TFRA YATOA ELIMU YA MATUMIZI SAHIHI YA MBOLEA NJOMBE

………………………. 

Kuelekea msimu
mpya wa kilimo mwaka 2025/2026 kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Mamlaka ya
Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imeendesha mafunzo ya matumizi sahihi ya
mbolea kwa wakulima wa Mkoa wa Njombe, kata ya Makowo, ili kuongeza tija na
uzalishaji.
 

Mafunzo hayo
yaliyoanza kutolewa katika kijiji na Kata ya Makowo leo tarehe 2 Oktoba,
2025  yanalenga wakulima wa mazao
mbalimbali yakiwemo ya kibiashara kama Viazi, Mahindi, Parachichi na Chai.
 

Akizungumza
wakati wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent, amesema
elimu hiyo inalenga kuwajengea uwezo wakulima juu ya matumizi sahihi ya mbolea
za kupandia, kukuzia na kubebeshea, ili kuepuka hasara na mavuno hafifu
kutokana na kutokuzingatia matumizi sahihi ya mbolea. Matumizi sahihi ya mbolea
yanaenda sambamba na utambuzi wa afya ya udongo na matumizi ya visaidizi vya
mbolea.
 

Hata hivyo
Mkurugenzi Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) ameahidi kupeleka
kifaa cha upimaji afya ya udongo (Soil Scanner) Halmashauri ya Njombe mji ili
kuwawezesha wataalamu kubaini mahitaji halisi ya udongo na kushauri aina bora
ya mbolea kwa wakulima.
 

Kwa upande wake,
Bwana Shamba wa kampuni ya mbolea ya OCP, Joshua Joel, amewataka wakulima
kutumia mbolea kwa kuzingatia upatikanaji na zinazowawezesha kupunguza gharama
za uzalishaji huku kampuni ikiwahakikishia wakulima kufikishia pembejeo hizo
kwa wakati.
 

Wakulima
walioshiriki mafunzo hayo, akiwemo Agnes Mgaya, Costa Abeck na Sabas Mwalongo,
wameshukuru kwa kupewa elimu ya mbolea na kueleza imewapa mwanga mkubwa kwani
awali walikuwa wakichanganya mbolea zaidi ya moja bila kufuata utaratibu wa
kitaalamu jambo lililowapotezea rasilimali fedha.
 

Aidha,
wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwapa mbolea za
ruzuku zilizopunguza gharama kubwa za uzalishaji na kueleza wanazipata kwa
wakati katika maeneo yao.

Kwa upande wake,
Mwenyekiti wa kijiji cha Makowo, Sabas Mwalongo, amewasisitiza wakazi wa eneo
hilo kuhakikisha wanayafanyia kazi mafunzo waliyopewa ili yaweze kuwasaidia
kufanya uzalishaji wenye tija kwa zao la viazi kwa kuwa ndiyo uchumi wa
wananchi wa kata ya Mkowo.

Ameishukuru
Serikali kwa kuwezesha mafunzo hayo kufanyika katika kijiji cha Makowo na
Marimba, huku akiomba zoezi hilo liwe endelevu.