2015–2020.

Watoto na vijana walio shuleni ndio taifa la kesho. Tabia nzuri zikijengeka mapema, huzuia matatizo makubwa ya kiafya baadaye.

Ripoti ya Shirika la Watoto Duniani (Unicef)  ya mwaka 2023 iitwayo: Healthy weight in childhood,  inaonyesha kuwa karibu asilimia 40 ya watoto  wa chini ya miaka mitano barani Afrika,  wanakula chakula chenye sukari nyingi kuliko inavyopendekezwa, jambo linaloongeza unene na hatari ya kisukari mapema.

Kampeni shuleni zinaweza kujikita katika kufundisha somo la lishe na afya ya mwili kama sehemu ya mitalaa, kukuza michezo shuleni na kuhamasisha wanafunzi kushiriki angalau dakika 60 za shughuli za kimwili kila siku na kupiga marufuku uuzaji wa soda na vyakula vya mafuta ndani ya shule.

Nyumba za ibada ziwe vituo vya mabadiliko

Nyumba za ibada zina nafasi ya kipekee kwani hukusanya idadi kubwa ya watu mara kwa mara na kuwa na ushawishi mkubwa kwa jamii.

 Viongozi wa dini wanaweza kutumia nafasi hii kufundisha waumini kuhusu afya njema, kwani afya bora pia ni sehemu ya maisha ya kiroho. Mikakati inayoweza kutekelezwa ni mahubiri yanayogusia umuhimu wa kujali miili yetu kwa kuepuka sigara, pombe na ulaji duni.

Nyumba za ibada kushirikiana na wataalamu wa afya kuendesha vipimo vya bure vya shinikizo la damu na sukari.

Ushirikiano kati ya Serikali na jamii

Ingawa elimu ni muhimu, sera za kitaifa pia zina nafasi kubwa. Serikali ikishirikiana na jamii zinaweza kupunguza magonjwa haya kupitia kuweka kodi kubwa kwa bidhaa hatarishi kama tumbaku na soda; uwekezaji wa ujenzi wa bustani na viwanja vya michezo vinavyohamasisha wananchi kufanya mazoezi.

Kwa mfano, Afrika Kusini ilipoanzisha ushuru wa sukari mwaka 2018, utafiti wa British Medical Journal (2021) ulionyesha ulipunguza ununuzi wa vinywaji vyenye sukari kwa asilimia 28.

Jamii sasa haina budi kuungana na kupaza sauti. Kama anavyosema mtaalamu mmoja wa afya ya umma: “Magonjwa yasiyoambukiza siyo matokeo ya chaguo la mtu mmoja, bali ya mifumo ya kijamii. Hivyo, lazima jamii nzima ishikamane kuyakabili.”

Kuanzia familia hadi taasisi, kila mmoja ana nafasi ya kubeba jukumu hili. Tukichukua hatua leo, tutajenga taifa lenye afya, nguvu na matumaini ya kesho.