Unguja. Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya NCCR Mageuzi, Laila Rajab Khamis amesema iwapo akichaguliwa atamaliza tatizo la ajira, kuimarisha huduma za afya na biashara Zanzibar.
Laila ametoa kauli hiyo leo Oktoba 3, 2025 wakati chama hicho kikizindua kampeni zake katika viwanja vya Nego Kibanda Maiti Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amesema iwapo wakiingia madarakani watahakikisha afya inaimarika kwa kusomesha watoto wa Kizanzibari kuwa mabingwa. Ameongeza kuwa kuna tatizo kubwa na sugu la ajira, lakini baada ya NCCR kuingia madarakani watajenga viwanda vingi kuhakikisha wanamaliza kabisa tatizo hilo.
Amesema ndani ya siku 100 baada ya kuingia madarakani, akichaguliwa atahakikisha wanajenga soko zuri kuliko masoko yote yaliyopo Unguja na kurejesha mikopo.
Awali, mgombea mwenza wa Chama hicho wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Eveline Munisi amesema lengo lao ni kuleta mageuzi katika sekta zote za Tanzania.