BAADA ya kuwepo kwa taarifa za Kocha Mkuu wa Gaborone United, Dimitar Pantev kufikia makubaliano ya kusaini mkataba wa kuiongoza Simba, mapema leo asubuhi ameaga rasmi.
Kuaga kwa kocha huyo raia wa Bulgaria, kunamfanya kuanza maandalizi ya kutua Dar es Salaam wikiendi hii tayari kujiunga na Simba.
Taarifa iliyotolewa na Gaborone United imesema: “Klabu ya Gaborone United inapenda kutoa taarifa rasmi kuwa Kocha Mkuu Dimitar Pantev ataondoka klabuni mara moja.
“Kocha Pantev ameijulisha klabu nia yake ya kuanza safari mpya katika taaluma yake ya ukocha, na baada ya mazungumzo na uongozi, Gaborone United imekubali kwa heshima ombi lake hilo. Asubuhi ya leo, Kocha Pantev ameaga wachezaji na benchi la ufundi katika uwanja wa mazoezi wa klabu.

“Tangu alipoungana na klabu, Kocha Dimitar Pantev amekuwa nguzo ya uongozi, weledi na mafanikio. Chini ya uongozi wake, Gaborone United ilibeba taji lake la kihistoria la nane katika Ligi Kuu ya Botswana msimu wa 2024-2025, mafanikio yaliyoweka jina lake kwenye historia ya klabu.
“Kwa niaba ya bodi ya wakurugenzi, benchi la ufundi, wachezaji, wafanyakazi na familia nzima ya Gaborone United, tunatoa shukrani za dhati kwa Kocha Pantev kwa mchango wake na kujitolea kwake bila kuyumba. Urithi wake utaendelea kuwa sehemu ya hadithi yetu ya fahari.

“Tunamtakia kila la heri katika ukurasa mpya wa maisha yake na mafanikio zaidi katika safari yake ya ukocha.
“Kuhusu nafasi iliyoachwa wazi, klabu itatoa taarifa kwa wakati muafaka.”

Pantev anatua Simba kuchukua nafasi iliyoachwa na Fadlu Davids ambaye aliaga rasmi Septemba 22, 2025 baada ya kupata dili la kwenda kuifundisha Raja Casablanca ya Morocco.