Kisa kufika uwanjani bila jezi, Junguni yapigwa faini

BODI ya Ligi Kuu Zanzibar, imeitoza Junguni United faini ya Sh200,000 kwa kuchelewa uwanjani kisha kufika bila ya kuwa na jezi na kusababisha mwamuzi kuvunja mechi.

Mechi hiyo ilipangwa kuchezwa Septemba 26, 2025 kati ya Junguni na Zimamoto kwenye Uwanja wa Gombani uliopo kisiwani Pemba saa 10:00 jioni lakini ulilazimika kuvunjwa baada ya timu hiyo kuchelewa na kufika uwanjani bila ya jezi.

Kwa mujibu wa ripoti ya kamisaa wa mechi hiyo, Junguni ilifika uwanjani ikiwa haina jezi za kuvaa, ambapo waamuzi waliwasubiri hadi saa 10:35 jioni, wakalazimika kuvunja mechi.

Taarifa iliyotolewa na Mjumbe wa Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF), Ali Juma Khamis, imeeleza kwamba, kwa mujibu wa kanuni za kuendesha mashindano Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), kifungu namba 15 kanuni ya saba, Junguni imepoteza mechi hiyo na Zimamoto kupewa ushindi wa pointi tatu na mabao mawili.

Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) inayoshirikisha timu 16, msimu huu 2025-2026 ilianza Septemba 25, 2025 na inatarajiwa kuendelea leo Oktoba 3, 2025 KMKM ikiikaribisha Mlandege kwenye Uwanja wa Mao A, Unguja saa 10:15 jioni.