Massawe Kaimu Mkurugenzi mpya TPSF, uteuzi wa Maganga wasimamishwa

Dar es Salaam. Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) limemteua, Deogratius Massawe kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF akichukua nafasi ya Raphael Maganga ambaye uteuzi wake umesimamishwa.

Massawe ambaye aliwahi kuhudumu kama Mkurugenzi wa Idara ya Fedha TPSF anakalia kiti hicho akikamilisha safari ya siku 609 alizohudumu Maganga tangu alipoteuliwa kuwa Mkurugenzi wa TPSF Februari Mosi 2024.

Taarifa iliyotolewa leo na Rais wa TPSF, Angelina Ngalula inaeleza kuwa Massawe anakaimu nafasi hiyo kuanzia leo Oktoba 3, 2025 bila kueleza sababu za kutolewa kwa Maganga.

Massawe ni mchumi, mtaalamu wa fedha na sera akiwa na Shahada ya Uzamili ya Biashara katika Uhasibu, Shahada ya Kwanza ya Forodha na Usimamizi wa Kodi, Diploma ya Kitaaluma katika Viwango vya Kimataifa vya Uhasibu wa Sekta ya Umma (IPSAS).

Pia Massawe ni Mhasibu wa Umma aliyesajiliwa (CPA) na mkufunzi wa fedha aliyeidhinishwa (CFE), anachukua nafasi hiyo akiwa na uzoefu katika sekta ya ushauri kwa mashirika yasiyo ya kiserikali na sekta binafsi.

“Massawe aliwahi kuhudumu kama Mkuu wa Idara ya fedha  TPSF. Anakuja na hazina kubwa ya uzoefu katika uongozi wa kifedha, upangaji mkakati na maendeleo ya taasisi uwezo muhimu katika kuendelea kuimarisha nafasi ya TPSF kama sauti ya sekta binafsi nchini Tanzania,” imeeleza taarifa hiyo ya Ngalula.