Gaza. Mjukuu wa Rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela, Nkosi Zwelivelile Mandla amekamatwa na majeshi ya Israel akiwa katika harakati za kutoa msaada wa kibinadamu kwa wakazi wa Gaza kupitia meli ya Global Sumud Flotilla.
Mandla, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Umtata huko Afrika Kusini, alikamatwa pamoja na mamia ya wanaharakati kutoka mataifa mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuvunja vizuizi vya baharini vinavyowekwa na Israel kwa Gaza.
Mandla Mandela alikamatwa akiwa kwenye meli ya Marinette, ambayo ilikuwa na lengo la kufikisha misaada ya chakula, dawa, na vifaa vya matibabu kwa watu wa Gaza. Majeshi ya Israel yalivamia meli hiyo katika maji ya kimataifa, na kumtia nguvuni Mandla pamoja na wanaharakati wengine.
Wakati wa tukio hilo, Mandla ameeleza kupitia mitandao ya kijamii kuwa “Nimekamatwa kwa nguvu na kutolewa kwa mabavu kutoka kwenye meli,” amesema.
Naye Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, amelaani vikali kitendo hicho, amesema kuwa “Huu ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa hivyo Israel inapaswa kuachilia huru wanaharakati wote waliokamatwa,” amesema Ramaphosa.
Ramaphosa ameongeza kuwa tukio hilo linadhihirisha ukosefu wa kuheshimu haki za binadamu na juhudi za kimataifa za kupatia suluhu mgogoro wa Gaza.
Mandla Mandela ni mmoja wa wanaharakati maarufu wa haki za binadamu na amekuwa mstari wa mbele katika kupigania haki za Wapalestina. Katika mahojiano ya awali, Mandla alieleza kuwa “hali ya Wapalestina chini ya utawala wa Israel ni mbaya zaidi kuliko ile ya Waafrika Weusi wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi (apartheid) nchini Afrika Kusini.”
Tukio hili limezua hasira na maandamano makubwa katika mataifa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Italia, Hispania, Ufaransa, na Brazil, ambapo wananchi wamejitokeza kuonyesha mshikamano na wanaharakati waliokamatwa na kupinga vitendo vya Israel dhidi ya misaada ya kibinadamu.
Hadi sasa, Israel haijatoa tamko rasmi kuhusu hatua itakazochukua kwa Mandla Mandela na wanaharakati wengine waliokamatwa. Hata hivyo, serikali ya Afrika Kusini inaendelea na juhudi za kidiplomasia kuhakikisha kuwa wanaharakati hao wanaachiliwa huru haraka iwezekanavyo.
Kwa sasa, Mandla Mandela anashikiliwa katika jela ya Ashdod, na inatarajiwa kuwa atafikishwa mahakamani au kuhamishiwa katika kituo cha uhamiaji kwa ajili ya mchakato wa kumrejesha nchini mwake.